Tabia Yako Njema Inatengenezwa Na Kukuzwa Na Bidii Yako.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya Bwana ametupa kibali cha kuiona tena. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana kwa maana fadhili zake ni kuu sana kwetu.

Tunaposema tabia njema ya mtu, tunaweza kuwazungumza watu hawa katika makundi matatu tofauti tofauti ili uweze kuelewa zaidi kile nataka ukijue;

Kundi la kwanza; wapo watu hawajamjua Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yao ila wana tabia nzuri na mwenendo mzuri kwa macho. Ila wakati mwingine ukienda kiundani zaidi unamkuta sio yule unayemwona kwa nje, ana vitabia fulani vichafu sana ambavyo unaweza usimpe ile hadhi yake ya kwanza kabla hujamjua vizuri.

Kundi lingine la Pili; wapo watu wanamjua Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yao ila tabia zao ni mbaya na wakati mwingine unaweza kuona asiyemjua Kristo ni afadhali. Hii inaletwa na mtu yule kuwa nusunusu ndani ya wokovu yaani anapenda ya dunia yasiyofaa, na palepale anapenda mambo ya Mungu. Mtu wa namna hii tabia yake lazima iwe na mashaka hata kwa wasioamini, maana utamkuta ni mwenye matusi, mzinzi, mkorofi, na tapeli anayechukua pesa za watu alafu harudishi.

Kundi lingine la tatu; ni yule mtu aliyeamua kujitoa asilimia zote kumfuata Yesu Kristo bila kusukumwa na mtu yeyote yule. Kinachomsukuma yeye kumtumikia Mungu kwa bidii ni ile kiu yake ya ndani kutaka kumpendeza Mungu wake pasipo kuangalia watu watamwangaliaje/watamsamaje.

Mtu huyu wa tatu yeye siku zote huwa hafanyi vitu kwa ajili ya kutafuta sifa kwa watu wengine, anafanya vitu kwa bidii ili kuendelea kuimarisha zaidi uhusiano wake na Mungu wake. Ikiwa ni maombi ataomba si kwa sababu anataka kuonekana mwombaji sana, ikiwa ni utoaji atatoa si kwa sababu anataka watu wamwone mtoaji sana la hasha atafanya matendo mema yenye utukufu kwa Mungu kwa sababu ya ushirika wake na Mungu.

Jinsi unavyozidi kumjua Mungu wako ndivyo na tabia yako inazidi kuwa njema zaidi, maana unazidi kubadilishwa baadhi ya misimamo yako uliyokuwa nayo awali ukijua upo sahihi kumbe sivyo unavyodhania. Moja ya njia nzuri ya wewe kukuelekeza wewe uwe na tabia njema isiyo na mashaka kwa wanadamu na mbele za Mungu, ni kusoma Neno la Mungu.

Neno la Mungu linampika mtu yeyote yule mwenye tabia yeyote ile, mwenye malenzi yeyote yale, anapoamua kujifunza Neno la Mungu kwa kuamaanisha kweli. Zipo tabia za asili zitaondoka kwa kuijua kweli ya Mungu, vitu vingine havimwondoki mtu kwa sababu tu ameokoka. Vile anavyozidi kuukulia wokovu ndivyo anavyozidi kutengenezwa tabia njema, unakuta mtu alikuwa na ile roho ya kiburi na dharau kwa watu wengine, ila inamwondoka kabisa.

Kumbe Neno la Mungu halitufanyi tu kujua ahadi za Mungu kwetu na kuwa werevu wa kuwajibu mataifa wasiomjua Kristo kama Bwana na Mwokozi wao. Bali tunakuwa na vitabia fulani vizuri zaidi hata kwa wale ambao wanakuwa shingo ngumu kumwamini Kristo, ila kupitia wewe wanaamua kubadilika kabisa kutokana na tabia yako.

Nakueleza vitu halisi ambavyo naviona mwenyewe, siku moja nikakutana na kijana mmoja akaniuliza wewe ndio fulani? Nikamjibu ndio mwenyewe, akasema nakuona sana kwenye mitandao ya kijamii. Kupitia wewe nimeamua kuokoka na sasa naenda kubatizwa maana unanigusa sana.

Huyu kijana hakujua kinachomgusa sio mimi bali Roho wa Mungu, mimi ni balozi tu wa kuwakilisha kile Roho Mtakatifu ananipa msukumo wa kukisema kwa wakati husika. Ili watu wake wapate kubadilika kupitia jumbe mbalimbali zinazotoka, hii haifanyiki ili kujichukulia utukufu, sifa na utukufu ni kwa Mungu tu.

Tamani kuanzia leo Neno la Mungu likubadilisha tabia yako mbaya na kuwa nzuri, najua una vitabia ambavyo huvipendi wewe kama wewe bila hata mtu yeyote kukuambia. Ila unajikuta unavifanya, Neno la Mungu linakuambia kuna vitu havitoki mpaka kwa kuomba tena wakati mwingine unapaswa kujinyima chakula.

Rejea; Akawaambia, Namna hii haiwezi kutoka kwa neno lo lote, isipokuwa kwa kuomba. Marko 9 :29

Tulitafute Neno la Mungu kwa bidii sana maana linatugusa kila eneo la maisha yetu ya kiroho na kimwili, utakuwa mwombaji mzuri kama unasoma Neno la Mungu, utakuwa mwalimu mzuri wa kufundisha Neno kama msomaji mzuri wa Neno la Mungu, utakuwa na tabia yeyote njema ikiwa tu utakuwa una Neno la Mungu ndani yako.

Hekima za dunia hazitakusaidia chochote mbele za Mungu, bali hekima ya Mungu ikiwa ndani yako itakusaidia kila eneo la maisha yako. Kwanini usiipende biblia na kuisoma kwa bidii ili uendelee kuwa bora zaidi katika matendo mema, badilika kuanzia leo kama ulikuwa unachukulia kawaida kawaida.

Bila shaka kuna kitu umekipata, na kitu hicho kimeugusa moyo wako kwa namna ambavyo unaona ni ya pekee sana kwako. Hicho ndicho Mungu alikusudia kwako siku ya leo, kiweke katika matendo ili kiweze kuzaa matunda mema katika maisha yako.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, ombi langu kwa Mungu akafanye jambo jipya ndani ya maisha yako ya wokovu.

Usiache kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Facebook; Chapeo Ya Wokovu.
Website; www.chapeotz.com
Email; chapeo@chapeotz.com
Wasap& calls; +255759808081.