Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali kingine cha kuiona leo. Bila shaka wengi waliitamani Leo na wengi walitamani ndugu zao waione leo, ila haikuwezekana, lakini mimi na wewe tumepata fursa hii adimu sana. Tunapaswa kuitumia kwa uaminifu mkubwa mbele za Bwana ili kumzalia matunda yaliyo mema.

Tunapokuwa ndani ya maisha ya wokovu kuna sehemu tunafika wakati tunakutana na mafundisho yakatufedheihesha mioyo yetu. Na kufika hatua kuona wokovu ni mgumu na haufai kwenda nao, na wakati mwingine tumefikiri kumwamini Yesu Kristo tulifanya makosa.

Mafundisho mengine yanaweza kututoa kabisa kwenye mstari wa Neno la Mungu na kupotoshwa ile imani yetu sahihi tuliyokuwa nayo. Hii ni kwa sababu imani yetu ilitegemea sana wengine pasipo wenyewe kulijua vizuri Neno la Mungu.

Kuvurungwa kwa mtu na kuiacha njia yake sahihi, ni kutokana na mtu kukosa maarifa sahihi ambayo ni Neno la Mungu. Kukosa kwako Neno la Mungu utafika kipindi utaona hata upagani nao ni imani sahihi ya mtu kwenda kuishi maisha ya umilele baada ya haya.

Shida inakuja pale wewe unayemwamini Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wako, unapoambiwa wote Mungu wetu ni mmoja na unajua Mungu wetu ni mmoja na hachanganywi na miungu mingine.

Unaweza kupata utata ndani ya moyo wako mpaka ukashangaa imekaaje hii, ndio maana unakuta mtu ni mkristo lakini bado anashiriki na marafiki zake ibada za miungu mingine. Alichoaminishwa yeye ni kuwa wote Mungu wetu ni mmoja, ni kweli wote Mungu wetu ni mmoja, mbona hawamtaki na wanaabudu miungu yao na kwenda kinyume na yule wanayesema ni mmoja?

Usipolielewa Neno la Mungu utakuwa mtu wa kutangatanga kila siku ukijua upo sahihi kumbe unamkosea Mungu wako aliye hai. Utawapendeza marafiki zako kwa kufanya wanayotaka wao ila ujue utakuwa umkasirisha sana Mungu wako, maana yeye ni Mungu mwenye wivu asiyependa kuchanganywa na mungu mwingine.

Vipo vitu vinaweza kuonekana vya kawaida, ila kutokujua kwako Neno la Mungu vinaweza kukufanya ukabaki njia panda na wakati mwingine umeona kama vile kumwamini kwako Yesu Kristo. Unakuwa kama vile ulikosea kufanya hivyo, hii ni kwa sababu ya mtu mmoja amekuja akakupindisha na andiko kidogo kutoka ndani ya biblia.

Hali kama hizi zinaweza kukufanya ukapata mkanganyiko mkubwa sana ndani ya moyo wako, kwa sababu ya uchanga wako wa kiroho. Ila mtu aliyeshiba Neno la Mungu moyoni mwake, hawezi kusumbuliwa na mafundisho feki yenye nia ya kumwondoa kwenye njia sahihi ya Yesu Kristo.

Fahamu wapo mafundi wa kuipindisha kweli ya Mungu kutumia hiyohiyo biblia yako unayoenda nayo kanisani kila mara bila kuisoma. Wanajua wasipoitumia hiyo unaweza usibanduke haraka, ila shetani anajua hilo ndio maana anaweza kutumia njia ile uliyoipita na kuiamini wewe kukuondoa kwenye kusudi sahihi la Mungu wako.

Kumpokea Yesu Kristo haitoshi ikiwa hutomjua vizuri uliyempokea na kumkiri, huenda ulimpokea Kristo kwa sababu ya shida fulani, huenda ulimpokea Kristo baada ya kuona kuna wakaka/wadada wazuri wa kuoa/kukuoa. Zipo sababu nyingi zinazomfanya mtu ampokee Yesu Kristo, baada ya Kumpokea Yesu Kristo unapaswa kujifunza Neno la Mungu ili usije ukarudi maisha yako ya kale.

Tusipopenda kujifunza Neno la Mungu tutakuwa watu wenye mashaka makubwa juu ya imani yetu, anayejifunza Neno la Mungu hawezi kulishwa mafundisho potofu akayaamini, anayejifunza Neno la Mungu hawezi kushikilia kitu moyoni mwake kinachomtenganisha na Mungu wake.

Kusoma Neno la Mungu kunakupa ujasiri, ujasiri ule ndio unaoondoa mahangaiko ya moyo wako. Haijalishi utakutana na mazingira magumu ya kujaribiwa kwako, hutoweza kuacha kumwamini Mungu kwa kupewa mawazo mbalimbali yanayokuonyesha una mwamini Mungu asiye halisi.

Acha kubaki njia panda, acha kuonewa na maneno ya kukupotosha na kujikuta unapata mahangaiko ndani ya moyo wako. Mjue Mungu wako wa kweli kupitia Maandiko Matakatifu, pasipo kusukumwa na mtu yeyote jisukume mwenyewe kuitafuta kweli ya Mungu. Una wasiwasi gani wakati una Roho Mtakatifu ndani yako wa kukusaidia kuelewa vizuri Maandiko Matakatifu.

Bila shaka kuna kitu umekipata kupitia ujumbe huu, kile umejifunza nenda kakifanyie kazi utaona mabadiliko makubwa sana ndani ya maisha yako ya wokovu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.