Unachotaka Kukifanya/Kukizungumza Kina Lengo La Kujenga Au Kina Lengo La Kubomoa/Kusambaratisha.
Tumsifu Yesu Kristo, siku nyingine tena mpya Bwana ametupa kibali cha kuiona tena, ni neema kwetu sisi kwenda kutenda yatupasayo kwa ajili ya kumletea sifa na utukufu.
Kuna nyakati tunaweza kuwa na roho ya mavurugano bila sisi kujijua kama tunachofanya hakijengi bali kinavuruga watu wengine na kuwapoteza kabisa kwenye kusudi la Mungu. Tusipolijua hili mapema tunaweza kugeuka kikwazo kwa watu wengine bila sisi kujitambua kama tunachofanya ni kosa.
Kuna nyakati pia tunaweza kuwa tunamani watu wawe katika hatua fulani tukifikiri sisi tulipo kwenye hiyo hatua tupo salama kumbe sivyo tunavyofikiria. Wakati Mungu anawaacha wengine wawe kwenye hatua fulani kwa Kusudi lake maalum na kwa kazi yake maalum.
Uwe makini sana, ndio maana unapozungumza jambo hebu liangalie watu wanalichukuliaje hilo jambo. Unapozungumza unataka watu wale wawe kwenye Kusudi fulani njema au unataka kuonekana na wewe umeongea au kufanya.
Tunajifunza Neno la Mungu ili tuwe imara kila eneo la maisha yetu ya kiroho na kimwili, hatujifunzi Neno la Mungu ili tuwe na roho ya mavurugano na mafarakano. Unapokua kiroho maana yake ufahamu wako nao unakuwa, huwezi kufanya kitu fulani kutaka kugombanisha watu. Utafanya jambo kutafuta kujenga palipo bomoka na sio kuharibu zaidi ya mwanzo.
Tunapaswa kuwa wa kweli kwenye maeneo yetu yote ya maisha yetu, ila sio kila sehemu zote utaweza kuusema ukweli wote kama ulivyo. Kuna maeneo unapaswa kusema nusu ya ukweli kutokana na mazingira ya kutokutaka ukweli huo.
Yesu alipokalishwa kwenye baraza kujibu mashataka, kuna vitu hakutaka kuzungumza kwa sababu aliona ni mtego na hata akiwajibu hawapo tayari kupokea, ndio maana alisema nyie mwasema.
SOMA; Hata kulipokucha, walikutanika jamii ya wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, wakamleta katika baraza yao, wakisema, Kama wewe ndiwe Kristo, tuambie. Akawaambia, Nijapowaambia, hamtasadiki kabisa. Tena, nikiwauliza, hamtajibu. Lakini tangu sasa Mwana wa Adamu atakuwa ameketi upande wa kuume wa Mungu Mwenyezi. Wakasema wote, Basi, wewe ndiwe Mwana wa Mungu? Akawaambia, Ninyi mwasema kwamba mimi ndiye. Wakasema, Basi, tuna haja gani tena ya ushuhuda? Maana, sisi wenyewe tumesikia maneno ya kinywa chake. LK. 22:66-71 SUV.
Unaweza kufikiri unachokifanya kinajenga kumbe hicho unachokazana kukifanya kinabomoa zaidi, unapaswa kuwa na tasimini kwa kile unachofanya. Usifanye kwa matakwa yako tu unapaswa kufanya kwa ajili ya utukufu wa Mungu Baba .
Kuna vitu unaona kabisa unafanya haviwapendezi watu, unajuaje kuwa haviwapendezi watu? Pale unapozungumza unasikia miguno ya kupinga au kukataa na kutokubali kile unachosema. Unajua kabisa unachokisema watu hawakubaliani na wewe, ikiwa hawakubaliani na wewe hata kama useme sana hawatakuelewa.
Sikufundishi uwe mwoga usiyeweza kuusema ukweli wa Mungu, nakufundisha hekima ambayo unapaswa kuwa nayo ndani yako ili unapozungumza Uzungumze kwa makini, na lengo lako kuu liwe kujenga na si kubomoa.
Najua umewahi kuona mtu anazungumza kitu watu wanaanza kuzomea badala ya kusikitika au kuitikia kwa wanachoambiwa. Na mwingine akaja akasimama akazungumza kitu kile kile watu wakamsikia na kumwelewa vizuri na kumpigia makofi na vigelegele.
Ukisoma habari za Nehemiah 5:1… unaona alivyokuta watu wakiwa na hali mbaya za kunyang’anywa mali zao kwa kushindwa kulipa madeni yao waliyokopa. Ukisoma hapo utaona Nehemiah akikemea hiyo tabia na watu walirejeshewa mali zao.
Usifikiri Nehemiah alikurupuka kukemea tu hiyo hali, Nehemiah alikuwa na kibali mbele za Mungu, aliposimama kutetea haki hata wale walio wanyang’anya ndugu zao mali waliona kweli wametenda kosa.
Neno la Mungu halitufanyi tuwe na vurugu, Neno la Mungu linatufanya tujue tusiyoyajua, tukishayajua tunaanza kuona kweli tunahitaji kubadili misimamo yetu ya awali. Hapa hakuna mtu anayekusukuma, wewe mwenyewe unaanza kutafuta hiyo sehemu nzuri unayoelekezwa.
Mungu akusaidie kuelewa zaidi hichi ninachokueleza hapa, ili kuepuka kuwa sehemu ya vurugu badala yake uwe sehemu ya kujenga. Haijalishi utaisema kweli ambayo itapenya ndani ya mioyo ya watu, uwe na uhakika una kibali mbele za Mungu kuzungumza hayo. Sifa moja wapo ya kujua unachokizungumza kina kibali mbele za Mungu ni kuona mwitikio wa watu kwako.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com