Haleluya;
Kuna msemo unasema, usimpe mtu samaki, mfundishe namna ya kuvua samaki.
Unaweza kuona ni msemo wa kawaida sana, ila ni msemo uliobeba maana kubwa sana, ikiwa utautafari kwa kina. Ila ni msemo rahisi sana kama utauchukulia ni msemo kama misemo mingine.
Heri kutumia nguvu kubwa kumfundisha mwanao namna ya kufanya au kujishughulisha ili aweze kupata jambo fulani. Usimpe mwanao urahisi sana, hatojua uthamani wa vitu.
Unaweza kuweka utaratibu mzuri tu nyumbani, vyombo vya chakula mnapomaliza kula chakula cha usiku, wa kuosha sio dada wa kazi ni yeye mtoto. Mpangie utaratibu wa yeye kuosha hivyo vyombo na uhakikishe kweli hilo analifanya.
Weka utaratibu wa watoto wako, awe wa kiume au awe kike, hakikisha wote wanajua kupika chakula mnachoweza kula familia nzima. Usiwalee kimayai mayai sana, utakuwa unawaharibu mwenyewe kwa kutowapa elimu ya maisha.
Weka utaratibu wa watoto wako kabla ya kulala, mnakuwa na ratiba ya kusoma Neno la Mungu kwa ufupi. Na kufanya sala ya pamoja, ikiwezekana weka zamu ya kila mmoja kutoa NENO. Utawajengea nidhamu binafsi ya kujiamini, na kuanza kuwafanya kuwa watumishi wazuri wa Mungu, na kuwajengea kumweshimu Mungu wao.
Weka utaratibu wa watoto wako wa kusoma Neno la Mungu, wape mtiririko kama huu tunaoufanya hapa Chapeo Ya wokovu whatsApp group. Hakikisha kila mmoja anasoma sura uliyompangia na kukueleza amejifunza nini katika sura hiyo.
Kujenga msingi imara mapema kabla ya kusimamisha ukuta wa nyumba, ni heri kuliko ukuta ulionakishiwa kwa marumaru safi huku msingi ukiwa mbofu.
Kumjengea mwamini namna ya kusimama mwenyewe na Mungu, bila kumtegemea mchungaji, mtume, nabii, mwalimu na mwinjilisti. Ni msingi imara na bora katika maisha yake, maana umempa msingi wa maarifa utakaomsaidia siku zote za maisha yake hata wewe usipokuwepo.
Wengi huwa hatukumbuki hilo kumpa mtu elimu/maarifa ya kuweza kujisimamia mwenyewe. Tunawafundisha watu kuendelea kuwa wategemezi, badala yake tunazidi kuwa na kizazi tegemezi kisichoweza kusimama kwa miguu yake chenyewe.
Leo tunajifunza umhimu wa kusoma Neno la Mungu, ni wajibu wa kila mmoja kujua hili. Hakuna wa kumsubiri mwingine asome na wengine tujihisi tumesoma, kila mmoja anapaswa kusoma.
Usipende sana kutoa vitu pasipo kumpa mtu elimu/maarifa, unaweza kumsaidia mtu ushauri wa namna ya kukabiliana na changamoto ngumu. Kuliko kutumia udhaifu wake kumfanya tegemezi kwako, akashindwa kukabiliana na changamoto za maisha yake.
Rejea: Pokea MAFUNDISHO yangu, wala si FEDHA, Na MAARIFA kuliko DHAHABU safi. MIT. 8:10 SUV
Fedha sio suluhisho endelevu la kumsaidia mwenye shida, unaweza kumsaidia leo, kesho akarudi tena na shida ile ile. Ila ungempa elimu ya namna ya kuzalisha hicho kiasi ulichompa, ingekuwa bora zaidi kuliko kutoa msaada kila siku, ipo siku utakuwa huna.
Siku nyingine hutokuwa na uwezo wa kumpa fedha, na ukija kumwambia huna ataona umemnyima. Maana hajui kuna kukosa, na hilo kosa ni lako kwa sababu hukumfundisha mapema.
Mama mfundishe binti yako mapema namna ya kuishi na mume wake, usisubiri afike siku ya harusi ndio unaanza kumpa mahusia, usisubiri ashindwane na mume wake uje usuhulishe ndoa yake. Utakuwa umechelewa sana na wakati ulikuwa na muda wa kutosha kukaa naye kumfundisha.
Baba mfundishe kijana wako wa kiume namna ya kumtunza mke wake, namna ya kuishi na mke wake kwa akili, namna ya kukabiliana na changamoto za ndoa. Nenda mbali zaidi, mfundishe namna ya kutafuta pesa bila kuacha kumwambia mafanikio yake yamhusishe Mungu asilimia zote.
Mzazi anza mapema kuwafundisha watoto wako kumtolea Mungu sadaka, namna ya kuwasaidia wahitaji, namna ya kuwahurumia wengine, na namna ya kuwasemehe waliowakosea.
Mafundisho ni muhimu sana, fedha na dhahabu ni matokeo tu ya mtu mwenye bidii ya kazi. Ila elimu ni bora zaidi kumpandia mtu, hili usije ukalisahau maisha yako yote.
Ana heri mzazi yule anayehakikisha watoto wake wanapata mafundisho sahihi ya Neno la Mungu. Mwalimu mzuri ni yule anayemfundisha mwanafunzi wake vitu vitakavyoenda kumsaidia katika maisha yake.
Na ili umpandie mtu mafundisho mazuri na sahihi, vizuri ukayaishi hayo unayowafundisha wengine. Kuna wakati unaowafundisha watahitaji kujifunza kupitia matendo yako. Ni hatari kama watashuhudia yale unayoyasema na kuwafundisha, wewe unaenda kinyume chake.
Jifunze kutafuta maarifa sahihi kabla hujakimbilia kitu na kukiamini hicho kitu.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
www.chapeotz.com
chapeo@chapeotz.com
+255759808081