Haleluya, nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, Mungu ni mwema ametupa siku nyingine tena tukiwa wazima. Leo wengi waliitamani kuifikia lakini hakuweza, sisi ambao tumepata fursa hii tuitendee haki siku ya leo kwa kumzalia MUNGU matunda mema.

Safari yetu bado ni ile ile ya kuendelea kusisitizana usomaji wa NENO, kumkiri Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wako sio tu umemaliza kila kitu. Unapaswa kuendelea kukua zaidi katika kujifunza NENO lake na mafundisho mbalimbali yanayoujenga mwili wa Kristo ndani yako.

Unaweza kuwa umeokoka lakini ukaendelea kubaki mchanga kiroho kwa sababu hujibidiishi katika mambo ya Mungu. Kukua KIROHO kuna hitaji bidii yako binafsi, unahitaji kujisukuma na kuwa na nidhamu ya kusoma NENO.

Biblia inapaswa kuwa kifungua kinywa chako kama ilivyo wengi wetu hatuwezi kuianza siku bila kunywa kitu chochote cha moto.

Familia chache sana ambazo bado hazijajua umhimu wa kunywa chai, CHAI imekuwa kipaumbele sana kwenye nyumba nyingi. Ukienda kutembelea ndugu na jamaa unaweza kuona ni jinsi gani chai imekuwa kinywaji cha wageni.

Mungu wetu alitupa NENO lake ili tuweze kuenenda vile apendavyo yeye tuenende. Huwezi kuenenda njia ikupasavyo pasipo kujua NENO linasemaje kuhusu wokovu wako.

Kuna wakati unaweza kujiona upo sahihi kwa unalolifanya au unalolielewa, au unaloliamini, kumbe umepotoka kabisa.

Tunahitaji NENO la MUNGU lituongoze, na katika hili hauna sababu ya kujitetea maana una biblia ambayo leo unaweza kuisikiliza kwa sauti, vipo vifaa vingi ambavyo technology imeturahishishia sisi kuwa na biblia mahali popote.

Hakikisha hili unaliweka moyoni kama ilivyo simu yako, ambayo haipiti nusu saa unaiangalia kama kuna ujumbe wowote umeingia. Hili nalo la kusoma NENO unapaswa kuliweka kwenye ratiba zako, yaani inakuwa kama sehem yako ya maisha.

Ikiwa kuna vitu ambavyo ukiviangalia sana kwa undani wake havina msingi sana kuwekwa moyoni, ila vimewekwa moyoni iweje NENO la MUNGU lisiwe kipaombele ndani yako.

Lazima ubadilike, huhitaji muujiza mwingine ili uwe msomaji wa neno, huhitaji ukombozi mwingine. Ukombozi pekee kwako ilikuwa kumwamini YESU Kristo kama Bwana na Mwokozi wako.

Mambo mengine yanahitaji bidii yako baada ya kuokoka, hakuna kipaji cha kusoma NENO ambapo unaweza kusema ni kwa ajili ya wenye vipaji tu.

Kuna maeneo hutokuwa karibu na mlezi wako wa KIROHO, utahitaji kusimama wewe kama wewe, utawezaje kusimama ikiwa ndani yako huna NENO la MUNGU?

Lazima ikifike kipindi uamke usingizini, usingizini ulionao ni mzito mno unahitaji kuamka kwanza maana sio usingizi wa kawaida. Elewa wajibu wa kusoma NENO sio wajibu wa mtu mwingine bali ni wajibu wako.

Pasipo neno hatuwezi kuepuka dhambi zingine, maana tutafanya tukijua tupo sahihi kumbe tumepotea njia kabisa.

Amua sasa kujiwekea utaratibu wa kuipenda biblia, iwe umetingwa sana lazima ujue una kiporo hujakimaliza cha kusoma NENO.

Haijalishi wewe ni nani, yaani namaanisha haijalishi Mungu anakutumia kiasi gani, unahitaji kulijua NENO zaidi ili upate kutumika vyema na Mungu.

Mkristo asiyependa NENO la MUNGU, ukristo wake una maswali mengi sana tena una mashaka huo ukristo wake.

Hatuishi tu kwa nguvu za ugali, roho zetu zinahitaji chakula cha NENO, ikiwa tutashindia tu viazi, tutausaidia mwili wa nje kuendelea kukua na kunenepa. Ila utu wetu wa ndani utaendelea kukonda na kuchakaa kabisa.

Siku ya leo isipite bila kusoma NENO la MUNGU, fanya yote ila biblia nayo iwepo katika hayo mengi. Hakuna kuingiza kisingizio katika hili.

Ulianza kusoma NENO tangu mwaka uanze, ila sasa uliacha, nakusihi urudi upesi sana. Kama ulifikiri WOKOVU ni mteremko ulikosea sana.

Jitoe sasa nakusisitiza tena na tena, leo utenge muda wako kwa ajili ya kujifunza NENO la MUNGU.

Ulikuwa bado hujajiunga na group letu la wasap, la kujifunza NENO kila siku? hakikisha unajiunga ili tuwe kitu kimoja. Hapa nikupe tahadhari mapema; lazima uje na nia ya kusoma NENO na si kujaribisha, wala kuja kusoma upepo unaendaje. Hakikisha una nia kutoka ndani ya moyo wako, kufanya hivyo utafikia lengo, kama upo tayari tumia namba hizo chini kuwasiliana nami.

Mungu akubariki sana, endelea kumtafuta na kumtumikia Mungu kwa bidii.

Samson Ernest.

+255759808081.