Jinsi Unavyozidi Kujifunza Neno La Mungu Ndivyo Unavyozidi Kufufua Vitu Vilivyolala Ndani Yako.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona, sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana kwa wema na fadhili zake.

Leo napenda kukumbusha jambo la msingi sana kama ulikuwa hujui na kama ulikuwa unajua basi utakuwa umeboresha zaidi. Pia nakukumbusha husomi Neno la Mungu kwa ajili ya wengine, ni kwa ajili ya faida yako mwenyewe.

Zipo faida nyingi sana kwa mwamini aliyeamua kutoa muda wake kwa ajili ya kusoma Neno la Mungu, kadri unavyozidi kusoma Neno la Mungu kuna vitu ndani yako vinazidi kuimarishwa na kuna vitu ndani yako vinazidi kufufuliwa zaidi ndani yako.

Kujifunza Neno la Mungu kila siku sio kupoteza muda wala sio jambo la kufanya ukiwa upo huru siku hiyo wala sio jambo la kufanya ukiwa unajisikia vizuri, yaani siku hujisikii hufanyi, siku unajisikia umechoka hufanyi, siku unaona hujakumbushwa husomi. Unapaswa kuelewa unachokifanya ni kwa ajili ya faida yako mwenyewe, na unapaswa kuliweka hili mstari wa mbele kabisa katika ratiba zako za siku.

Ndani ya Neno la Mungu kuna ahadi zako ambazo Mungu amekuahidia kukutendea katika maisha yako ya wokovu, ndani ya biblia kuna maisha yako uliyopaswa kuishi ukiwa ndani ya Kristo. Ndani ya biblia kuna namna ya kuishi na watu, ndani ya biblia kuna hekima ya kiMungu inakuwezesha kuongoza watu, na ndani ya biblia kuna vipawa na karama mbalimbali ambazo mtu anaweza kujitambua.

Kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu kuna vitu ndani yako vinazidi kukuzwa na vingine vinazidi kufufuliwa ambavyo hukuvijua kama unaweza kuvitenda wewe. Unaweza kujishangaa ulikuwa sio mwombaji ukageuka kuwa mwombaji mzuri, unaweza kujishangaa ulikuwa sio mwalimu ukawa mwalimu mzuri, unaweza kujishangaa ulikuwa sio mnyenyekevu ukawa mnyenyekevu.

Huwezi amini kuna watu mpaka leo wanahifadhi vitu moyo pasipo kuweza kusamehe, huyo hajamjua Mungu vizuri lakini kadri unanvyozidi kumjua Mungu utajiona hustahili kumshikilia mtu moyoni mwako. Utafufua moyo wa msamaha ndani yako, utafufua upendo ndani yako, utafufua kuwajali na kuwathamini wengine.

Unaweza kuwa ulikuwa mvivu sana kwenye mambo ya Mungu lakini ghafla katika kujifunza kwako Neno la Mungu ukafufua bidii yako ya kumpenda sana Mungu wako. Haya yote yanatoka kwa Mungu mwenyewe, na ahadi nyingi alituahidi ila kutokana na kutojua kwetu hatutaki kuutafuta uso wake kwa bidii.

Ipo faida kubwa sana katika kusoma Neno la Mungu, binafsi naona mabadiliko makubwa ndani yangu. Huwa napenda kujichunguza kujua maendeleo yangu yakoje kadri ninavyosoma Neno la Mungu. Nikashangaa siku moja nikawa na tabia moja ya ajabu sana kwangu, nasema ya ajabu sana kwa sababu kabla ya hapo sikuwa nayo kwa kiwango kile. Ila kwa awamu hii imeboreshwa zaidi ya awali yaani ni kama vile kuna kitu kilikuwa nusu sasa kimekuwa kamili.

Unaweza kuona ni jinsi gani Neno la Mungu linaweza kututengeneza vizuri pasipo kuhangaika kutafuta watu wengine watuambie sisi ni akina nani. Maana tayari unaona kujiona mtu wa tofauti ndani yako, na vizuri zaidi unapojifunza jambo ndani ya biblia na likaugusa moyo wako jaribu kuliweka kwenye matendo.

Hili nimekuambia mara nyingi sana la kuweka Neno la Mungu katika matendo, kuna tofauti sana mtu anayesoma Neno la Mungu na kuliacha hapo. Na kuna tofauti kubwa sana na mtu anayesoma Neno la Mungu na kuliweka katika matendo, haijalishi siku za mwanzo atakuwa anakoseakosea uwe na uhakika baada ya muda fulani atakuwa imara sana katika hilo.

Vipo vitu vingi sana vya kiMungu vimelala ndani yako, usikubali ufe navyo, anza kumtafuta Mungu kwa bidii sana kwa kusoma Neno lake utaona mabadiliko ndani yako. Sikuelezi hadithi za zamani nakueleza vitu halisi kabisa, kuokoka tu hakutoshi kama hutamzalia Mungu matunda ya kuokoka kwako.

Fanya bidii sana kusoma Neno la Mungu, tenga muda wako kusoma Neno la Mungu, hakuna kisingizio katika eneo hili kama kweli upo siriazi na mambo ya Mungu. Ukiona huwa unaanza kusoma Neno la Mungu na kuishia njiani, tafuta kikundi/mtu aliyejitoa kweli kusoma Neno la Mungu umfuatilie kwa Karibu sana moja wapo ni hapa chapeotz.com tunakuletea jumbe za kukusaidia kusonga mbele.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, kwa uweza wa Mungu tutahakikisha unalipenda Neno la Mungu na kujua faida zake.

Chapeo Ya Wokovu.

Chapeo@chapeotz.com

+255759808081.