“Kwa maana wataondoka Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, watatoa ishara na maajabu, wapate kuwadanganya, kama yamkini, hata hao wateule”, Mk 13:22 SUV.
Sio jambo la kuficha na sio siri tena kuhusu hili, siku za leo ndani ya makanisa yetu kuna wahudumu wa neno la Mungu wenye roho na maisha kama ya wale walimu wa sheria za Mungu waliopotoka kipindi cha Yesu.
“Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule”, Mt 24:24 SUV.
Yesu anaonya sana kuhusu hili, na kutupa tahadhari juu ya hili, kuwa si kila anayemkiri Kristo ni mwamini wa kweli, na sio wakristo wote ni wamishenari, wachungaji, wainjilisti, walimu, mashemasi na watenda kazi katika shamba lake.
Wanaweza kuonekana kwa nje ni watumishi wa Mungu wa kweli, na wakawa wanakazia au wanasisitiza sana ujumbe wao kwenye msingi wa neno la Mungu na kujiweka katika viwango vya juu vya haki.
Wanaweza kuonekana kuwa wanahusika kwa dhati juu ya kazi ya Mungu na ufalme wake, wakionyesha shauku kubwa katika wokovu kwa waliopotea au wasioamini huku wakikiri kwa uwazi upendo wa Kristo kwa watu wote.
Wanaweza kuonekana ni watumishi wakubwa wa Mungu, viongozi wa kiroho wanaostahili kuhemishiwa na kusifiwa, wakionyesha kuwa wametiwa mafuta na Roho Mtakatifu. Wakijiona wanaweza kutenda miujiza, kuwa na mafanikio makubwa, na kuona watu wengi wanaweza kuwafuata wao.
“Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”, Mt 7:21-23 SUV.
Elewa watu wa namna hii sio watu waliotokea pasipo julikana, na sio wanajiendea tu wao wenyewe, wanao mababa zao wa kiroho wanaowaelekeza na kuwaelea namna ya kufanya huduma zao.
“Nikatambua, na tazama, siye Mungu aliyemtuma; lakini amefanya unabii huu kinyume changu; nao Tobia na Sanbalati ndio waliomwajiri”, Neh 6:12 SUV.
Watu wa namna hii wanaolaghai watu kwa mafundisho yao ya uongo, kwanza kabisa walianza kupata nafasi hii ya ushawishi kanisani kwa namna hii;
Kwanza, baadhi ya walimu au wahubiri wa uongo wanaanza huduma zao vizuri, katika ukweli, usafi na Imani ya kweli katika Kristo. Baadaye sasa kutokana na kiburi chao kuinuka, tamaa zao mbaya, na kutotaka kushauriwa na baba zao wa kiroho.
Kinachokuja kutokea kwao kule kumpenda kwao Kristo hufa polepole, baadaye wanatengwa na ufalme wa Mungu kutokana na kuiacha kweli yake na kuyageukia mambo yasiyofaa mbele zake.
Watu wa namna hii hufanyika vyombo na watenda kazi wa Shetani, huku wakijifanya kuwa wao ni watumishi wa Mungu wanaosimamia haki.
“Kwa hiyo basi si ajabu, kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili”, 2 Wakorintho 11:15 NEN.
Pili, unapaswa kufahamu kuwa walimu au wahubiri wa uongo kamwe hawajawahi kuwa waamini wa kweli wa Kristo. Asije mtu akakudanganya kuwa hao ni watumishi wazuri wa Mungu, ukawaamini na kuwasikiliza yale wanayokutaka ufanye.
Shetani amewapandikiza kanisani tangu mwanzo wa huduma yao, wakitumia vipaji vyao kujinufaisha wao wenyewe na kuwa mafanikio yao ya kimwili. Sio vibaya kuwa na mafanikio ila yanapaswa kuwa katika njia sahihi.
Mkakati wa shetani ni kuwaweka katika nafasi ya umaarufu mkubwa ili waweze kudhoofisha kazi ya kweli ya Kristo kwa waamini. Wote tunajua watu maarufu ndio wanaoaminika haraka, sasa Shetani anajua akiwatumia, Injili ya kweli itapata madhara na jina la Yesu litaaibishwa waziwazi.
Yesu aliwaonya sana wanafunzi wake na kuwarudia mara kwa mara kuhusu hili kuwa wawe macho na walimu na wahubiri wa uongo, wasije wakawapotosha.
“Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali”, Mt 7:15 SUV.
