Neno La Mungu Linatupa Kujua Aliyepitia Jaribu Fulani Aliwezaje Kulivumilia na Kulishinda Hilo Jaribu.
Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana wetu Yesu Kristo ametupa kibali cha kuiona tena. Ni Neema kubwa sana kupata kibali mbele za Mungu, tunapaswa kumshukuru Mungu kwa uweza wake.
Unapoambiwa biblia ina majibu ya kila kitu usifikiri watu wanaipa sifa ili watu wapate kuhamasika na kuisoma. Ukiona unawaza hivyo ujue ipo vita ndani yako inayokufanya uendelee kuwa mzembe wa kutokusoma Neno la Mungu.
Neno la Mungu limebeba kila kitu cha maisha ya mwanadamu, majaribu yote unayopitia leo sio mambo mageni. Unaweza kuona kama vile unapatwa na jambo jipya kumbe walishapita wenzako siku nyingi sana.
Ikiwa ni kukosa mtoto tunamsoma Elisabeth mama yake na Yohana mbatizaji, alikuwa tasa wa miaka mingi sana mpaka anafikia uzee wake alikuwa hajawahi kupata hata ule ujauzito wa kusema uliingia na kuharibika. Lakini tunaona Mungu akaja kumbariki mtoto wa pekee aliyekuja kuhubiri kwa uwazi kabisa habari za Yesu Kristo.
REJEA: Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti. Luka 1:5.
Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana. Luka 1:7.
Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana. Luka 1:13.
Kwa hiyo kukosa kwako mtoto mpaka leo upo mwaka wa kumi kwenye ndoa, sio jambo geni sana kwa msomaji wa Neno la Mungu. Huyu aliitwa tasa wala hakuwa na tatizo la kusema imeingia mimba na kutoka, kwa tafsiri rahisi tunaweza kusema tatizo lake halikuwa na dawa.
Kama ni mbuzi jike tunaweza kusema hana faida yeyote bora kumla nyama au kumuuza maana hazai chochote. Kama ni mti wa matunda tunaweza kusema bora kuukata usiendelee kubana nafasi ya miti mingine.
Ikiwa unapitia kwenye hali ya upweke na kutengwa na ndugu zako, tunamsoma Yusuph kijana mdogo aliyependwa na baba yake. Aliuzwa utumwani kwa ajili tu ya chuki na wivu wa kaka zake kuwasimlia ndoto yake.
REJEA; Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia. Mwanzo 37:5.
Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa,Mwanzo 37:23.
Wakapita wafanya biashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika, wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri. Mwanzo 37:28.
Unaweza kuona ni jinsi gani Neno la Mungu linatupa kila kitu, unapolisoma kwa undani na kulitafakari vizuri linakupa ujasiri wa kusonga mbele. Huwezi kutamani kumwacha Yesu Kristo kwa sababu umekutwa na matatizo fulani mabaya kwako.
Tunamwona tajiri mkubwa na mtumishi wa Mungu Ayubu, aliyepigwa na majaribu kila kona ya maisha yake, watoto wake wote walikufa, mifugo yake yote ilikufa na yeye mwenyewe akapigwa na ugonjwa wa majipu, alibaki na mke wake tu ambaye alikuja kumwambia amkufuru Mungu.
REJEA; Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu wayo wa mguu hata utosi wa kichwa.
Naye akashika kigae cha kujikunia; akaketi majivuni.
Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu, ukafe.
Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake. Ayubu 2 :7_10.
Nimekupitisha kwa baadhi ya watumishi na Changamoto walizopitia, zipo Changamoto nyingi sana ambazo siwezi kuzitaja kwa pamoja. Ikiwa ni huduma na uongozi tunamsoma Daudi akikabiliana na Sauli, kama ni kubakwa tunamsoma dada yetu Tamari, mambo ni mengi sana.
Lakini nia yangu nilitaka kukupa mwanga na uhakika wa kile nilichokuwa nakueleza kuwa kila jaribu unalopita wewe, Neno la Mungu limeeleza kwa uwazi na namna walivyoshinda wenzako waliopitia hilo. Uzuri wake ni kwamba biblia inakupa mwanzo na mwisho wake ulikuwaje.
Wokovu wako hauendeshwi na hali nzuri, hatuokoki kwa sababu tuna shida sana, hatuokoki kwa sababu tuna biashara nzuri, hatuokoki kwa sababu tuna kazi nzuri. Hatumtegemei Mungu kwa sababu hatuna hali mbaya kiuchumi, hatufurahii wokovu kwa sababu tunasoma shule/vyuo vizuri, hatufaruhi wokovu kwa sababu biashara na kazi zetu zinaenda vizuri.
Tunampenda Yesu Kristo na kumtumikia/kumtumainia siku zote za maisha yetu, kwa sababu yeye ni Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Hata kama biashara na kazi zetu zitaharibika bado tutaambatana na Yesu Kristo, hata kama upo mwaka wa kumi leo hujapata mtoto hakuna kwenda kwa waganga wa kienyeji kutafuta msaada. Msaada wetu pekee ni Yesu Kristo, yeye hujibu kwa wakati wake wala hakawii/ hachelewi.
Kwanini Neno la Mungu lisiwe chakula chako cha kiroho kila siku, kwanini unasitasita kusoma neno la Mungu, kwanini unaona kusoma biblia ni mateso. Hujajua tu kuwa dira ya maisha yako yote ipo ndani ya Neno la Mungu, iwe huduma au maisha yako ya kawaida.
Mungu akusaidie kuelewa faida ya kusoma Neno la Mungu, na hasara za kutokusoma Neno la Mungu. Bila kusukumwa na mtu yeyote, utaanza kujisukuma mwenyewe kusoma Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana kwa muda wako, karibu sana tujifunze Neno la Mungu pamoja.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com