Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo, siku nyingine tena mpya Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye kwa uweza wake mkuu, na hii ni nafasi kwetu kwenda kumzalia Bwana matunda mema.

Tunakutana na Changamoto mbalimbali tunapoanza siku, unaweza kuamka leo ukiwa hujajipanga kukutana na jambo fulani ukashangaa limekukumbuka tu ghafla.

Unaweza kuamka leo ulikuwa hujui kama unaenda kukutana na shida fulani ofisini kwako, ikatokea na ikavuruga baadhi ya mipango yako ya siku.

Unaweza kuamka leo ukaweka ratiba zako vizuri, ikatokea dharura ambayo unapaswa kukatisha mambo yako na kwenda sehemu fulani. Labda sehemu hiyo ni msibani au kuna jambo lako ulilokuwa umewaachia watu walifanye limeharibika.

Unaweza kuamka leo ukapanga utamaliza kazi zako muda fulani, ila ikatokea mkuu wako wa kazi akakuongezea majukum mengine zaidi. Au ikatokea wewe ndio unapaswa kusimama katika zamu ya mtu mwingine kwa kutokuwepo kwake.

Siku zingine unaamka hujisikii kufanya chochote kutokana na mambo fulani yanayotatiza kichwa chako, na kuna vitu vya muhimu unapaswa kuvifanya siku hiyo. Ila mwili unakataa na kuona kama mateso fulani hivi kuanza kufanya kitu ambacho kitatumia akili nyingi au nguvu kubwa.

Pamoja na hayo yote unaweza kushangaa huwezi kuondoa ratiba yako ya kula chakula, unaweza kubanwa sana kuanzia unaamka asubuhi mpaka mchana. Lazima utatafuta chakula kilipo ule, ikipita mchana hutoweza kulala usiku bila kula.

Hata ule uvivu uliokuwa umekushikilia unashangaa unashindwa na njaa iliyokukabili, unashangaa uchovu uliokuwa nao unaukataa na kula chakula hata kama ni kidogo. Si unajua ukichoka sana hata ile kula yako inakuwa ndogo, lakini si utakula hata kama ni kidogo?

Unajisukuma kula kwa sababu unajua usipokula utapata madhara fulani, unajua usipokula hata huo utendaji wako wa kazi hautakuwepo tena. Unaweza kwenda kula kwa lazima hata kama ulikuwa hujisikii vizuri kwa sababu huna namna nyingine.

Kinachotufanya tushindwe kusoma Neno la Mungu ni nini, kwanza kabisa ni uvivu. Uvivu una nafasi kubwa sana kumfariji mtu asiwe msomaji wa Neno la Mungu, ukifuatilia sababu ya kumfanya awe mvivu inaweza isiwe na uzito sana.

Jambo lingine ni uchovu wa mwili, wengi tunachukulia nafasi kubwa sana kuupa mwili nafasi ya kujitetea sana pale tunapokuwa tumechoka na mizunguko ya kutwa nzima. Kweli kuna wakati mtu unachoka, ila wakati mwingine tunatumia huo mgongo kutofanya vitu vya msingi.

Hivi umewahi kujiuliza uchovu huwa unaenda wapi unapopata taarifa nzuri sana, labda ukapigiwa simu kazini kwako umepandishwa cheo au ukaambiwa katika wanafunzi wa nchi nzima mliokuwa mnasoma nao. Wewe ndio umeongoza kwa nafasi ya kwanza, hebu niambie ule mchoko huwa unaenda wapi?

Labda ikatokea tena ulikuwa umekaa porini umechoka sana kwa safari, akatokea simba mbele yako. Utaendelea kukaa au utatafuta njia ya kuokoka na hilo balaa si lazima utakimbia? Ndio utakimbia hata ulikuwa unasema miguu inakuuma huwezi kukimbia.

Labda porini mfano unaweza kuwa mgumu kwako, ulikuwa unasikia usinginzi mzito sana ndani mwako. Akatokea mtu anakwambia kuna watu wamevamia ofisi yako, usingizi wote utakuisha, je huo usingizi umeenda wapi? Mfano sio mzuri sana ila najaribu kukuonyesha nguvu ya mtu iliyo ndani yake, upo uwezo wa ziada ambao Mungu kauweka ndani yako.

Ukitambua kitu unachokifanya, hutoruhusu utawaliwe na uvivu wala uchofu, tengeneza sababu za kujisukuma kwa kujiondoa eneo lililokufunga na kukuambia umechoka sana lala/pumzika. Iambie hiyo sauti ikitokea jambo la hatari hapa utaendelea kusema umechoka sana au utakurupuka tu hapa. Maana hiyo sauti inakuzuia usijenge mahusiano yako na Mungu wako.

Ukijikuta umechoka sana, hebu jaribu kujenga utulivu wa ndani na fanya kitu chochote ambacho kitatibua zile hisia zako za ndani. Unaweza kusikiliza nyimbo unayoipenda sana, au unaweza kufanya jambo lolote lile unalojua moyo wako utafurahi.

Utashangaa umejifungua kwenye kitanzi cha uchovu na kupata muda wa dakika chache kusoma Neno la Mungu. Mpaka hiyo hali ije ikurudie, wewe utakuwa umemaliza kusoma na kutafakari kile umekisoma.

Siku zingine kuondoa hiyo hali ya uchovu, pata muda mchache wa kusinzia angalau nusu saa, hapo utaupa mwili wako nguvu za kusoma Neno la Mungu. Ukiona hilo nalo linakushinda, oga maji ya baridi kisha ingia moja kwa moja kwenye kusoma Neno la Mungu.

Mpaka hapo adui yako wa uchovu na uvivu utakuwa umemwepuka kirahisi sana, na kama atajitokeza siku nyingine ukashindwa kukabiliana naye. Haitajirudia kesho kwa sababu unajua ulipokosea na utapata namna ya kukabiliana naye.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.