Kinachomfanya Mtu Asome Neno La Mungu Sio Uhuru Mkubwa Alionao Kuliko Wengine.

Asifiwe Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana wetu ametupa kibali cha kuiona tena leo, sifa na utukufu tumrudishie yeye mwenza wa yote.

Kuna wakati tunajipa moyo na kuendelea kujifariji kuwa hatuna muda wa kutosha wa kusoma Neno la Mungu, na wakati mwingine tunaenda mbali zaidi kuona wanaosoma biblia ni watu wasio na majukumu mengi ya kufanya, ndio maana wao wanapata uhuru mwingi wa kusoma Neno la Mungu.

Huenda hatujawahi kukaa chini siku moja tukajitafakari kwa kina tunatafuta uhuru upi ambao tunautaka uwe kwetu ndipo tuweze kusoma Neno la Mungu. Huenda uhuru tunaoona hatuna kuna wengine wanautamani wangekuwa nao wangefurahi sana. Hao wanaotamani uhuru wetu, wao wanakazana kumpa Mungu muda wao wa kusoma Neno la Mungu kila siku, bila kujali ufinyu wa muda wao.

Najua unaelewa vizuri ukiwa na majukum mengi ndio unatimiza ratiba zako nyingi zaidi kuliko wakati ambao unajiona huna mambo mengi. Mtu anayejiona hana muda wa kusoma Neno la Mungu ndiye anayeongoza kukaa vijiweni, ndio anayeongoza kuchati kwenye makundi ya wasap, ndio anayeongoza kulala sana akitoka kazini/shuleni, ndio anayeongoza kuingia facebook na instargram.

Unajiuliza mtu anatafuta uhuru upi wa yeye kusoma Neno la Mungu unaukosa, kama anapata muda wa kukaa kijiweni, kama anapata muda wa kuchati kwenye magroup ya wasap, kama anapata muda wa ku like na ku comment post mbalimbali facebook na instargram. Kinachomshinda mtu huyu kukosa muda wa kusoma Neno la Mungu ni kipi?

Unaweza kuona wengi wetu sio tatizo la muda/nafasi, tatizo letu lipo ndani yetu, mtu anakwambia sijapata muda wa kwenda kanisani wakati huo alikuwa amekaa tu hafanyi chochote. Lakini wale waliokuwa wanafanya kazi kuanzia asubuhi mpaka wa ibada unafika, wao ndio wamepenyeza wakapata nafasi ya kumwabudu Mungu wao katika kusanyiko la pamoja.

Mtu yule yule ambaye anafanya kazi/biashara zake tangu ameiona siku mpya, ndio yule yule utamwona akisoma Neno la Mungu na kupata nafasi ya kulitafakari. Lakini yule ambaye amewahi kutoka kazini au wakati hana kabisa majukum mengi ndio utamkuta ni mvivu namba moja wa kutokusoma Neno la Mungu.

Kipindi cha nyuma kuna kaka mmojs alikuwa amejiunga na Chapeo Ya Wokovu wasap GROUP, huyu kaka alikuwa chuo nafikiri ndio ilikuwa mwaka wake wa mwisho wa masomo. Alivyomaliza chuo akaniambia sasa nimemaliza chuo kuanzia sasa utakuwa unaniona nikisoma Neno la Mungu kila siku kuliko kipindi cha nyuma. Kwa kweli huyu kaka kama alisoma Neno kwa bidii alivyomaliza masomo yake alifanya hivyo wiki moja ya kwanza, baada ya hapo alipoteana mpaka hivi sasa ninavyokuandikia haya.

Unaweza kuona wengi wakiwa wamebanwa ndio wanakuwa wasomaji wazuri kabisa wa Neno la Mungu, mwingine anakwambia unajua mtumishi inapofika jioni huwa nakuwa nimetingwa sana kwa kuandaa chakula. Mwingine anakuambia unajua ikifika jioni huwa naenda mazoezi ya kwaya kwa hiyo muda wangu wa kusoma Neno la Mungu unakuwa hakuna.

Hizo ni sababu za mtu asiyejua anachokifanya, hivi kweli upo siriazi unaweza kutoa sababu kama hizo, kwa hiyo muda wako huwa unaupata tu ukiwa unaenda kupika au huwa unaupata ukiwa unaenda mazoezi ya kwaya. Unaweza kujipa majibu mwenyewe na ukaona uzembe wako upo wapi, visingizio ni vingi sana mpaka inafika kipindi tunajidanganya wenyewe.

Uhuru unaoutafuta wewe hutakaa uupate moja kwa moja, nafasi hiyo hiyo uliyonayo sasa itumie vizuri kusoma Neno la Mungu. Usifikiri ipo nafasi nyingine utaipata zaidi, huko ni kujidanganya ndugu yangu, muda unao mwingi sana sema unaupoteza kwenye vitu visivyo na faida kwako. Hushindwi kupata dakika 30 au lisaa limoja kwa siku la kusoma Neno la Mungu, kama kuna watu hawana muda basi naamini watakuwa hawawezi kupokea simu zao wala kuandika ujumbe wowote wala kukaa na familia zao.

Nje na hapo tutaendelea kujifariji hatuna muda wa kusoma Neno la Mungu wakati mtu anaweza kukaa akiangalia TV, mwingine anakikisha hapitwi na tamthilia ila anakubali kumaliza siku bila kusoma Neno la Mungu, mwingine anahakikisha hapitwi na mpira ila anapitwa na siku bila kusoma Neno la Mungu.

Uhuru unaoutaka wewe unaweza kuutengeneza mwenyewe ukawa msomaji mzuri kabisa wa Neno la Mungu, acha kufikiri wanaosoma Neno la Mungu wana muda wa kutosha sana kufanya hivyo. Huko ni kujidanganya ndugu yangu lazima uamue mwenyewe kujitoa kwa ajili ya hili.

Bila shaka kuna kitu umekipata cha kukusaidia kutojipa sababu za kushindwa kusoma Neno la Mungu, anza kufanyia mazoezi muda wako, punguza kukaa vijiweni na marafiki zako, punguza makundi ya wasap unayochati, punguza kuingia kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii. Najua inaweza kuwa ngumu kwako ila ukitambua umhimu wa kusoma Neno la Mungu hivyo vyote havitakuwa kikwazo kwako, hebu jitoe katika hili la kusoma Neno la Mungu nakwambia hutojuta.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu.

Email; chapeo@chapeotz.com

WhatsApp; +255759808081