Haleluya, nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, jina lipitalo majina yote, si lingine bali ni jina la Yesu Kristo. Habari za leo, siku nyingine tena Bwana ametupa kibali ya kuiona, hatuna budi kufanya jambo jema ambalo litakuwa alama njema kwetu.
Kila mmoja anatamani kufika hatua fulani katika kumjua Mungu, hatua hizi ndizo zinatufanya tuwe wanafunzi wa YESU. Mwanafunzi ni mtu anayefundishika na anayekubali kufundishwa, na anayetamani kufikia hatua fulani.
Huwezi kukua kama wewe mwenyewe hutaki kukua, hii ni tofauti na makuzi ya mwili wako, mwili ukila tu unaupa nguvu ya kukua zaidi. Unaweza kujizungusha ili usile chakula, itafika wakati njaa itauma sana na hutaweza kujizuia kula.
Wengi wetu tumekuwa watu wa visingizio, tunafanya jambo kwa makusudi kwa kofia ya uchanga wa KIROHO. Ni sawa wewe ni mchanga wa KIROHO mbona huna tabia ya kuonyeka na kufundishika.
Mwingine anakuambia siwezi kusoma NENO la MUNGU sielewi kabisa, sasa dawa ya kutoelewa ni kuacha kusoma au kutafuta marafiki wenye uelewa pale unaposhindwa kuelewa, ukaeleweshwa.
Mwingine anakuambia mimi bado sijawa na muda wa kutosha wa kusoma NENO la MUNGU, wakati mtu huyu anazunguka kwenye mitandao ya kijamii, analike na kutoa comment kwa jumbe za wengine.
Mtu huyu huyu yupo vizuri sana kwenye magroup ya wasap ya kuchati utumbo/upuuzi, alafu anakuambia hana muda wa kutosha kusoma biblia.
Uvivu ni kitu kibaya sana, tunapenda Mungu atufanyie vitu ila sisi hatutaki kutoa muda wetu kwa ajili yake. Tunafikiri upo muujiza wa kutufanya tukue KIROHO kwa jinsi tunavyotaka wenyewe pasipo kuwa na bidii ya kutulia mbele za Mungu.
Aliyeamua kusogea hatua fulani kiroho, na aliye siriaz na kile anataka, ni mtu msikivu sana, ni mtu anayekubali kuonyeka, ni mtu anayetamani kuona anasogea hatua fulani. Mtu huyu huwezi kumsukuma kufanya jambo, utamkuta ameshafanya maana anajisukuma mwenyewe.
Kujipa sababu za kuendelea kuwa mzembe, ama kuendelea kubaki pale pale, huo ni uvivu wa mtu binafsi ambao unapaswa kupingwa kwa hali zote.
Miaka yote hatuwezi kuendelea kubaki wachanga kiroho, tunahitaji kukua, mtoto akifikisha miaka miwili bado hatembei tunajua kabisa ana matatizo ya ukilema.
Wengi tumekuwa vilema wa KIROHO, mtu ameokoka mwaka wa pili sasa bado yupo vilevile, amebaki na wimbo wa mimi bado mchanga kiroho.
Jiulize na kujihoji wewe mwenyewe, baada ya kugundua ni mchanga KIROHO, kuna hatua gani umechukua? Hizo hatua ulizochukua uliendelea nazo au uliishia njiani na kurudia wimbo wako uleule.
Tabia hizi za kusingizia lazima tufike wakati tuzichukie, una masaa 12 ya mwanga/nuru, ina maana kati ya masaa haya upo bize kiasi kwamba huwezi pata nusu saa ya kuketi ukajifunza NENO la MUNGU.
Umepewa zawadi mikononi mwako, ya kitu kinachoweza kukusaidia maisha yako kiroho na kimwili, huhitaji kwenda kuomba kwa mtu mwingine.
Biblia ni zawadi yako, maneno yaliyo ndani ya biblia ni zawadi kwako, zawadi hii haijui dhehebu/dini yako. Maneno yaliyopo ndani yake, ni kweli tupu hakuna kupindisha ukweli.
Dhehebu/dini yako inaweza kukwepesha kweli ya Mungu, ila NENO likabaki pale pale na ukweli wake.
Elewa hili litakusaidia sana, ili ifike wakati ujue kuwa biblia iliyojaa maneno ya Mungu ni chakula kwako. Chakula hichi ndicho kitakufanya ukue kiroho.
Huwezi kuondoka kwenye uchanga wa kiroho kwa kujisemea tu mdomoni, lazima uamue mwenyewe kuondoka humo.
Tuachane na ubishi wa mapokeo ya dini zetu, YESU Kristo hakuleta dini alileta WOKOVU. Kila atakayemwamini, atapokea uzima wa milele.
Amka leo mkristo, acha hadithi za kujitia moyo, unahitaji kuchukua hatua, ipo raha katika kujifunza NENO.
Huwezi kuiona raha hii kama bado hujajitoa kusoma NENO la MUNGU.
Tumeanza mwezi Feb leo, maana yake JAN ndio tumeachana nayo ki hivyo, yaani hakuna JAN nyingine ya mwaka 2017. Haipo na haitakuja kutokea zaidi utakutana na JAN ya mwaka mwingine.
Ikiwa ulijiambia mwaka huu lazima usome biblia, mbona hujaanza sasa, na kama umeanza mbona umerudia njiani.
Nilikuambia tangu mwanzo achana na visingizio, utaendelea hivyo mpaka tunafunga huu mwaka 2017.
Ipokee zawadi hii ya NENO moyoni mwako, hutokuja kujuta maisha yako yote, hakuna kitabu bora kama biblia, nasema hakuna, amini usiamini nakwambia hakuna.
Sikuambii vitabu vingine ni ovyo, sijakuambia kusoma vitabu vya watumishi wengine haifai; nimekwambia haviwezi kufikia ubora wa biblia, hata kama unaviona ni vizuri sana.
Unatamani kuwa pamoja na wenzako wenye nia moja ya kujifunza NENO la MUNGU? Ungana na wenzako katika group la wasap kwa kutuma ujumbe wako kwa njia ya wasap, kupitia namba nitakazotoa hapo chini. Hakikisha huna visingizio, na hakikisha umedhamiria kutoka ndani ya moyo wako maana pasipo hivyo utaondolewa mapema sana.
Leo tupo kitabu cha 1 Nyakati 15, ambapo tunaenda kusoma na kupata muda wa kutafakari kwa pamoja na kushirikishana yale tuliyojifunza katika sura hii. Huhitaji nguvu kubwa ya kusoma sura nyingi, ni sura moja tu na unapata muda wa kutulia mbele za Mungu, kujua Mungu amekusudia nini juu ya maisha yako kupitia NENO lake.
Nakutakia wakati mwema.
Samson Ernest.
+255759808081.