Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, Mungu ni mwema ametupa nafasi nyingine tena ya kuifikia leo, si kwa jeuri zetu wala si kwa uweza wetu, bali kwa uweza wake.

Tabia yeyote inayopandwa ndani ya mtu, iwe tabia mbaya au iwe tabia nzuri, upo wakati mtu huwa anaingiza hiyo tabia ndani yake.

Mtu anaweza kujifunza jambo lolote lile likawa kama vile alizaliwa nalo akiwa analijua, kumbe sivyo hivyo, hii ni kwa sababu alilipenda ndani yake lile jambo akajifunza.

Wengine wanaweza hawakulipenda hilo jambo, ila kutokana na marafiki alionao muda mwingi, alipandiwa ndani yake zile tabia za marafiki zake.

Marafiki wana mchango mkubwa sana kumwambukiza mtu kitu ndani yake, ilimradi wale marafiki wameligeuza hilo jambo kuwa sehemu ya maisha yao.

Nilikuambia hapo mwanzo, tabia iwe nzuri au mbaya, inawezekana kuambukizwa/kupandwa ndani ya mtu.

Ndio maana unapaswa kuchagua marafiki wa kuwa nao, sio uchukie wengine na utengane nao kwa sababu za tabia zao la hasha. Unapaswa kuwa na marafiki wa karibu sana wenye tabia ile unayoitamani kuwa nayo wewe.

Kuambatana na marafiki wavivu, bila kujielewa na wewe unakuwa mvivu vilevile na marafiki zako walivyo.

Ninaposema marafiki maana yake ni kundi la watu fulani uliopatana nao, upo tayari kuwasikiliza hata kama sio kila jambo utakubaliana nalo, ila ndani yako unajua hawa ni marafiki zangu na hutokubali kuwaangusha.

Tunaelewa imani huja kwa kusikia, inaweza kuwa yapo mambo ulikuwa hukubaliani nayo kwao, ila jinsi unavyozidi kusikia hilo jambo ndivyo linavyozidi kujengeka ndani yako.

Haijalishi hiyo imani unayojazwa ndani yako ni imani nzuri au imani mbaya.

Uwezekano upo umeshindwa kuwa mtu wa kusoma NENO la MUNGU kwa sababu marafiki ulionao, ni marafiki wasiopenda NENO la MUNGU.

Inawezekana kila ukijaribu kusoma NENO, kuna maneno wanakupa ya kukukatisha tamaa.

Huenda kila ukijaribu kuwashiriki zoezi unalofanya la kusoma biblia, wanakupa maneno ya kukuvuta nyuma usiendelee.

Maneno hayo huenda umeona ya kawaida ila yamekuwa sumu kubwa ndani yako, ambayo yamekufanya na wewe umekuwa mtu wa maneno matupu na si vitendo.

Uwezekano upo ulianza vizuri sana kuwa na tabia ya kutenga muda wako kwa ajili ya kusoma NENO, ila baadaye akatokea rafiki akatamka neno la kukuondoa kwenye lengo lako la kusoma.

Huenda ulikuwa na kundi la marafiki wanaojifunza neno, ila kutokana na kundi lingine lisilopenda kukuona ukijifunza neno, wamekuwa sehemu ya wewe kurudi nyuma.

Nikwambie kwamba, hao ni marafiki wasiofaa katika safari yako ya KIROHO, ili kuwafanya kuwa marafiki wema. Lazima uamue leo kutofautiana nao, utofauti huu utakuwa na vita ndani yake ila utakuwa mwema.

Huenda unajiliuza utapata wapi marafiki wanaopenda kujifunza NENO la MUNGU, usipate tabu kuhusu hilo, Chapeo Ya Wokovu wasap group limekutengenezea utaratibu wa kukutana na marafiki wanaopenda kujifunza NENO.

Kuna utaratibu mzuri unaokubana usome NENO hata unapojisikia kuacha kusoma, utaratibu huu ni upi huo ambao utakufanya wewe uliyeshindikana miaka mingi? Swali zuri sana; ni marafiki utakaokutana nao.

Nilikuambia kuambatana na marafiki uliokubaliana nao, wana mchango mkubwa sana kukubadili tabia yako. Kama ulikuwa na tabia ya uvivu unaenda kuwa na tabia njema ya kujifunza NENO la MUNGU.

Najua umeokoka, lakini una changamoto ya kutosoma NENO, hilo ni tatizo kwako. Unapaswa kuikataa hiyo hali, ndio maana nakuambia kuhusu marafiki wa kuambatana nao.

Sio lazima kuwa na hili group, unaweza kutengeneza ratiba yako mwenyewe ya kujisomea NENO la MUNGU ukapata muda wa kutafakari yale uliyojifunza.

Nimekuambia unaweza kuambatana na marafiki wanaopenda kusoma NENO, kwa sababu kuna nguvu kubwa katika marafiki. Ila unaweza kuchagua kile unapenda moyoni mwako kati ya kuambatana na marafiki wenye lengo moja au kuwa na ratiba yako mwenyewe.

Unahitaji nidhamu ya hali ya juu sana katika kufanikisha hili zoezi la kusoma NENO, elewa hili usije ukalisahau katika safari yako mpya ya kujifunza NENO.

Usije ukajidanganya nilianza kusoma NENO, ukaona huelewi ukaacha, hapo utakuwa umekubali kurudi kundi la wavivu.

Chagua sasa kuwa rafiki wa kujifunza NENO la MUNGU, achana na urafiki wa kukubana usijue maarifa ya NENO la Mungu.

Umejisikia ndani ya moyo wako kuungana na wenzako waliopo group la wasap, tumia mawasiliano ya namba za simu hapo chini. Hakikisha umedhamiria ndani ya moyo wako, pia hakikisha unatuma sms kwa njia ya wasap na si sms ya kawaida.

Leo tupo kitabu cha 1 Nyakati 16, tunaenda kusoma sura hii na kupata muda wa kutafakari kwa pamoja, na kushirikishana yale tuliyojifunza.

Mungu aendelee kukufungua ufahamu wako zaidi, ili upate kuelewa zaidi umhimu wa kusoma NENO.

Samson Ernest.

+255759808081.