Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona tena. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, ametupa nafasi nyingine ya kwenda kumzalia matunda yaliyo mema.

Watu wanaugua ndani ya mioyo yao kiasi kwamba hata homa ya malaria ni afadhali, unaweza kumwona mtu anatembea barabarani ukafikiri ana amani ila ukikaa naye kwenye mazungumzo ndani ya muda mfupi utagundua ana mizigo mizito.

Unaweza kumwona mtu anazidi kupauka ngozi yake ukafikiri mafuta kumbe kinachompausha ni maumivu ya moyo wake, unaweza kumwona mtu anafanya vitu vya ajabu ajabu watu wakashindwa kumwelewa. Hata yeye mwenyewe wakati mwingine anashindwa kujielewa kwanini anafanya hivyo.

Unaweza kumwona mtu ni mkorofi na anawanyanyasa watu kutokana na nafasi yake, kumbe kinachomfanya awe hivyo ni ndani ya moyo wake kuna shida. Maumivu anayopitia mtu kwenye maisha yake yana mchango mkubwa sana kumbadilisha hali yake ya utu ikatoweka kabisa.

Mtu akikosa utulivu wa moyo wake kwa kuzidiwa na maumivu ya changamoto fulani anayopitia, asipokuwa makini hata ule moyo wa ibada utaondoka kwake. Kuna nafasi kubwa kuondoka kwenye mstari wa Mungu na kuhamia upande mwingine usiompendeza Mungu.

Labda iwe mtu yule anayepitia katika hali ngumu ya kuujeruhi moyo wake, awe ni mtu aliyekuwa mchaji wa Mungu katika roho na kweli. Vinginevyo huyu mtu atafika hatua ataona mambo ya Mungu hayana maana tena kwake.

Wengi wanaugulia ndani kwa ndani lakini kwa mwenekano wa nje wanaonekana wapo salama, mtu ana kazi nzuri ila ukimwona ni kama mtu asiye na kazi kabisa. Mtu ana miradi mingi ya kumwingizia pesa ila ukimwona ni mtu mwenye mateso mengi na inafika wakati mwingine anakosa usingizi, si kwa kuwaza biashara zake. Anafikiri kama ilikuwa ni kuondolewa na pesa angeshaviondoa siku nyingi, kwa kuwa havihitaji pesa anabaki anateseka ndani kwa ndani.

Vijana wengi sana wamejeruhiwa na mahusiano, wamebaki watupu ndani yao hata ile nguvu ya Roho Mtakatifu haimo tena ndani yao. Kwa sababu wamewabeba wadada na wakaka ndani ya mioyo yao, hata ile hamu ya ibada imeondoka ndani yao, hata ile kiu ya maombi haimo tena ndani yao.

Wababa/wamama wengi wanaenda imradi wamefanikiwa kuamka wazima, ila ndani ya mioyo yao wana mateso magumu sana. Usiku mmoja kwao ni kama siku nzima, maana nyumba zao zimegeuka uwanja wa vita, vitanda vyao havilaliki tena, ugomvi usiku kucha hawalali.

Tutapataje kupona ikiwa kila siku tunaingia kanisani na kutoka, na kanisani ukiingia unakutana na mambo mengine zaidi. Mara nyingine watu wanaanza kukutupia lawama kwa kutoeleweka kwako, wakati mwingine hata ofisini kwako wanashindwa kukuelewa. Yaani kila kona unageuka kama kituko.

Lakini ipo siri katika kusoma Neno la Mungu, neno la Mungu linaponya bila kutumia hata panadol, Neno la Mungu linainua moyo wa mtu uliokosa tumaini, Neno la Mungu linaondoa roho ya kisasi ndani yako, Neno la Mungu linaua kabisa chuki ndani yako. Kila eneo la maisha yako uliyoona huwezi tena kusonga mbele, jibu lake utalipata ndani biblia yako.

Umefika hatua ya kukata tamaa na kumwona Mungu hana tena maana kwako, kwa sababu hukuwa na utaratibu wa kulisha moyo wako Neno la Mungu. Wenye bidii ya kulisha mioyo yao Neno la Mungu hawafiki hatua wakaacha kumtukuza Mungu katikati ya shida yao.

Hebu Karibu usome ushuhuda wa huyu ndugu aliyekata tamaa, ila baada ya kuanza kusoma Neno la Mungu moyo wake uliinuliwa kwa upya.

Jina la Bwana lipewe sifa wapendwa.
Ninayo furaha kubwa asubuhi ya leo, kupitia kitabu hiki cha Ayubu nimeponywa sana acha niseme ukweli.
Nimejua kweli njia za Mungu hazichunguziki.
Nilipata jaribu katika ndoa yangu nikaona kuwa ni mwisho wa maisha. Nimekuwa nikiliishi jaribu na sio kumuishi Kristo Yesu.

Kupitia tafakari zenu wana Chapeo ya wokovu, katika Kitabu hiki nimegundua kwa hakika kumbe sio adhabu kwangu ila Mungu anataka roho yangu ipone. Kuthibitisha hilo kafanya moyo wangu kuwa mgumu kushawishika kuwaamini waganga wa kienyeji.
Kanielekeza mahali pamoja tu kwenye neno lake.

Baada ya Yote kutokea nikaona vitu ambavyo sikuwahi kuona;
1. Kiu ya kuomba…nisipoomba nahisi siko sawa.
2. Hamu ya kusoma neno…hapo mwanzo hata kuifungua biblia sikujua.
3. Hamu ya kutafuta nini Mungu anasema…kuingia kundi hili ni matokeo yake.

Kiukweli sitaangalia tatizo la ndoa yangu tena, bali yeye aliyezifanya mbingu na nchi.Namshukuru Mungu ameponya ufahamu wangu.
Nawashukuru wana Chapeo Ya Wokovu wote kwa tafakari zenu.
Nakushukuru kaka Sam kwa mafunuo haya aliyokupatia Mungu, nawe ukatii.

Bwana awabariki wote.
Sifa na utukufu ni kwake.

Huo ni ushuhuda wa ndugu ambaye tupo naye group la wasap, kupitia Neno la Mungu amepona majeraha ya moyo wake. Ukimfuatilia zaidi atakuwa amepita kwenye maombi mengi sana ya kuombewa, ila alivyoamua kuanza kusoma Maandiko Matakatifu aliinua moyo wake kwa upya.

Unaweza kuona ni jambo la kawaida ila kama wewe umewahi kuumizwa na mahusiano ya uchumba au ndoa utakuwa unanielewa vizuri. Hapa tunajifunza kukaa karibu na Mungu inatufanya tupone maumivu mengi sana ndani ya mioyo yetu, cha kushangaza mtu akiumizwa anakaa mbali na Mungu wake.

Kukaa mbali na Mungu unampa nafasi shetani kukupelekesha anavyotaka yeye maana unakuwa huna stamina zozote. Mbaya zaidi uwe mtu uliyekuwa huna mpango wowote wa kujifunza Neno la Mungu. Umeamka siku huna utulivu ndani ya moyo wako, mwambie Mungu akupe utulivu. Na siku umeamka huwezi kusoma kabisa Neno la Mungu mwenyewe, jifunze kwa kuwasikiliza wengine.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.