“Akamwapia, Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu. Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mfalme akafanya huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia”, Mk 6:23‭-‬26 SUV.

Nafasi kama hii Ester aliipata kwa mfalme Ahasuero wakati Wahayudi wametangaziwa kuuwawa wote, Malikia Ester alipopewa nafasi ya kuomba chochote hakupoteza nafasi hiyo.

“Mfalme akamwambia Esta tena siku ya pili pale pale penye karamu ya divai, Malkia Esta, dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utafanyiziwa. Ndipo malkia Esta alipojibu, akasema, Mfalme, ikiwa nimepata kibali machoni pako, na mfalme akiona vema, nipewe maisha yangu kuwa dua yangu, na watu wangu kuwa haja yangu” Est 7:2‭-‬3 SUV.

Kupitia Ester tunaona Taifa lake lilipona, wakapata nafasi ya kuishi tena, yale mabaya yaliyokusudiwa kwao yakawa yamekoma.

Tofauti na binti Herodia baada ya kucheza vizuri kwenye sherehe ya kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwa Herode.

Herode alimpa nafasi ya kuomba chochote, binti huyu aliona akamuulize mama yake kitu gani amwombe baba yake kutokana na nafasi aliyopewa.

Haikuwa nafasi ndogo, Herode alifurahi kiasi kwamba alikuwa tayari kutoa nusu ya ufalme wake, kwa lugha nyingine alikuwa tayari kutoa nusu ya utajiri wake.

Kwa kuwa binti alikuwa anamsikiliza mama yake, na mama naye alikuwa na chuki zake kwa Yohana mbatizaji. Mama yake alimwambia akaombe kichwa cha Yohana mbatizaji.

Ombi hilo lilimsikitisha Herode sana, lakini hakuwa na namna maana alishamwapia na kumwambia aombe chochote atapewa na umati wa watu walisikia alichosema.

Yohana aliuwawa na kichwa chake kikawa kimekatwa, na huo ukawa mwisho wa maisha yake.

Zipo nafasi huwa tunazipata katika maisha yetu, nafasi ambazo huwa tunapewa uhuru wa kuomba chochote tufanyiwe.

Baadhi yetu huwa tunaomba vitu ambavyo havina faida kwetu, vitu ambavyo vinakidhi haja ya mioyo yetu kwa muda mfupi.

Wapo watu waliotumia fursa zao vizuri, mmoja wapo tumemwona malkia Ester, wapo wengine walitumia nafasi hii vizuri walipoulizwa “wataka nikufanyie nini?”.

“Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona”, Mk 10:51 SUV.

Mungu anaweza kukupa nafasi ya kuomba lolote kwake kama alivyofanya kwa Mfalme Suleiman, akakuambia wataka nikupe nini au wataka nikufanyie nini?

Unaweza kufanya kama binti Herodia alivyoomba kichwa cha Yohana, badala ya kuomba jambo la maana unaomba wale wasiokupenda wafe au wapate shida.

Hujui kuwa ukiwa Duniani huwezi kukosa maadui, ungeomba jambo la msingi lingekusaidia katika maisha yako yote na ukamtukuza Mungu wako kwa matendo yake makuu aliyokufanyia.

Huna kazi, huna pesa, biashara zako zinahitaji mtaji, una mahitaji ambayo unahitaji fedha, alafu unapewa nafasi ya kuomba chochote unaomba usiyempenda afe.

Unaweza kuona jinsi gani mtu anaweza kupoteza jambo la muhimu kwa kuomba kitu kisichomsaidia katika maisha yake.

Jifunze kutumia fursa vizuri, unaweza kukutana na nafasi hii aliyokutana nayo binti huyu, alafu ukaomba kichwa cha mtu.

Wapo watu tunaojifunza kwao waliopewa nafasi ya kuomba chochote na wakaomba mambo ya maana na ya msingi yaliyowasaidia katika maisha yao.

Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081