Ustahimilivu Wa Moyo Kuweza Kupambana Na Mambo Magumu Unajengwa Na Neno La Mungu.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye kwa fadhili zake kuu kwetu, maana sio kwa ujanja wetu kuiona leo.

Kabla ya yote nitoe pole kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wote waliopatwa na msiba wa watoto wadogo wa shule huko Arusha. Ni msiba mkubwa sana kwa taifa letu na pigo kubwa kwa familia, ila hatuna budi kukubaliana na matokeo. Tunachopaswa kufanya mimi na wewe ni kuwaombea hawa ndugu wapate faraja ya kweli ndani ya mioyo yao na Mungu aendelee kuwatia nguvu katika kipindi hichi kigumu kwao, ili wavuke salama.

NENO LA FARAJA: Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Zaburi 23:4.

Baada ya salamu hizo sasa nikiombe urudishe moyo wako hapa ili tuweze kwenda pamoja katika ujumbe wa leo niliokuandalia hapa.

Hakuna ajuaye kesho atakumbukwa na nini, hakuna ajuaye kesho ataamka alivyoamka leo au atamka na jambo jipya la kuumiza moyo wake. Wapo walio na mahusiano mazuri na Mungu huwa wanapata taarifa ya jambo kabla, kama anaweza kulizua kwenye maombi atafanya hivyo. Na kama haiwezekani kufanya hivyo basi hubaki akisubiri huku akimwomba Mungu ampe stamina za kuweza kukabiliana na hilo jambo.

Vilevile yapo mambo huwa hatuwezi kupewa taarifa kutokana na uwezo mdogo wa kukubali kukabiliana nayo, pia wakati mwingine Mungu anashindwa kusema nasi kwa urahisi kutokana na sisi kuwa mbali naye. Hata pale anapojaribu kuwatumia watumishi wake waje kwetu kututaarifu, huwa tunawapuuzia na kuona ni mawazo yao na wamekosa cha kufanya.

Pamoja na hayo yote tukirudi katika moyo wa somo hili, tunawezaje kuwa na stamina za kukabiliana na mambo magumu yanayotupata. Yaani mtu akipatwa na jambo awe na uwezo kulipokea na kulikubali hata kama liwe gumu kiasi gani kwake, hata kama atalia na kuomboleza, mwisho wake akubali kweli limempata.

Ukomavu wa kiroho ni mhimu sana katika maisha yetu, unapofikia kwenye matatizo magumu ukaanza kutamani kutafuta sumu ujiue fahamu hapo uchanga wa kiroho unakusukuma kufanya hivyo. Yaani kupitia uchanga wako wa kiroho shetani anaweza kutumia kutojua kwako kukushawishi kufanya jambo lisilofaa mbele za Mungu.

Neno la Mungu lina uwezo wa kumsaidia mwamini yeyote hata kama atajikuta ametengwa na watu wote katika shida yake, maana anapotulia na kujiona yupo peke yake Roho Mtakatifu anamkumbusha Neno La Mungu kupitia kitabu fulani kinasema hivi na vile. Anapokaa anajiona amebaki yatima au mjane na hana msaada wowote tena, Roho Mtakatifu anamkumbusha mstari fulani katika biblia unasema Mungu ndiye Baba wa yatima na mume wa wajane.

Ustahimilifu wetu wa mambo magumu unaletwa na ukuaji wetu wa kiroho, ukuaji wenyewe wa kiroho ni pale mtu mwenyewe anapojitoa kujifunza Neno la Mungu. Bidii yako ya kumjua Mungu kupitia Neno lake, inakupa uwezo wa wewe kukabiliana na mambo mbalimbali katika maisha yako.

Kama nilivyokuambia wengi wetu hakuna anayejua atatokewa na nini baada ya saa moja mbele, labda itokee Mungu akakupa taarifa kuna jambo fulani linakuja mbele yako. Hii haitokei mara zote ukapata taarifa, swali la kujiuliza unapokutwa na hali ya kutatiza utaweza kukabiliana na maumivu hayo?

Lazima ifike wakati tuelewe kwamba kujenga mahusiano yetu na Mungu ni mhimu sana, unapokuwa na nafasi ya kumpa Mungu muda wako kusoma Neno lake unapaswa kuelewa hupotezi kitu bali unaongeza kitu.

Neno la Mungu lina msaada mkubwa sana kama utalielewa vizuri, kwanza ni rahisi hata mtu akija kwako akakuambia Neno la Mungu linasema hivi. Moyo wako utashuka upesi baada ya kusikia Mungu anasemaje kuhusu changamoto unayopitia, ila kama huelewi chochote kuhusu Neno la Mungu utaona kama vile watu hawajui kabisa hali unayopitia ndio maana wanasema hivyo kirahisi. Kumbe wakati mwingine Mungu ametumia watu kusema na wewe, ila kwa sababu huelewi unawakataa na kuwafukuza kabisa.

Hebu chukulia hili suala la kusoma Neno la Mungu ni la muhimu sana kwako, litakusaidia wewe na utawasaidia wengine wakati usioujua wewe. Kuna wakati utakosa hata mtu wa kukufariji, je ndio itakuwa mwisho wa maisha yako? La hasha maisha lazima yaendelee.

Bila shaka kuna kitu ambacho umejifunza kupitia ujumbe huu, lengo kuu ni wewe kuweka akilini mwako kusoma Neno la Mungu ni muhimu. Ukishaliweka akilini mwako suala la kusoma Neno la Mungu hutopata tena ugumu wa kulisoma.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.

Chapeo Ya Wokovu.

Chapeo@chapeotz.com

+255759808081.