Mara ngapi umesikia habari mbaya kwa mtu fulani unayemfahamu kabisa, habari hizo zikawa zina lengo la kuondoa uhai wake. Wewe kama mtu uliyeokoka, ulichukua hatua gani ya kuokoa maisha ya mtu yule?

Mara ngapi umesikia watu wakipanga mabaya juu ya mtu fulani, huenda ulisikia wakipanga kuweka sumu kwenye chakula atakachokula. Na wewe ukanasa mazungumzo hayo, ulitumia njia gani kuhakikisha mpango huo wa kumwekea sumu haufanikiwi.

Mara ngapi umesikia habari mbaya ofisini kwako juu ya mtu fulani unayemfahamu, ukasimama kama mtu uliyeokoka kuhakikisha mpango huo unaopagwa haufanikiwi. Kwa kwenda kutoa taarifa kwa mhusika au mahali panapohusika ili kulinda usalama wake.

Mara ngapi umesikia hatari fulani inakuja, baada ya kusikia hayo ukaamua kuwaambia wale wanaohusika na kile kinachokuja mbele yao. Na kweli kilitokea kile ulichosikia kitatokea.

Mara ngapi umesikia mpango wa watu kwenda kuiba mali za fulani, baada ya kusikia huo mpango mbaya ukachukua hatua haraka kwenda kumweleza mhusika anayetarajiwa kufanyiwa kitendo hicho kibaya.

Au wewe huwa unaogopa kuonekana mchonganishi, au wewe huwa unaogopa kuonekana mbaya, huwa unaona bora kukaa kimya. Alafu mtu huyo anatokewa na kitu kile kile ulichopata taarifa mapema kabisa, ukaamua kukaa kimya.

Kama umekuwa ukikalia kimya mipango mibaya inayopangwa na watu juu ya wengine wasio na hatia, unapaswa kujua kuwa ulikuwa unakosea sana. Na unapaswa kutubu juu ya hilo, hukupaswa kukaa kimya wakati uhai wa mtu umesikia kwa masikio yako upo hatarini.

Huenda umewahi kusikia watu wanapanga mabaya juu ya kuvuruga amani juu ya ndoa ya wapendwa fulani, kwa kuwa hutaki kuonekana mbaya. Ukakaa kimya, na mwisho ule mpango ukatimia kuharibu hiyo ndoa, au Mungu akaamua kuingilia kati baada ya kukuona wewe umekaa kimya wakati aliruhusu ulisikie hilo.

Hili tunajifunza kwa Mjomba wake Paulo, kuna mpango mbaya ulikuwa unapangwa juu ya mtume Paulo, wakati watu hao wanapanga mabaya juu ya mtumishi wa Mungu Paulo. Mjomba wake alinasa hayo mazungumzo yao ya kutaka kumuua mtume Paulo.

Alivyosikia mpango huo wa kutaka kumuua Paulo, alienda haraka kwa Paulo kumpa taarifa zile juu ya mpango uliopagwa juu yake. Na taarifa zile zilifanya mpango wa mauji juu ya Paulo usiweze kufanikiwa kwa siku hiyo.

Rejea: Mjomba wake Paulo akasikia habari za kuotea kwao, akaenda akaingia ndani ya ngome akampasha Paulo habari. Paulo akamwita akida mmoja, akasema, Mchukue kijana huyu kwa jemadari; maana ana neno la kumwarifu. MDO 23:16‭-‬17 SUV.

Unaona hapo ndugu yangu, ndio maana nilianza kukuuliza mara ngapi Mungu ameruhusu umesikia mpango mbaya juu ya mtu fulani unayemfahamu. Unaweza kuwa umesikia mara nyingi ila umekuwa mtu wa kupuuza, kufanya hivyo ulikuwa unakosea sana.

Mungu anaporuhusu usikie mipango yeyote mibaya juu ya mtu fulani, haijalishi hao wanaopanga huo mpango huwa mnashirikiana mambo fulani. Hakikisha unatoa taarifa haraka kuokoa maisha ya huyo mtu.

Usiseme atajua mwenyewe, huo sio moyo wa mtu aliyeokoka, mtu mwenye Neno la Mungu la kutosha moyoni mwake, huo ni upagani. Kupata taarifa mbaya juu ya mtu fulani alafu unakaa nazo kimya, usije ukafanya hivyo kama hukuwahi kufanya hivyo.

Rejea: Basi yule jemadari akamwacha kijana aende zake, akimwagiza, Usimwambie mtu awaye yote ya kwamba umeniarifu haya.  Akawaita maakida wawili, akasema, Wekeni tayari askari mia mbili kwenda Kaisaria, na askari wapanda farasi sabini, na wenye mikuki mia mbili, kwa saa tatu ya usiku. Akawaambia kuweka wanyama tayari wampandishe Paulo, na kumchukua salama kwa Feliki liwali. MDO 23:22‭-‬24 SUV.

Huyu Mjomba wake na Paulo alimwokoa ndugu yake, unaona kwenye andiko hilo takatifu nililokupa linapanga kumhamisha mtume Paulo kwenye mji ule aliokuwepo kwa ulinzi mkali.

Hapa Yesu Kristo hakumtokea Paulo amweleze mpango mbaya juu yake, Yesu Kristo alimtumia mjomba wake Paulo kumpa taarifa, na Paulo akampa maelekezo mengine mjomba wake aende kwa jemadari kumweleza habari hizo alizozisikia.

Unaona ni jinsi gani huyu ndugu alivyokuwa mwaminifu hadi akamfanya jemadari amtafutie ulinzi mkali wa kumtoa kwenye mji ule na kumpeleka mahali pengine.

Uwe mtu usiyepuuza mambo ya msingi kama haya, bora kuonekana mbaya kwa watu lakini ukawa umeokoa uhai wa mtu mwingine. Haijalishi hao wanaopanga mabaya ni ndugu zako, kama unaona wapo kinyume na Neno la Mungu usisite kufikisha taarifa mahali husika.

Kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, tuma ujumbe wako wasap kwa namba +255759808081 utaunganishwa kwenye kundi letu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com