Ashukuriwe Yesu Kristo aliye hai kwa kutuletea neema hii ya wokovu bure, vinginevyo ingekuwa ni shida kubwa mno. Mara ngapi tumeingia kanisani na machafu yetu bila kuyatubia, na tunatoka nayo vilevile bila hofu yeyote.

Pamoja na kuingia na kutoka bila kutubu, bado Yesu anaendelea kutuvumilia, huenda siku moja tukabadilika. Lakini bado tunashindwa kuelewa hii neema tumeipewa bure kwa gharama kubwa ili tuimie vizuri kumwendea Mungu atusamehe.

Kuna vitu vingi sana tunavipuuza siku hizi, hofu ya Mungu haimo tena ndani yetu, ikiwa mtu amezini na mume/mke wa mtu. Anaweza kusimama madhabahuni na kutoa huduma huku anaendelea kufanya uchafu wake, unafikiri mtu yule ana hofu tena ya Mungu ndani yake.

Ikiwa msichana anaweza kuwa na kibarua cha kuchoropoa mimba, alafu anapata ujasiri wa kusimama mbele ya madhabahu na kuhudumia watu bila shaka yeyote. Unafikiri usalama wa kanisa upo wapi, unafikiri mtu yule analeta hasira ya Mungu kiasi gani anapomwona anafanya vitu vya ovyo bila kutubu na kuacha.

Lakini wakati wa agano la kale ilikuwa hairuhusiwi mtu yeyote kuingia hekaluni ukiwa u mchafu. Maana yake ilikuwa lazima ujitakase kwanza ndipo uingie hekaluni mwa Bwana. Je sisi tunafanya hivyo, au kwa sababu yale mapigo ya papo kwa papo hatuyaoni, nasi tunaona tupo huru kufanya chochote kile bila mtu yeyote kutugundua.

REJEA; Akawasimamisha walinzi malangoni pa nyumba ya BWANA, asiingie aliye mchafu kwa vyo vyote. 2 NYA. 23:19 SUV.

Umeenda mbele za Mungu mara ngapi kumwomba akusaidie hitaji fulani, lakini wewe hutaki kutubu na kuacha dhambi unazofanya. Mara ngapi umeona Mungu hakujibu na umekuwa mtu wa kulalamika, lakini hutaki kuacha uovu wako.

Lazima tujenge utaratibu mzuri wa kwenda mbele za MUNGU kwa toba na kujitakasa kwa damu Yesu Kristo. Tusijenge mazoea ya kumwendea Mungu, tupo kipindi cha neema tunapaswa kujiangalia vizuri, tusije tukajifariji hakuna tatizo tukaendelea kutenda mabaya.

Tujue tunayofanya mabaya, hatupaswi kuyafanya kwa sababu Neno la Mungu linatukataza kutenda yaliyo kinyume. Usijifiche kwenye WOKOVU alafu u mtenda mabaya usiye na chembe ya hofu mbele za Mungu.

Mungu atusaidie kuelewa Neno lake zaidi na zaidi, ili tuzidi kuimarika kiroho katika safari yetu ya wokovu.
Tuzidi kujifunza kwa pamoja,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.