Tukiwa waamini wazuri wa Yesu tunapaswa kuwapima walimu, wahubiri na viongozi wa kanisa. Je, wanaenda sawasawa na neno la Mungu? Hilo ni la muhimu sana, hatupaswi kuwa wakristo wa jumla bila kupima mafundisho yao kwa maandiko matakatifu.
Hatua 5 za kufuata ili kuweza kuwapima na kuwatambua walimu wa uongo au manabii wa uongo;
- Angalia tabia zao na uzipambanue. Ili uweze kumtambua nabii wa uongo au mwalimu wa uongo, angalia ana juhudi katika maombi?, anaonesha kujikabidhi kwa Mungu kwa dhati na usafi? Tunda la Roho linajidhihirisha kwake? (Gal 5:22-23).
Anawapenda wenye dhambi na kuchukia uovu wao na kupenda haki? Anakemea dhambi bila uoga au anahubiri tu mafanikio na mengine ila dhambi anaiacha ikitendeka kwa uwazi?
“Basi, kwa maonyo mengine mengi Yohana aliwasihi na kuwahubiria watu Habari Njema. Lakini Yohana alipomkemea Mfalme Herode kuhusu uhusiano wake na Herodia, mke wa ndugu yake, na maovu mengine aliyokuwa amefanya, Herode aliongezea jambo hili kwa hayo mengine yote: alimfunga Yohana gerezani”, Luka 3:18-20 NEN.
- Angalia kiwango chao cha kuyategemea Maandiko Matakatifu.
Kama kuna jambo la msingi kwa mhubiri au mwalimu au mtumishi yeyote ni kuthamini neno la Mungu, kulimiani na kujua kuwa katika agano la kale na jipya, maandiko yote yamevuviwa na Roho Mtakatifu na tunapaswa kuyatii mafundisho yake.
“Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia. Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu. Maana yeye ampaye salamu azishiriki kazi zake mbovu”, 2 Yoh 1:9-11 SUV.
- Pima tunda la Roho katika maisha yao na ujumbe wao.
Walimu na wahubiri wa uongo siku zote hawawafanyi waongofu wapya walijue neno la Mungu sawasawa na wajue kujisimamia katika Imani pasipo kuwategemea wao.
Siku zote wao huwafanya washirika au waumini wawe tegemezi kwao kwa kila kitu, washirika wanakuwa ni watu ambao hawawezi hata kujiombea hadi waombewe na nabii wao. Ukiona hivyo ujue huyo sio mtenda kazi wa Mungu.
- Angalia dhamira yao.
Kiongozi wa kweli hutafuta kufanya mambo haya; kumtukuza Kristo katika huduma yake na sio yeye kutukuzwa (2Kor 8:23), kuliongoza kanisa katika hali ya utakatifu, kuwarejesha wale waliopotea njia ya kweli, kuitangaza, kuitetea, na kuihubiri injili ya kweli ya Kristo (Lk 3:18-20). - Pima uadilifu/nidhamu yao juu ya fedha ya Bwana.
Zile sadaka, vikumi, malimbuko, mavuno, na machangizo mengine wanakataa kujichukulia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili yao wenyewe?
Wanatunza fedha zote za kanisa kwa uadilifu? Wanawajibika kuiendeleza kazi ya Mungu katika maeneo ambayo yanahitaji injili kulingana na maandiko matakatifu? (1Tim 6:9-10, 3:3).
Kama wanajinufaisha wao tu, na kazi ya Mungu haisongi mbele, ujue huyo ana wito mwingine na sio wa Mungu. Wana wa Mungu hawana ulafi huo wa kula na kujinufaisha wao tu huku kazi ya Bwana haiendi mbele.
Unapaswa kuelewa kuwa pamoja na jitihada zote hizi za kuwatambua walimu na manabii wa uongo, bado watakuwepo walimu wa uongo ndani ya kanisa, ambao kwa msaada wa Shetani hutaweza kuwatambua kabisa hadi pale Mungu atakapoamua mwenyewe kuwafunua na kuwaweka wazi.
Sikuambii haya ili kukuchanganya, uelewa na ujiweke vizuri mbele za Mungu, hakikisha unajaa neno la Mungu moyoni mwako, ili kuweza kuzibaini baadhi ya mbinu za Shetani kupitia walimu na manabii au wahubiri wa uongo.
Mwisho, nakukaribisha kwenye kundi la kusoma neno la Mungu kila siku na kushirikishana tafakari zetu kwa njia ya wasap. Ukiwa na kiu ya kusoma neno na unapenda kuungana na wandugu wengine, wasiliana nasi kwa wasap +255759808081.
Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest