Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema machoni pa Bwana wetu ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.

Kuwa mwombaji pasipo kulijua Neno la Mungu kuna leta mashaka kwa mwombaji, kwa sababu kuomba pasipo kulijua Neno la Mungu ni hatari kubwa sana kwa mwombaji.

Wote tunajua maombi ni muhimu sana kwa maisha yetu ya wokovu, umuhimu huu unaleta maana kama mwombaji atakuwa ni mtu anayemjua Mungu wake. Usipokazana kumjua Mungu kupitia Neno lake, kuna maeneo utafika utaona maombi hayana msaada kwako.

Wengi sana wamekuwa kwenye maombi ya muda mrefu ila baada ya kumaliza maombi yale, walienda kuanguka kwenye uzinzi/uasherati. Vijana wengi wamekuwa kwenye maombi ya muda mrefu ili Mungu awakutanishe na waume/wake zao, ila utashangaa kijana aliyekuwa kwenye maombi ya kumaanisha(kufunga) anaoa/anaolewa na mtu asiyemjua hata Kristo.

Utajiuliza ndiyo Mungu alimwelekeza aoe/aolewe na mtu anayelikataa hata kusikia jina la Yesu Kristo au aliona vipi. Ndio pale utakuta alidanganywa/alijidanganya kuwa ataweza kumbadilisha wakiingia naye kwenye ndoa. Badala yake hajabadilika na ndoa imekuwa kitanzi cha yeye kumwacha kabisa Yesu Kristo na kuwa mateso yasiyo na kikomo, na wengine wameua huduma zao.

Kuomba pasipo Neno la Mungu moyoni mwako kuna maeneo mengi sana utashindwa kuvuka, kuna muda unaweza kuomba na Mungu akikujibu utashindwa kuelewa kama amekujibu. Kuna vitu unaweza kuomba na palepale shetani akachomekea majibu yake, sasa usipokuwa na Neno la Mungu kutambua hizo ni hila za shetani. Hata akija mtu akakuambia huyu sio Mungu aliyekujibu utakataa kabisa, hapo ukute Mungu amemtuma mtumishi wake kukupa kweli wa hayo majibu sio sahihi.

Lakini unapokuwa na Neno la Mungu moyoni mwako, utakuwa mnyenyekevu na mtiifu wa kujirudi haraka hata pale utakapojua ulikosea sehemu ukijua ndio Mungu amehusika. Lakini usipokuwa na Neno la Mungu utaona maombi yako yamejibiwa, na utakuwa mgumu wa kuelewa hata pale watu wa Mungu wakija kukuambia hapo sio sahihi.

Haiwezekani dada umemwomba Mungu akupe mume alafu anakukutanisha na mwanaume ukajua ndiye mume wako, na ukampitisha moyoni mwako, na ukaanza kutangaza umepata wa kukuoa. Alafu mwanaume yule kila siku anakusumbua mfanye naye mapenzi, wakati mwingine ametaka kukubaka pale ulipomkatalia na anakuona mshamba na hujielewi.

Haiwezekani kaka umemwomba Mungu akupe mke alafu anakukutanisha na mdada ambaye ana wanaume zaidi ya watatu na wote amewambia anawapenda na wataishi naye. Na wakati mwingine anafanya nao uchafu ila kwako anajifanya ametulia na hapendi kabisa mmkosee Mungu kwa tendo la uasherati.

Hapa usipokuwa na Neno la Mungu moyoni mwako, kila Mungu akijaribu kusema na wewe na kukupa picha ya unayeenda kuishi naye. Lazima utakataa kwa sababu moyoni mwako upo mtupu, na hutakuwa na upembuzi yakinifu wa kupembua lililo baya na lililo zuri. Utasema ina maana wewe hujui mema na mabaya la hasha ninachosema hapa ni mambo ya rohoni yanayohitaji msingi wa Neno la Mungu.

Wengi sana wameanguka eneo hili, na ukimuuliza si uliona kabisa mzigo ulionao si wako? Atakujibu ndio niliona ila nilijua atabadilika tukiingia kwenye ndoa. Aliyeokoka hawezi kuolewa kwa kulazimisha mimba, aliyeokoka kisawasawa na Neno la Mungu limo ndani yake hawezi kulazimisha kuzini kwanza ndipo aishi naye.

Kwa mtu aliye na Neno la Mungu moyoni mwake na aliye na utii katika Neno la Mungu, akisikia mkaka anaingiza habari za mapenzi wakati hajafikia hatua ya kufanya hivyo. Moja kwa moja atajua amekutana na tango pori lenyewe bila kuuliza kwa mchungaji wake huyu kaka vipi mbona simwelewi. Yeye kama yeye atamsimamisha na kumwambia amekosea njia akatafute mwingine wa saizi yake.

Mwombaji wa kweli unapaswa kuwa na Neno la Mungu, na Neno la Mungu utakuwa nalo kwa kusoma biblia yako kila wakati. Unapaswa kujua ahadi za Mungu juu ya maisha yako, hata unapokwama sehemu katika maombi yako, lipo Neno litakujia na litakuondoa eneo ulipokwama.

Usikazane kuomba alafu ndani yako huna Neno la Mungu, mwombaji lazima awe na kiu ya kusoma Neno la Mungu kujua ahadi za anayemwomba kila siku. Pasipo Neno la Mungu utaingizwa kichakani na shetani ukijua Mungu amesema na wewe kumbe hila za baba wa maovu.

Ndani ya maombi wengine wamepewa huduma za kiutumishi na shetani wakizani ni Mungu, kumbe utumishi wao ni kwa ajili ya kumzalia shetani matunda kwa kuwapotosha watu wa Mungu, kwenye kweli ya Mungu. Na wanatumika kwa bidii sana kupotosha maandiko Matakatifu wakijua wao ndio wanajua zaidi.

Uzuri wa Neno la Mungu linakupa hadi vitu/mambo ya kuomba na kuombea, na unapoomba unakuwa huna mashaka yeyote kwa sababu unajua Baba amekupa maelekezo mazuri kupitia Neno lake.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.