Tujifunze muda mwingine kabla ya kulalamika, tuwe tunajiuliza maswali kwanza kama hili, je! Uhusiano wetu na Mungu upo vizuri au haupo vizuri? Hii itatusaidia sana kupunguza malalamiko mbele za Mungu, kusema Mungu ametuacha, na kusema Mungu hatuoni.

Mtu analalamika Mungu hamwoni katika shida yake, huku yeye anamkosea kwa matendo yake maovu. Huyo anayemlalamikia Mungu hamwoni, ndiye anayemkosea kwa matendo yake maovu.

Unakutana na dada analalamika ameomba sana Mungu ampe mume mwema kutoka kwake, badala yake ameishia kukutana na wanaume walaghai. Ambao huishia kumwacha, yaani wanamwambia watamwoa ila mwisho wa siku huishia kumwacha.

Bora wangekuwa wanamwacha akiwa salama, anasubiri azini nao kwanza, wakishamkimbia ndio anaanza kulalamikia Mungu hamwoni kiu yake ya kutaka mume.

Unamkuta kaka analalamika hapati kabisa mwanamke mwaminifu wa kuweza kumwoa, anafika mbali zaidi anaanza kumlalamikia Mungu hamsikii maombi yake. Wakati yeye mwenyewe sio mwaminifu mbele za Mungu ila anataka mwanamke mwaminifu, yaani ni mchafu, anataka mwanamke msafi.

Hawezi kufikiri kwamba anapaswa kutengeneza uhusiano wake kwanza na Mungu wake, anaishia kulalamika mbele za Mungu. Anaishia kulawalaumu akina dada anaokutana nao, na kuwaona sio watu wazuri, ndio wale utawakuta wanasema wakuamini ni mama yako mzazi tu.

Unakuta mtu analalamika Mungu hamjibu maombi yake, wakati mtu huyo anaabudu sanamu. Mtu huyu anayeabudu SANAMU anategemea Mungu aliye hai amsaidie, Mungu mwenye wivu, asiyependa kuchanganywa na miungu mingine. Leo hii anamlalamikia hamjibu maombi yake, amesahau mungu anayemwabudu hachangamani na Mungu wa kweli.

Rejea: Kisha akaniambia, Mwanadamu, umeyaona wanayotenda wazee wa nyumba ya Israeli gizani, kila mtu ndani ya vyumba vyake vya sanamu? Maana husema, BWANA hatuoni; BWANA ameiacha nchi hii. EZE. 8:12 SUV.

Mtu anakwambia anaona mambo yake yanazidi kuharibika, huku anaabudu JUA, hivi kweli anategemea Mungu ahusike vipi kwenye maisha yake ya kiroho wakati amemzuia mwenyewe?

Rejea: Akanileta mpaka ua wa ndani wa nyumba ya BWANA, na tazama, mlangoni pa hekalu la BWANA, kati ya ukumbi na madhabahu, walikuwako watu kama ishirini na watano, wamelipa kisogo hekalu la BWANA, na nyuso zao zimeelekea upande wa mashariki, nao wanaliabudu jua, kwa kuuelekea upande wa mashariki. EZE. 8:16 SUV.

Hebu tufike mahali tuseme hapana, kama kuomba tumeomba sana, kama ni kutoa sadaka tumetoa sana, na kama kuhudhuria ibada tumehudhuria sana. Shida inakuwa ipo wapi? Mbona kama Mungu yupo mbali nasi, lazima kutakuwa kuna mahali hatuendi sawa.

Kujikagua maisha yako ni jambo la msingi sana, lazima ufike mahali uangalie kipi kinakutenga na Mungu wako. Kipi kinakufanya Mungu asijibu maombi yako, unaweza kuhangaika sana kumbe tatizo ni wewe mwenyewe.

Kama unaabudu sanamu, Mungu atawezaje kuonekana kwenye hayo masanamu? Utalalamika usiku na mchana. Lakini ukweli Mungu hawezi kuonekana kukusaidia katika maisha yako wakati umemsimamisha mungu mwingine.

Mungu anataka ajitukuze yeye, na sio miungu mingine, na sio hivyo vinyago vya kuchonga, na sio hizo sanamu za kubandika ukutani. Alafu unategemea Mungu ahusike kukujibu hitaji la moyo wako.

Utasema ndugu unatusema sisi, utasema ndugu unawasema watu fulani, sitaki niwe msemaji sana, napenda Neno la Mungu liseme zaidi lenyewe.

Rejea: Akaniambia, Ingia uyaone machukizo mabaya wanayoyafanya hapa. Basi, nikaingia, nikaona; na tazama, kila namna ya wadudu, na wanyama wachukizao, na taswira za vinyago vyote vya nyumba ya Israeli, zimepigwa ukutani pande zote. EZE. 8:9‭-‬10 SUV.

Achana na kuabudu wadudu, achana na kuabudu wanyama, achana na kuabudu twasira za vinyago vya kuchonga, na achana na kuabudu sanamu za kubandikwa kwenye kuta za majumbani/mahekaluni.

Mungu akufungue ufahamu wako.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081