Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona tena. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana wetu kwa uweza wake mkuu kwetu.
Zipo nyakati tunafika tunakosa ile furaha ya kweli na kuanza kutafuta vitu vya kutufurahisha, ila tunakuja kugundua ilikuwa ni furaha ya muda mfupi. Wakati mwingine tumejikuta tumejiingiza kwenye vitu visivyofaa na vinavyomkosea Mungu kwa kuitafuta furaha ya mioyo yetu.
Unakuta mtu anajilazimisha kunywa pombe ili kuondoa maumivu ya moyo na kuleta furaha ya moyo wake, anashangaa anafanya hivyo lakini anajikuta hali ya kukosa furaha bado ipo pale pale.
Unapojikuta upo katika wakati mgumu alafu hiyo hali inakusukuma kufanya vitu vingine visivyofaa, ujue hapo Mungu hahusiki na hicho kitu. Unapaswa kukataa hilo mapema na kwenda mbele za Mungu wako.
Unaweza kwenda sehemu nzuri za kutuliza mawazo yako ili kurejesha ile furaha ya moyo wako na ukaikosa kabisa, ukakuta bado maumivu yanaendelea. Unaweza kuona kama vile Mungu amekuacha kabisa unapopita nyakati kama hizi, na ndizo nyakati unapaswa kuwa nazo makini sana.
Wengi walioanza vizuri na Yesu Kristo wamefika kipindi wameacha wokovu, ndani yao walikosa ile hamu ya ya kuendelea kufanya ibada na Mungu wao. Ile hamu ya kuomba haikuwa tena ndani yao, ile hamu ya kusoma Neno la Mungu haikuwa tena ndani yao.
Unapofika wakati kama huu usikubali kubebwa na hali hiyo, ikatae kabisa ili uruhusu Mungu awe na wewe hata kwenye jaribu unalopitia. Jaribu lisikufanye ukamchukia Mungu bali furaha yako ya wokovu ikawa yenye nguvu zaidi hata kama maumivu ni makali.
Rejea; Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi. Zaburi 51:12 SUV.
Neno la Mungu linaleta/linarudisha furaha ya kweli; pale unapojikuta upo kwenye wakati ambao huna tumaini na mambo yanaonekana magumu kwako. Neno la Mungu litakurudishia furaha yako, furaha ambayo inakuwa haina kufanana na kitu chochote, kutafakari kwako ukuu wa Mungu kupitia Neno lake inakupa ujasiri wa kusonga mbele.
Neno la Mungu linatengeneza furaha ya kweli; furaha inategenezwa kwa gharama kubwa sana ndio maana hakuna kitu chochote zaidi ya Mungu kinachoweza kutengeneza furaha ya kweli. Vingine ni kuhangaika tu lakini unapokuwa na Neno moyoni mwako, utautafakari ukuu wa Mungu katika maisha yako.
Unapokuwa msomaji wa Neno la Mungu, kuna majeraha sugu yaliyojenga makazi ndani ya moyo wako, yataondolewa kwa jinsi unavyozidi kujifunza Neno la Mungu na kuliweka moyoni mwako. Nakueleza habari za ukweli kabisa, Neno la Mungu linaleta furaha ya kweli, wengi waliojua siri hii wamekuwa watu wapya kabisa.
Rejea; Nimeifurahia njia ya shuhuda zako Kana kwamba ni mali mengi. Nitayatafakari mausia yako, Nami nitaziangalia njia zako. Nitajifurahisha sana kwa amri zako, Sitalisahau neno lako. ZABURI. 119:14-16 SUV.
Umeona hiyo mistari inavyosema, Neno la Mungu ni kweli na hakika, utafurahije juu ya Bwana ikiwa humjui vizuri unayemfurahia. Upo kwenye tatizo gumu alafu uwe na furaha kwa Mungu!! Inakuwa kama vile haingii akilini ila ndio ukweli wenyewe kama utaelewa haya ninayokueleza.
Unapokuwa unasoma Neno la Mungu unapaswa kuelewa haya ili ufurahie usomaji wako wa Neno, nimeshuhudia wengi sana wakipona bila kuombewa baada ya kuanza kusoma Neno la Mungu na kulitafakari. Leo hii wana furaha ya kweli isiyohitaji mtu yeyote kuisukuma au kuifufua au kuileta au kuisababisha.
Maana wapo watu wanatafuta furaha kwa waume/wake zao lakini hawaipati. Lakini wangejua furaha ya kwanza kabisa inapaswa kutoka kwa Mungu mwenyewe, na inakuja pale unapoendelea kujifunza na kulifakari Neno lake.
Mjue sana Mungu uondokane na masumbuko ya moyo wako, unaugua ndani na kukosa furaha ya maisha yako kwa kutokuwa na maarifa ya Neno la Mungu. Kibinadamu utaugua kwa mambo mbalimbali yanayogusa maisha yako ila utakuwa na ujasiri wa kumweleza Mungu hali unayopitia.
Wakati mwingine unayetafuta akuombee hawezi kueleza vizuri mbele za Mungu jinsi unavyojisikia ndani yako, ila wewe mhusika Unaweza kumweleza mambo yako akakusaidia. Utamweleza kwa uzito, kwa sababu wewe ndio mhitaji/mhusika.
Bila shaka kuna hatua umepiga baada ya kusoma ujumbe huu, nikuombe ulifanye Neno la Mungu kama sehemu ya maisha yako. Litakubeba katika maeneo mengi sana ya maisha yako.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, usiache kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.