Neno La Mungu Lina Nguvu Ya Kunyonya Mawazo Mabaya Yanayokujia.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya Bwana ametupa kibali cha kuiona tena. Sifa na utukufu tumrudishie yeye kwa fadhili zake kuu kwetu.

Tunaishi katika dunia iliyo na kila changamoto mbalimbali, kuna wakati mwingine tunajikuta tunapambana na mambo mpaka tunajiona kabisa ndani yetu imani inaanza kushuka kutokana na yale magumu tunayokutana nayo.

Huwa hatusemi wazi wazi ila ndani ya mioyo yetu tunaona kabisa pasipo msaada wa Mungu, tulipofikia ni pagumu sana. Hapa usipopata watu wakasimama na wewe kukuombea, na usipokuwa na ujazo mzuri wa Neno la Mungu moyoni mwako ni hatari sana kwako kumwacha Mungu na kugeukia miungu mingine.

Sio ajabu ukawa mshirika mzuri wa kanisa ila ukawa mhudhuriaji mzuri kwa wachawi, sio ajabu ukawa na ulinzi nyumbani/ofisini kwako uliopewa na wachawi, huku unasema Yesu ni Bwana na Mwokozi wako.

Yapo mambo ya msingi huwa tunashindwa kuelezana ukweli tukifikiri ni ngumu kwa mkristo kuyatenda, lakini cha ajabu biblia imeyaweka wazi kabisa. Tunaona hata kwa wana wa Israel walifika mahali wakaona Mungu wao hawasaidii tena, wakaona wajitengenezee sanamu waiabudu kama mungu wao.

Hata leo bado watu wanafikia hatua kwenda kutafuta msaada kwa wachawi, lakini bado wanaingia makanisani na kutoka. Ni vitu ambavyo vipo na tunapaswa kujua chanzo chake ni nini mpaka mtu kufikia hatua hiyo, huku bado tunamwona sehemu za ibada akimwabudu Mungu asiyependa kuchanganywa na miungu mingine.

Mazoea ya kumwabudu Mungu yanaweza kuchagia kwa asilimia kubwa sana kurudi nyuma, mazoea ndio yanamsababisha mtu aone kusoma Neno la Mungu hakuna haja. Bila kujua Neno la Mungu lina uwezo wa kunyonya kila wazo potofu linalotutaka tuache njia sahihi na kutushauri kugeukia njia mbaya.

Kama nilivyosema tangu mwanzo, tupo dunia yenye mambo mengi sana pasipo msaada wa Mungu hatutaweza kushinda kila changamoto zinazotujia. Changamoto zingine zinakuja zimebebana kiasi kwamba usipokuwa na stamina, na chujio ambalo ni neno la Mungu, nakwambia utaacha wokovu.

Hujawahi kuona una shida alafu akakujia mtu anakwambia we nenda kwa babu fulani au mama fulani atakurekebishia mambo yako haraka. Huyu babu/mama fulani sio anaenda kukupa ushauri au panadol za kutuliza maumivu ya kichwa, unaelekezwa kwa mchawi. Kama hujawahi kukutana na washauri wa namna hii mshukuru Mungu ila naamini utakuwa umewahi kusikia kwa marafiki zako wakishauriwa hivyo.

Fikiri anakujia mtu anakupa ushauri wa namna hiyo na wewe wakati huo umebanwa kisawasawa, mtu huyu anakutolea mifano hai aliyotendewa yeye baada ya kwenda au akupitisha kwa watu unaowaamini wewe waliwahi kuwa na shida fulani wakapona. Ujasiri wa kutokwenda utaupata wapi kama huna Neno la Mungu la kutosha ndani yako, kwanza hofu ya Mungu inaweza isiwe ndani yako wakati huo.

Hebu fikiri dada/mama umevuka kwenye miaka ya ishirini na kitu leo upo thelasini na kitu kuelekea arobaini na kitu, huna dalili za kuolewa zaidi sana wanakuja wanaume karibia wote wanakutaka kimapenzi kwanza. Kama ni maombi ya kufunga kwa ajili ya Mungu kukupa mume wako umefanya hivyo sana, kama ni uaminifu mbele za Mungu umejitahidi sana.

Inafika hatua kibidanamu unaona kabisa ndani yako unajisikia kuchoka, unaanza kujisikia hata ile hamu ya kwenda kanisani inatoweka kabisa, unaanza kuona ile hamu ya kuomba Mungu inakuisha kabisa, unaanza kuona kwenda kushirikiana na wenzako mambo ya kanisani inakuisha kabisa.

Usipokutana na Neno la Mungu katika hali uliyofikia, nakwambia kuasi kwako kupo mlangoni kwako kunasubiri utoke. Lakini tukisimama vizuri katika kulisoma Neno la Mungu tunakuwa tunajiwekea akiba ya kutosha. Ambayo muda mwingine tunajikuta hatuwezi kushika biblia tusome Neno la Mungu, ndio wakati sasa wa yale tuliyoyajaza mioyoni mwetu kutusaidia kushinda mawazo mabaya.

Mawazo mabaya/potofu yanakosa nguvu ndani yetu ya kutupoteza njia salama kwenda njia mbaya kwa sababu ya akiba ya Neno la Mungu iliyo ndani yetu. Kama huna utaratibu wa kusoma Neno la Mungu uwe na uhakika utakuwa mkristo jina ila moyoni mwako utakuwa unajua machafu unayoyatenda.

Hakikisha unaona jambo hili la kusoma Neno la Mungu ni mhimu sana kwako, asiwepo mtu wa kukupotosha kuhusu hili. Tenga muda wako kila siku kusoma Neno la Mungu itakusaidia sana maeneo yako yote ya maisha.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.

Chapeo Ya Wokovu.

Chapeo@chapeotz.com

+255759808081.