“Akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni”, Mt 18:3 SUV.

“Akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni”, Mt 18:3 SUV.

Badiliko analolitarajia Yesu kwako wewe unayemwamini au unapoongoka au kuokoka, huanzia kwa hatua ndogo sana kama za mtoto mdogo anayemtegemea mama yake kwa kila kitu.

Tunapoongoka tunapaswa kuwa wanyenyekevu kwake, tunaomtegemea yeye kwa kila kitu, wanyonge kwake na wenye utayari wa kufinyangwa na Baba yetu aliye mbinguni.

Tukishakuwa watoto wake tunaomtegemea yeye kwa kila kitu, kinachotarajiwa na Yesu kwetu ni haya mambo mawili muhimu; la kwanza ni kuachana kabisa na mambo yote yasiyo ya Kimungu, tunaposema mambo yote ujue ni yote yasiyompendeza, hatupaswi kuwa nusu nusu.

Na jambo lingine la pili ni kumgeukia Mungu na kutenda matendo ya haki, yaani kuzaa matunda yapasayo toba, “Basi zaeni matunda yapasayo toba”, Mt 3:8 SUV.

Unapaswa kuelewa kuwa kuongoka hakumaanishi tendo moja kusikitikia au kutubu, inapaswa kuwa ni tabia katika maisha yetu yote kwa ujumla tunapokuwa hapa duniani.

Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti”, 2 Kor 7:10 SUV.

Kwanini hili linapaswa kuwa mwendelezo katika maisha yetu? Kwa sababu kwa asili yetu tunafuata muundo wa maisha unaotuondoa katika njia ya Mungu na kutuelekeza kwenye mauti ya milele.

Ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine”, Efe 2:2‭-‬3 SUV.

Kuongoka ni mwitikio wa mwanadamu kwa wokovu ambao ni karama ya Mungu, ukitekelezwa kwa namna ya pekee ya neema na nguvu za Roho Mtakatifu ambayo hupokelewa kwa imani.

Waliposikia maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, Basi, Mungu amewajalia hata mataifa nao toba liletalo uzima”, Mdo 11:18 SUV.

Tunapojenga uhusiano wetu mpya na Mungu wetu, kuongoka kunahusu mabadiliko katika maeneo yafuatayo; mahusiano yetu na Mungu na watu, tabia zetu njema, kujitoa kwetu, na mambo ya kumtukuza Mungu na mtazamo wetu kwa ujumla wa maisha yetu.

Kuongoka au kuokoka ni sehemu ya imani halisi iokoayo na hitaji la msingi la wokovu na utakaso wa mwanadamu.

Uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi“, Mdo 26:18 SUV.

Ukiyashika haya na kuyaweka moyoni mwako, maisha yako ya wokovu yatakuwa salama na yenye kumtukuza Mungu siku zote za maisha yako hapa duniani.

Kuongoka kwetu kunapaswa kuwa kwa faida na kuwavuta wengine kwa Yesu Kristo, vile watu wanavyoona tunaishi, wanapaswa kuvutwa na matendo yetu mema waje kwa Yesu.

Nakualika kwenye programu nzuri ya kusoma neno la Mungu kila siku na kutafakari, ambayo itakufanya ukue kiroho, programu hii ipo wasap, tuna kundi nzuri la kusoma biblia. Wasiliana nasi kwa wasap +255759808081, utaunganishwa na wewe uwe miongoni mwa wanaosoma biblia.

Soma neno ukue kiroho

Mungu akubariki sana

Samson Ernest