Kutaka kupata vitu vingi, kutaka Mungu akuinue zaidi kwenye huduma yako, kazi yako, masomo yako, unahitaji kuwa na kitu kwanza unachofanya au ulichonacho mkononi mwako.

Badala yake wengi tunataka Mungu atufanye tuwe wafanyakazi wenye mafanikio makubwa, lakini ile kazi ndogo tuliyonayo sasa tunaifanya kizembe. Hatuna uaminifu wowote kwa kile kidogo ambacho tumepata nafasi ya kuwa nacho, lakini pamoja hayo bado tunataka Mungu atupandishe juu zaidi.

Mtu ana huduma ndani yake, na anatamani Mungu ampandishe viwango vya juu zaidi, lakini pale alipo anafanya huduma kizembe, hajali sana mambo ya Mungu, hajibidiishi kwenye Neno la Mungu, hana muda wa maombi, ibadani anaenda akitaka mwenyewe. Alafu amekaa anataka Mungu amwinue viwango vya juu zaidi, lakini kile Mungu alichompa haikutumii ipasavyo.

Ndugu yangu, kama unataka hatua nyingine zaidi, unahitaji kuonyesha kile kidogo ulichonacho unakimudu vizuri, sio kidogo kinakushinda alafu unataka kingine kikubwa zaidi.

Kipo kipawa/kipaji/karama Mungu ameweka ndani yako, kabla hujaanza kumwomba Mungu akuinue zaidi ya hapo ulipo, onyesha kumudu na kuzalisha matunda ya kutosha kutokana na hatua yako ndogo uliyonayo. Ukionyesha uaminifu kwa kidogo, ni ishara nzuri kwako unaweza kuwa mwaminifu na kikubwa pia.

Hii ni kanuni ya kiMungu, huwezi kuikwepa, kama una kitu tayari na unakifanyia kazi, utapewa zaidi, ila kama unacho kidogo alafu hukifanyii kazi. Uwe na uhakika hata hicho kidogo ulichonacho utanyang’anywa, na utabaki mikono mitupu.

Rejea: Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyanganywa hata alicho nacho. LK. 19:26 SUV.

Usidharau hicho kidogo ulichonacho, hicho kitu kidogo ulichonacho sasa kitakufanya upate kingine zaidi, huo ni mtaji wako unapaswa kuutunza vizuri. Tunza kitu chako kidogo ulichonacho, sio kukitunza tu bila kukifanyia kazi, hakikisha kinazaa matunda zaidi ya hapo.

Hicho kipawa chako kidogo ulichonacho sasa kitakuwa kikubwa kwa kuzaa mambo makubwa zaidi ndani yako, kama utakifanyia kazi hicho kidogo ulichonacho sasa. Bila kuonyesha bidii zaidi katika hicho kidogo, utakosa vyote, yaani hata hicho kidogo ulichokuwa nacho utanyang’anywa.

Usiseme mimi sina kipawa/kipaji/karama yeyote, huo ni uongo, kila mmoja ana mtaji wake amepewa na Mungu, yupo amepewa mtaji wa sh. 10,000, yupo amepewa mtaji wa sh. 5,000, na yupo amepewa mtaji wa sh. 2,000. Kila mmoja kutokana na uwezo wake, hawa wote watapata mara mbili yake kama watafanyia kazi mtaji waliopewa.

Huwezi kusema mimi nimezaliwa sina kipawa chochote, huko ni kujidanganya mwenyewe, na ukiendelea kujifariji hivyo, utashangaa kuna kitu ulikuwa unakifanya watu wanakufurahia sana. Baada ya muda fulani kupita ukija kujaribu kukifanya kama ulivyokuwa unafanya, utashangaa huwezi kufanya tena, ukishaona hivyo usianze kutafuta mchawi, wakati mchawi ni wewe mwenyewe.

Mungu akusaidie ukitumie vizuri kile kidogo ulichonacho ndani yako, narudia tena kutafuta kupata zaidi wakati kile kidogo ulichopewa hujakizalisha kwa chochote. Uwe na uhakika utaingia hasara ya vyote, kile ulichokuwa nacho utanyang’anywa na kile kikubwa ulichokuwa unakitamani hutakipata.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com
+255759808081