Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali cha kuiona tena leo. Hatuna budi kumrudishia sifa na utukufu kwa nafasi hii adimu aliyotupatia siku ya leo.
Tunapoanza jambo mara nyingi huwa tunalianza kwa juhudi kubwa sana, kila mmoja anayetutazama anafika kipindi anavutiwa na ile bidii yetu. Anapovutiwa na bidii yetu tunaanza kumsogeza karibu na sisi, mtu yule anaanza kupata hamasa ya kuchukua hatua za yeye kuanza kufanya na kuishi kama anavyotuona sisi tunaishi.
Kutokujua kwetu ile bidii tunayoifanya katika maisha yetu ya kila siku, kuna watu tunawabadilisha na kuwaweka karibu zaidi na Mungu wetu. Lakini badala yake katika bidii yetu, tumeingiza mazoea ambayo tumeanza kufanya vitu kwa kawaida sana sio kama ile tulivyokuwa mwanzo.
Mara nyingi mazoea haya huja pale tunapoanza kufanikiwa na kujulikana kwa wengine, mazoea haya mara nyingi huja pale tunapopata sifa nyingi za watu, mazoea haya mara nyingi huja pale tunapoona hakuna zaidi yetu. Tunapofika hatua hii tunaanza kupoteza ule mfano wa kuigwa kwa wengine maana tayari inafika wakati hata hao waliokuwa wanajifunza kwetu tunaanza kuwadharau.
Unapoingiza mazoea kwenye jambo lolote lile, ujue umefika hatua ya kuzika ile bidii yako iliyokuwa inakufanya upendwe na watu wengine. Kama watu walikuwa wanasema kwanini wasiwe kama wewe, watabadilisha kauli na kusema wasije wakawa kama wewe uliyeanza vizuri ukapoteana.
Kwanini tukubali kuzika ule uwezo wetu mkubwa tuliokuwa na mwanzo, kwanini tuzike zile nguvu za Mungu tulizokuwa nazo mwanzo, kwanini tuzike ile barua njema iliyokuwa inasomwa na kila mmoja wetu. Ni kwa kutoingiza mazoea yeyote katika kila jambo tunalofanya, kudumu katika lile tunalofanya itupa mwanga na uzoefu wa kulitenda hilo jambo kwa ufanisi zaidi.
Isiwe jinsi unavyozidi kuwa mzoefu kwenye eneo/nafasi inayokufanya uwavute na wengine, ikakufanya ukawa kiburi na mvivu wa kutofanya vizuri zaidi. Utageuka mfano mbaya wa kutoigwa kutokana na mwenendo wako mbaya ulioanza nao.
Mazoea haya ndio yanawatesa waimbaji wengi wa nyimbo za injili, mazoea haya ndio yanawatesa wahubiri/watumishi/wachugaji/walimu wengi wa Neno la Mungu. Wanaanza vizuri sana na kutengeneza umakini mzuri wa watu wengine lakini wakishapata jina, ile bidii yao iliyowafanya wawepo pale wanaisahau na kuingiza mazoea/ukawaida.
Mungu wetu hatutaki tuwe hivyo badala yake anatutaka tuwe wenye bidii siku zote za maisha yetu, kadri unavyozidi kufanikiwa inapaswa kukupa changamoto ya kufanya vizuri zaidi na zaidi. Lakini ukishaanza kuweka mazoea hata ile bidii ya kuutafuta uso wa Mungu inapotea, umesahau Mungu ndio alikuwa anahusika kukuinua zaidi.
Mazoea haya ndio yanawafanya wengi wetu tuache kusoma Neno la Mungu, tukishasomasoma na tukafika maeneo fulani tunaona tumeshaweza na kuelewa kila kitu. Inatupa kiburi, na kiburi kile kinaondoa hamu ile ya ndani iliyokuwa inatufanya tuendelee kujifunza Neno la Mungu zaidi.
Kuepukana na hili janga, ni kujitahidi kutojiingiza katika mazoea ya aina yeyote yale, hii itakusaidia sana kuendelea kujifunza mengi na kujua mengi zaidi. Mungu ataona unyenyekevu wako kwake na ataendelea kukupa ile haja ya moyo wako, unaweza kuwa ulikuwa unaelewa maandiko Matakatifu kwa kiwango cha chini sana. Ila kupitia bidii yako isiyo na chembe ya kukata tamaa, isiyo na chembe ya dharau, isiyo na chembe ya kujiinua, amini hutotoka kama ulivyokuwa mwanzo.
Hakikisha ndugu aitwaye mazoea anakaa mbali na wewe, ukimruhusu akaanza kukutawala uwe na uhakika itabaki nilikuwaga zamani nasoma sana Neno la Mungu. Lakini sasa husomi sana, na wala huna tena huo moyo wa kuweza kutenga muda wako kwa ajili ya Bwana, na kama upo basi hukusukumi ufanye vitu kwa bidii.
Usikubali kuwa miongoni mwa watu walioanza vizuri wakamaliza vibaya, kuwa miongoni mwa watu walioanza kwa unyonge na sasa wamekuwa imara kwa bidii yao. Narudia tena usiingize mazoea kwa chochote unachokifanya, hutafika mbali na jambo uliloanza nalo.
Kusoma Neno la Mungu ni wajibu wa kila mwenye safari ya kuukulia wokovu, ili ukue kiroho unapaswa kuwa na ratiba ya kusoma Maandiko Matakatifu. Itakujengea uwezo wa kujitambua mbele za Mungu, na kumwona Mungu ni Baba yako anayeweza kukusaidia kile unajua ukimwomba atakupa.
Ujasiri wetu mbele za Mungu wa kumwendea, unaletwa na kujua Neno lake. Kujua Neno la Mungu inatupa nguvu za kudai haki zetu za msingi, ambazo tulijua ni haki kutokuwa nazo. Itafaa nini kujiingiza kwenye mazoea yanayotupelekea kuzika bidii yetu? Haitafaa kitu.
Bila shaka umedaka kitu cha kukusaidia katika usomaji wako wa Neno la Mungu, ulichojifunza kiwe ndio silaha yako ya kumshinda adui mazoea.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa Chapeo Ya Wokovu kupata masomo mengine mazuri zaidi. Usisahau kutushirikisha maoni yako hapo chini kwenye sehemu ya comment, na usiache kuwa miongoni mwa watu wanaohamasisha wengine kwa vitendo kusoma Neno la Mungu.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.