Habari Njema Kwako Unayesoma Biblia Lakini Huelewi Unachosoma.
Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana wetu Yesu Kristo ametupa kibali cha kuiona tena leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye kwa kuwa fadhili zake ni kuu mno kwetu.
Karibu sana katika somo la leo tujifunze kwa pamoja namna ya kutoka kwenye hali ya kutokuelewa kile unachosoma, na kuweza kuelewa vizuri kile unachosoma ndani ya biblia.
Yapo mambo machache yanayoweza kumpelekea yeyote anayesoma Neno la Mungu asiweze kuelewa vizuri kile anachosoma. Ili mtu aweze kuelewa vizuri kile anasoma ndani ya biblia anapaswa kuhakikisha anakuwa mtu wa namna hii;
1. Roho Mtakatifu.
Ili uwe umejazwa na Roho Mtakatifu unapaswa kuwa ni mtu aliyeokoka yaani kumkiri Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wako. Na ili Roho Mtakatifu awe ndani yako, njia zako zinapaswa kuwa safi zenye kumpendeza Mungu wako, ndipo Roho Mtakatifu atakuwa mwalimu na kiongozi wako kwa kila hatua ya maisha yako.
Changamoto inakuja pale mtu anaposema ameokoka alafu bado kuna mambo mabaya anayafanya, ili wokovu wako usiwe na mashaka yeyote. Unapaswa kuziacha zile njia mbaya na kumgeukia Yesu Kristo kisawasawa, ndipo hata Roho Mtakatifu ataweza kutulia ndani yako kukusaidia yale usiyoyaweza.
Kama hujawahi kujazwa Roho Mtakatifu, tamani sana kujazwa Roho Mtakatifu, unaweza kujiuliza nitajazwaje sasa na huyo Roho Mtakatifu. Swali zuri sana; hii inaletwa na kiu yako mwenyewe ya ndani ya kutaka kujazwa na Roho Mtakatifu, na ishara moja wapo ya kujua umejazwa ni kunena kwa lugha mpya.(soma kitabu cha Matendo 2:1…)
Usomaji wako wa biblia unategemea sana Roho Mtakatifu, hii ni muhimu sana wala sio jambo la kujadili sana. Ili uelewa vizuri maandiko Matakatifu na Mungu aweze kusema na wewe vizuri moja kwa moja, unahitaji Roho wa Mungu aweze kukufanulia vizuri na kukupa uelewa mzuri ndani ya ule ujumbe uliokusudiwa kwako.
2. Msongo Wa Mawazo.
Wengi wetu tunakuwa tunaruhusu mawazo yatutawale ndani yetu kutokana na zile changamoto tunazopitia wakati huo. Ukiwa na mawazo mengi ndani yako kuelewa kwako Neno la Mungu itakuwa ngumu sana, kwa sababu akili yako haipo kwenye kile unachokisoma.
Hili lin aweza kuwa tatizo kwako usipoliondoa mapema, na msongo wa mawazo unakuja pale tunaposhindwa kukubaliana na hali halisi iliyotupata. Ili utoke kwenye gereza hili unapaswa kukubali hali halisi, ili iwe rahisi kwako kujua ni njia ipi utatumia kuziba pengo lililotokea.
Tuchukulie mfano labda umefukuzwa nyumbani, hapa hata ulie usiku na mchana ukweli utabaki palepale umefukuzwa na wazazi/walezi wako hawakutaki. Unachopaswa kujiangalia na wewe kuacha kujiumiza kwa mawazo na kulia sana, cha maana sana kwako ni kuangalia utapata wapi sehemu ya kujihifadhi kwa muda wakati unafikiria cha kufanya.
Maisha yanaendelea siku zote, uwe unapita pagumu au uwe unapita parahisi, siku zinaenda wala hazisubiri mtu. Ukielewa hili moyo wako utaupunguzia mizingo mingi sana ambayo mingine umejipa kazi mwenyewe kuibeba. Wakati hukupaswa kabisa kujibebesha mambo mengi kiasi hicho yasiyo na ulazima kuyabeba.
Labda tuchukulie mfano mwingine unaweza ukanielewa zaidi, tuchukulie umeondokewa na mpendwa wako uliyekuwa unamtegemea kwa baadhi ya mambo yako. Kuumia utaumia sana na kulia utalia sana, ila ni kosa kulia kama mtu asiye na matumaini ya Kristo ndani yake. Kifo ni njia ya wengi wetu tutapita mlemle lakini tunalotumaini la ufufuo wa watakatifu siku ya parapanda ikilia.
Ikiwa ni Upendo tunapaswa kumwonyesha mtu sasa hivi, sio usubiri mtu afe ndio unaanza kuonyesha uchungu, wakati yupo mzima hukuonyesha ukaribu wowote wa maana zaidi ya kumkwepa kwepa tu. Ili kujiepusha na machungu ya kumwaza sana aliyetuacha, ni kuonyesha kumjali anapokuwa hai ili anapotokea amekufa usiwe na deni ndani ya moyo wako.
Ukiweza kutuliza moyo wako pale unapopita katika magumu yeyote yale, utakuwa na nguvu ya kumwomba Mungu, utakuwa na uwezo wa kushika biblia yako na kusoma kilichoandikwa. Ukiumia sana na kushindwa kufanya mambo mengine, haitachukua siku nyingi sana ukiwa bado akili yako haijatulia. Siku za mwanzo utapata shida na unaweza usifanye chochote cha maana ila Mungu atakutia nguvu kwa namna ya pekee sana.
Shida inakuja pale mtu ameshikilia jambo miezi hadi mwaka, mpaka anashindwa kufanya kazi zake vizuri eti sababu alitendewa jambo baya miezi kadhaa iliyopita au alitokewa na jambo la kuumiza moyo wake miezi kadhaa iliyopita. Bado moyoni ameshikilia lile lile jambo, mtu wa namna hii hamjui Mungu, huwezi kukaa na hasira wiki au mwezi kwa jambo lolote lile kama unajua unapaswa kusamehe ndipo na Mungu aweze kukusamehe makosa yako.
Hayo ndio mambo makuu mawili yanayosababisha mtu asiweze kuelewa vizuri kile anasoma ndani ya biblia yake. Kuepuka hiyo hali ni kufuata kile nimekuelekeza kwa upana, sijakutajia sababu nyingi sana kukupa nafasi ya kufanyia kazi zaidi haya machache.
Hakikisha unafanyia kazi haya ndipo mambo mengine madogo madogo utaweza kuyafanyia kazi kiurahisi. Maana tayari kiu ya kusoma Neno la Mungu itakuwa imejenga vizuri sana ndani yako.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com