Kuonekana Kwa Nje Una Bidii Ya Kumpenda Mungu Alafu Ndani Yako Unajua Sivyo Ulivyo Ni Kujitengenezea Mazingira Ya Kujizalilisha.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, bila shaka nawe umepata nafasi nyingine tena ya kwenda kumzalia Mungu matunda yaliyo mema kwa kuwajibika katika eneo alilokujalia uwepo.

Karibu sana tujifunze pamoja mambo machache ya kukusaidia kuimarisha uhusiano wako na Mungu ili uweze kusonga mbele zaidi ukiwa imara. Unaweza kuenenda katika picha fulani hivi nzuri watu wanayoiona kwa nje, kumbe ndani yako huna tabia njema kama inavyoonekana kwa nje, badala yake ukawa na matendo machafu kwa siri.

Unaweza kuonekana kwa nje una bidii ya kuutafuta uso wa Mungu, kumbe sivyo ulivyo ndani yako, badala yake ukawa na agenda yako binafsi ndani yako. Wakati watu wanakuona wewe ni mwana wa Mungu aliye hai, na wakati mwingine watu wamekuweka katika kundi la wacha Mungu. Lakini baadaye inakuja kuonekana ulikuwa humchi Mungu katika roho na kweli, ulikuwa umevaa utakatifu kwa nje ila ndani yako umejaa upagani mtupu.

Unaweza kuonekana kwa nje unasoma sana Neno la Mungu, ila moyoni mwako unajua kabisa husomi Neno la Mungu. Ila unataka kuonekana kwa watu kuwa unasoma, na unafanya kuonekana kwa watu kwa maslahi yako binafsi unayolenga kwa watu hao. Badala ya kuonyesha mabadiliko kadri unavyozidi kumjua Mungu, unazidi kuporoka siku hadi siku.

Hii ni kwa sababu hatupo kumaanisha ndani ya mioyo yetu kwa kile tunachokifanya, haiwezekani ukawa mwenye bidii ya kweli kuutafuta uso wa Mungu alafu ukawa unashuka kiroho kila siku. Ndio maana unaweza kukaa na mtu ndani ya dakika chache ukagundua ameokoka au hajaokoka, kama tu utakuwa vizuri kiroho na makini. Mazungumzo yake na watu wengine yanaweza kukupa picha ya ndani ya mtu alivyo, japo anaweza kujaribu kuuficha uhalisia wake ila kama wewe ni mtu wa rohoni utajua hapa pako vizuri na hapa sio pazuri.

Nizungumze sasa na mtu wa namna ya kujenga mwenekano mzuri wa nje kuonyesha anamtafuta Mungu kumbe sivyo watu wanavyomwona. Ipo hatari kubwa sana kuja kupata aibu ya mwaka, nakwambia ukweli usiopingika, usipotubu na kutengeneza na Mungu wako vizuri. Itafika hatua mambo yote yatakuwa hadharani, kama ulikuwa unafanya uchafu wako kwa chinichini itafika saa huo uchafu utaonekana kwa uwazi.

Leo binti upo kanisani na unaonyesha unampenda sana Mungu, kumbe nyuma ya pazia unatembea ovyo na waume za watu, siku itafika matunda ya uchafu wako yatadhihirika wazi na ulimwengu wote utajua. Kinachokuja kutokea watu wataona mimba, hata kama utazitoa sana hizo mimba itafika kipindi utaitoa vibaya ndipo watu watajua siku hiyo hiyo michezo yako. Maana utapatwa na mateso ambayo hukutegemea.

Leo kaka upo kanisani lakini michezo yako ni michafu kwa chinichini, lakini kwa nje unaonekana mcha Mungu, unaonekana mwombaji mzuri, unaonekana mwimbaji mzuri, kila shughuli ya kanisa upo. Hakuna asiyekujua kuwa wewe ni mtoaji mzuri wa zaka, ila ukweli unaujua ndani yako huna mahusiano mazuri na Mungu wako.

Hizi drama unazocheza nazo kuwalaghai watu, nakwambia utaumbuka siku moja, usifikiri kumwona dada fulani alikuwa vizuri kanisani alafu akapata mimba ukafikiri iliota tu ghafla. Kuna uasi ndani yake ulishaingia siku nyingi ila hakutaka kutubu na kuachana na hiyo tabia mbaya, usifikiri mpaka mtu kukamatwa akifanya jambo fulani baya ilitokea tu ghafla akawa hivyo.

Ikiwa watu wanakuona upo siriazi kweli na kusoma Neno la Mungu, lakini ndani ya moyo wako unajiona kabisa umeshapoteza uhusiano wako na Mungu. Nikiombe sasa umrudie Mungu wako, hayo maigizo yako hayatakufikisha mbali utakuja kuumbuka, huo usanii wako wa kucheza na vichwa vya watu kuna siku utakuja kutereza kidogo tu watu watajua kila kitu, kuwa wewe hukuwa umeokoka.

Yafaa nini kuwaonyesha wanadamu upo vizuri alafu umefarakana na Mungu wako, hakufai chochote ndugu yangu. Mungu anakupenda sana ndio maana anakupa maneno kama haya maana anakujua vizuri sana kuliko wakujuavyo watu wake. Siku akitaka kuwaonyesha matendo yako, utakuja kujuta na hutasema wamekusingizia maana dhamiri yako itakuwa inakushtaki ulichokuwa unakifanya ni kweli, na sio kizuri.

Umeamua kumfuata Yesu achana na maigizo, mfuate kweli kwa kumaanisha, mambo ya kusikia umeaguka sijui umefanyaje hiyo ni kutosimama katika sehemu yako vizuri. Utakuja kutikiswa kidogo na tatizo watu wakijua upo vizuri kumbe ni hewa tupu ndani, hapo ndipo utaanguka na watu watajua waziwazi huyu alikuwa mbovu.

Neno la Mungu libadilishe tabia yako, Neno la Mungu libadilishe utu wako wa ndani, ifike hatua watu wanavyokuona kwa nje na ndani iwe vivyo hivyo. Ifike wakati watu wanavyokufahamu una tabia nzuri katika mazingira unayofahamika, wakuone vile vile ukiwa ugenini.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.