Tumefunika Maandiko Matakatifu Tumebakia Wasikilizaji Na Waitikiaji.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya Bwana wetu Yesu Kristo ametupa kibali cha kuiona tena leo. Fursa kwetu kwenda kufanya yale yanayomzalia Bwana matunda yaliyo mema.

Kuna vitu tunafanya vya kusikitisha sana ambavyo tunaweza kuona tupo sawa ila tunajidanganya na kuendelea kujifariji kwenye vifungo ambavyo tupo. Wakati wengine wanakuombea utoke kwenye tanuru lililokubana muda wako wa kushindwa kusoma Neno la Mungu, wewe mwenyewe unaona hicho kitendo cha kutosoma Neno la Mungu ni sahihi kwako.

Inapotokea jambo lolote unaanza kunukuu vibaya Maandiko ambayo hata hayahusiani Kabisa na kitu unachofikiria wewe ni sawa. Wakati mwingine tumehalalisha uongo kuwa ukweli na kuusimamia huo uongo kama vile ndio ukweli wenyewe.

Wengine wamelishwa mapokeo ya dini zao kiasi wanaona haina haja ya kusoma Neno la Mungu, na hawa ndio wanaosumbua sana na kujiona wanaifahamu vizuri biblia kumbe wanafahamu misingi ya dini zao. Ambapo kama dini ingekuwa inampeleka mtu mbinguni basi kila mmoja mwenye dini ataiona hiyo mbingu, wala haina haja kuhubiri injili na kusisitizana watu wajue Neno la Mungu waache kudanganywa ovyo.

Siku moja nikaota ndoto ya ajabu sana, ndoto yenyewe ilikuwa hivi; nilikuwa nimeenda kusali kanisa moja hivi liko pembeni kidogo ya mji wa SINGIDA. Wakati mtumishi yule anaendelea kuhubiri mbele ya madhabahu ile…niliona pembeni ameweka Bia, akiongea kidogo anapoza koo lake na Bia ile kama maji. Sasa mimi nikawa nashangaa sana ila waumini wengine wakawa wanaona kawaida, wakati naendelea kutapatapa kujiuliza hiyo imeanza lini mchungaji kunywa Bia huku akiendelea kuongea…huu mshangao ulinishika mpaka naamka asubuhi.

Ndugu yangu ilikuwa ni habari ya kushangaza sana kwenye video hii ya bure kabisa kwenye ndoto, baadaye sasa nikapata fahamu ya hiyo ndoto. Mchungaji yule alichokuwa anakifundisha sio mafundisho ya Neno la Mungu bali yalikuwa mafundisho yanayolewesha fahamu/akili za waumini wale. Ndio maana walikuwa wanaona sawa tu wakati mimi nashangaa na kuwageukia wenzangu wanachukuliaje jambo hilo na tangu lini bia imekuwa kama maji ya kunywa madhabahuni…nimekueleza kwa ufupi sana.

Wakristo wa leo hatutaki kusoma Neno la Mungu, ndio maana tunanyweshwa mafundisho yasiyofaa huku tukiona ni mafundisho ya Neno la Mungu. Ndio maana leo hii watu wameacha kumwinua Yesu Kristo wanamwinua mchungaji, mtume, nabii wao.

Watu wameacha kumwogopa Mungu wanamwogopa nabii/mchungaji/mtume wao, wameacha kulitii neno la Mungu na huwezi kuwaambia chochote kwa sababu walichoambiwa hakiendani na Neno La Mungu. Kwa hiyo wanaona Maandiko Matakatifu hayafai kwao ila maneno ya nabii/mtume/mchungaji yanafaa kwao.

Sikuambii uanze kudharau wachungaji/manabii/mitume itakula kwako ndugu yangu, ninachokuambia hapa ni kutekwa/kubanwa ufahamu wako mpaka unashindwa kujitegemea mwenyewe. Yesu Kristo amekupa mamlaka ya kuomba lolote utakalo kwa jina lake, leo hii anakuja mtumishi anakwambia toa laki moja nikuombee maombi ya kufunguliwa katika laana…!!

Nielewe vizuri sikuambii ni kosa kutoa sadaka yako nzuri, ninachokuambia ni kwamba huwezi kununua uponyaji wa Mungu. Ndio maana maandiko yanasema hivi mlipewa bure toeni bure, hakuna aliyemnunua Roho Mtakatifu awe ndani yake, hakuna anayenunua nguvu za Mungu, hakuna anayenunua uwezo wa kutoa pepo wachafu.

Kwanini uliwe pesa zako kama umeokoka mwaka wa kumi leo, hutaki kujishughulisha na Neno la Mungu, ukiambiwa usome Neno la Mungu unasema upo bize sana. Lakini kwenye mambo mengine haupo bize, umebaki mshirika wa kuibeba biblia tu.

Kusikiliza na kutulia hekaluni mwa Bwana ili kufundishwa Neno la Mungu ni nzuri sana, ila hupaswi kufungwa ufahamu wako kiasi kwamba unashindwa kutenga muda wa kusoma Maandiko Matakatifu. Wakati mwingine kanisani matangazo yanakuwa na maelezo ya kina kuliko Neno la Mungu, sasa usipokuwa na muda kujilisha Neno la Mungu utabaki msindikizaji tu.

Bila shaka kuna kitu kimekusuma kuitafuta kweli ya Mungu, nakusihi sana utoe muda wako kusoma Neno la Mungu. Furaha yangu kwako ni kumjua Mungu wako vizuri, furaha yangu ni kukuona unakua kiroho kila siku, furaha yangu ni kukuona unafika hatua unajiamini na kusimama kwa miguu yako mwenyewe. Hii yote itakuja pale tu utakapojua upendo wa Mungu juu yako.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, naamini hata Neno la Mungu utaweza.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.