Maandiko Matakatifu Yanakupa Uwezo Wa Kujua Ukweli Kuhusu Wokovu Kwa Pande Zote Mbili.

Siku nyingine tena Bwana wetu Yesu Kristo ametupa kibali cha kuiona tena, nafasi nzuri kwetu kwenda kufanya yale yampendezayo yeye. Wengi waliitamani leo ila hawakuweza kuifikia, ila mimi na wewe tumepata nafasi adimu sana ya kuweza kufanya jambo jema. Pia hatuna budi kumrudishia Mungu sifa na utukufu kwa uweza wake huu.

Mara nyingi tumeambiana jambo nusu nusu na kuficha upande wa pili ili kulinda watu wasije wakajua yote wakakimbia, tumesahau tunapofanya hivyo ni hatari kwetu kama tutakuwa tuna makusudi mabaya ya kunyonya wengine, au ikawa nzuri kwetu kama tutakuwa tuna malengo mazuri. Maana mtu akija kujua alikuwa anadanganywa, atakimbia na ataanza kusambaza sumu ya kuwa wewe ni muongo.

Tunashindwa kuambiana ukweli wa jambo kwa maslahi yetu binafsi ila Mungu ni mwema kwa watu wake kadri wanavyozidi kumjua yeye anawapa uwezo wa kuelewa mambo mengi zaidi. Inabaki kwa wale wasiopenda kujishughulisha kusoma Neno la Mungu, hawa wanakuwa wanampa kibali yule aliyewabana eneo fulani la kiroho waendelee kuwa vilevile.

Mtu anapokujia kila siku kukuambia wokovu ni raha bila kujua hiyo raha inatokana na nini, na mtu akifanya nini ndipo ataona hiyo raha. Huyo mtu atakimbilia haraka kuokoka alafu akija kupata kajaribu kidogo atatamani kurudia maisha yake ya zamani. Lakini angejua raha inayozungumzwa ni kule mtu kusimama katika roho na kweli, hata inapotokea dhoruba kali katika maisha yake, Yesu Kristo anasimama juu yake kumtetea.

Hapo mtu anakuwa ndani ya wokovu anajua kabisa upo wakati mgumu utakuja na atapaswa kupita humo akiwa amemshikilia Yesu Kristo. Na kusema Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yake, haijalishi kuna vitu alikuwa navyo vikamwondoka. Bado mtu huyu atajua Mungu anampenda na hatamwacha kamwe hata kama mali zake zimepotea, hata kama amefukuzwa kazi, hata kama amefiwa na mke/mume wake, hata kama ameondokewa na watoto wake wote, na hata kama wazazi wake wamemwacha yatima.

Shida inakuja kwa mtu anaokoka anajua hataweza kuguswa na vitu vya kuumiza moyo wake, amesahau mshitaki wetu Ibilisi anatusemea kwa Mungu. Pale Mungu anapojivunia kuhusu sisi watoto wake tuliosimama na yeye vizuri, shetani anamwambia wanafanya hivyo kwa sababu umewapa afya njema. Ili Mungu kumthibitishia shetani kuwa wewe humtegemei Mungu kwa sababu ya afya yako njema, Mungu ataruhusu ugonjwa ukupate.

Kwa wale wanaojua maandiko kwa upande mmoja wataanza kukuambia umelaaniwa na Mungu, unahitaji kukombolewa. Hawajui kuwa wewe upo kwenye eneo ambalo Mungu anataka kujichukulia sifa na utukufu. Kama hujasimama vizuri na humjui Mungu wako vizuri utaona wanayosema watu ni kweli utakuwa umelaaniwa au utakuwa umefarakana na Mungu wako.

Wakati mwingine Mungu anajaribu kumwonyesha adui yetu kuwa sisi tunamtegemea yeye katika roho na kweli, kwa kuruhusu vile vitu vizuri tulivyokuwa navyo vipotee kabisa katika miliki yetu. Shetani atakapoona bado tunaendelea kumpenda Mungu wetu, hata pale alipojaribu kutushawishi tuende kwa waganga wa kienyeji kutafuta msaada tulikataa. Mungu hujitwalia utukufu kupitia sisi, hata ndugu, jamaa na marafiki walioshiriki kusema wanayofikiri wao wanaona kweli kiwango chetu cha kumpenda Mungu kipo vizuri.

Hatupaswi kumpenda Mungu kwa sababu anatupa mali nyingi, siku hizo mali zikituondoka tutaacha kumpenda Mungu? La hasha upendo wetu kwa Mungu haupo katika mali zetu, bali upendo wetu upo kwake kwa sababu yeye alitupenda kwanza, akamtoa mwanaye wa pekee kwa ajili ya kutukomboa sisi wanadamu wenye dhambi.

Mbaya sana kumpenda Mungu katika maisha ya furaha na amani, siku ukibanwa vizuri na changamoto za maisha, ile furaha yako ya awali itaondoka. Atakuja mtu atakuambia twende ukatulize mawazo yako na pombe utakubali, atakuja mtu atakuambia mtu fulani anakusumbua we twende kwa babu/bibi fulani akakomeshwe.

Ungejua zipo nyakati utapita ngumu, usingehangaishwa na ushauri mbaya wa watu, shida yetu tunajua tukiokoka hatuwezi kuguswa na jambo lolote baya. Tunaona mabaya ni kwa ajili ya wenye dhambi tu, ni kweli ila tumechukua ukweli wa upande mmoja. Kisu ni kizuri ukikitumia kwa matumizi yaliyo sahihi, vile vile kile kisu kinaweza kutumika kama silaha ya kuua, kama utamuua mtu utaenda kufungwa. Lakini fahamu kisu ni kile kile kizuri kinachokusaidia kila siku kukatakata nyanya, vitunguu, kuchinja kuku/ng’ombe/mbuzi ukala nyama.

Ili kuepuka utapeli katika maisha yako ya wokovu, hakikisha unamjua Mungu vizuri kupitia Neno lake. Acha kumfahamu Mungu upande mmoja wa mazuri tu, acha kumfahamu Mungu upande wa kuponya magonjwa tu, acha kumfahamu Mungu upande mmoja wa miujiza yake tu. Mfahamu Mungu vizuri pande zote mbili, ili unapofika nyakati fulani dunia ikaona umefarakana na Mungu wako, kumbe Mungu anataka kuwaambia watu huyu ni mtoto wangu mwaminifu kwangu. Hata akipatwa na matatizo bado anampenda Mungu katika shida yake.

Ifike kipindi watu wasijue tu upo kanisani kwa sababu Yesu Kristo alikuponya, watu wajue upo kanisani kwa sababu umejua uweza wa Mungu juu ya maisha yako kuliko miungu mingine. Hata itokee ukaugua tena wakuone umesimama palepale ndani ya wokovu, isitokee tena ukawa mtu wa kutangatanga, leo ulisema Yesu ni mzuri, kesho ukabadilisha Yesu ni mbaya.

Haya yote utayaelewa vizuri kama utatoa muda wako kulisoma Neno la Mungu, Neno la Mungu linakupa ukweli wa pande zote mbili. Upande ule watu wasiopenda kuusikia na upande ule wengi wanaopenda kuusikia.

Bila shaka kuna kitu umekipata cha kuweza kukusaidia kuongeza bidii ya kujifunza Neno la Mungu kwa juhudi zote, weka zaidi katika matendo huku ukimwomba Roho Mtakatifu akusaidie kuelewa yale usiyoweza kuelewa kwa akili za kibinadamu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.