Kabla ya kumjua Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yetu, tulikuwa tunaenda kama dunia inavyotaka tuenende kwa tabia fulani chafu. Kutojua kwetu kuwa tulikuwa tumefungwa akili zetu, ili tufanye ujinga huku tukijiona wajanja sana kupita waliomjua Kristo kama Bwana na Mwokozi wao.
Zipo tabia za wazazi wetu tunaweza kuwa tumeziinga, zikawa mwiba kwetu, utaachaje kuiga tabia mbaya wakati umekua una mwona mama yako anampiga baba yako. Utashindwaje kuwa na foleni ya wanaume, wakati unakua ulikuwa unamwona mama yako akipishanisha wanaume kutwa nzima.
Utaachaje kunywa pombe wakati baba yako alikuwa anakunywa kila siku nyumani, na zingine alikuwa anaziweka ndani ya friji. Utaachaje kuwa mvutaji mzuri wa sigara wakati kila siku baba yako alikuwa anakutuma ukamnunulie, alafu uje umeiwasha hiyo singira.
Utaachaje kuwa omba omba wakati mzazi wako alikuwa anakufundisha hiyo tabia mbaya ya kuwaomba watu pesa. Utaachaje kuwa tapeli wa kuwachukulia watu pesa zao ukiwadanganya utawalipa, lakini huwalipi. Ni kwa sababu ulifundishwa hiyo tabia na mlezi/mzazi wako, kwa kumwona akiwafanyia wengine hivyo.
Utaachaje kutoa mimba kila siku mpaka umefikia hatua umeng’oa na kizazi, ni kwa sababu umerithishwa roho chafu na mzazi wako aliyekuwa anafanya huo upuuzi.
Yapo makosa mengi yaliyowahi kufanywa na wazazi wetu, yakatuambikiza na sisi, huenda isiwe wazee wetu ila marafiki tuliokutana nao huko nje. Kwa kuwa hatukuwekewa misingi mizuri na wazazi wetu, tunajikuta tumeingizwa kwenye maovu yanayomchukiza Mungu wetu.
Neno la Mungu linatuasa hivi;
Wala msiwe kama baba zenu, na kama ndugu zenu, waliomwasi BWANA, Mungu wa baba zao, hata akawatoa kuwa ushangao, kama mwonavyo. Msiwe sasa wenye shingo ngumu kama baba zenu; lakini mjitoe kwa BWANA, mkaingie katika patakatifu pake, alipopatakasa milele, mkamtumikie BWANA, Mungu wenu, hasira yake kali iwageukie mbali. 2 NYA. 30:7-8 SUV
Usiwe na tabia kama za wazazi na ndugu zako, uwe na tabia njema ya kumpenda Mungu, usiwe na tabia za kivuvi zinazokupelekea uone mambo ya KiMungu ni kawaida kawaida. Uwe na moyo wa kumpenda Mungu, maana wewe si wa kwenye giza tena, wewe ni mwana wa nuru.
Usifanane na watu wasiopenda kusoma Neno la Mungu, fanana tabia zako na watu wanaosoma Neno La Mungu. Kufanya hivyo utamjua Mungu vizuri zaidi kupitia neno lake, na utayaishi yale unayoelekezwa na Neno la Mungu.
Ikiwa unajiona una tabia chafuchafu za matusi kama vile hujaokoka, unapaswa kukaa chini na kujichunguza kwa upya. Kama una tabia za uasherati na uzinzi, na wakati unasema umeokoka, unapaswa kujirudi kwa upya mbele za Mungu.
Chochote unachokifanya kama mtu aliyeutumwani mwa dhambi, unapaswa kujichunguza kwa upya ujue unapokosea ni wapi. Ili ujue namna ya kuepukana na hilo balaa la kukosesha mahusiano yako na Mungu.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Usiache kutembelea mtandao wetu,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com