Unaweza ukachukulia maombi ni jambo la kawaida sana, ukaona watu wanaopenda kuomba sana ni watu wenye shida sana kwenye maisha yao.

Ukachukulia maombi kama vile unavyoweza kuyachukulia, vile unayachukulia maombi, vile una mtazamo juu ya maombi. Unajikuta huna muda wa kuomba, na ukajikuta huna msukumo wowote wa kufunga na kuomba.

Watu wanaposema tufunge na tumwendee BWANA kwa sala na toba, unaona kama unajitesa sana. Kwa sababu ndani yako huna msukumo wa maombi, ama kwa sababu hujajua umhimu wa kuomba Mungu.

Maombi yana msingi mkubwa sana wa kutengeneza hali ya kiroho iliyoharibiwa na maovu ya wanadamu kukawa sawa. Maombi yanarejesha uhusiano mzuri na Mungu wako.

Unaweza ukaona kufunga alafu ukawa kwenye maombi mazito ya kukesha hadi usiku wa manane ukiomba. Ukaona ni jambo ambalo huliwezi, sio kwa sababu una shida ya kiafya, ni kwa sababu huna msukumo ndani ya moyo wako.

Mbaya sana kama huna tatizo lolote la kiafya alafu ukawa huna muda wa kuacha kula kwa masaa kadhaa kwa ajili ya kumwomba Mungu.

Vizuri na inafaa sana kuwa na siku ulizotenga kwa ajili kusema na Mungu wako ukiwa umeacha chakula cha mwili au tumbo.

Sio kana kwamba maombi ya kawaida hayawezi kuwa na maana mbele za Mungu, sio kana kwamba maombi ya kawaida hayawezi kujibiwa ama kusikilizwa na Mungu wako.

Maombi ya kufunga yana uzito mkubwa mbele za Mungu, unapoingia kwenye maombi, alafu Neno la Mungu likawa limejaa moyoni mwako. Maombi hayo lazima yawe na majibu mazuri mbele za Mungu.

Kuomba ukiwa na Neno la Mungu lililojaa moyoni mwako, utaomba ukiwa na uhakika zaidi, yaani imani yako inakuwa kubwa kutofautisha na yule asiye na Neno la Mungu moyoni mwake.

Haijalishi hali yako ya kiroho imechafuka kiasi gani, toba ya kweli iliyoambatana na maombi ya kufunga. Lazima Mungu aonekane kwako/kwenu, hata kama hasira ya Mungu iliwaka juu yako/yenu, Lazima Mungu atakusamehe/atawasamehe.

Rejea: Jikazeni mkaomboleze, enyi makuhani; Pigeni yowe, enyi wahudumu wa madhabahu; Njoni mlale usiku kucha katika magunia, Enyi wahudumu wa Mungu wangu; Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimezuiwa katika nyumba ya Mungu wenu. Takaseni saumu, iteni kusanyiko la dini, Wazee na wakusanye wenyeji wote wa nchi; Waende nyumbani kwa BWANA, Mungu wenu, Na kumlilia BWANA, YOE. 1:13‭-‬14 SUV.

Kumlilia Mungu ni jambo la msingi sana, acha watu wakuone wa kulialia wewe unajua unafanya nini mbele za Mungu. Maana maandiko matakatifu yanatuelekeza hivyo, yaani tuende mbele zake kwa machozi.

Umeona mzigo ulionao umekuwa mzito, omba msaada kwa waombaji wenzako wakusaidie kubeba hitaji lako. Usiogope kuwahimiza wachukue maombi ya kufunga kwa ajili ya hitaji lako au la nchi yako.

Usielemewe na mzigo mkubwa peke yako, washirikishe ndugu zako wa kiroho, kama wewe ni mwaminifu mbele za Mungu na wanakuelewa vizuri. Hawatasita kufanya hivyo.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest.
chapeo@chapeotz.com
www.chapeotz.com