“Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo”, Gal 5:13 SUV.

Mtume Paulo aliwakumbusha Wagalatia jambo la muhimu sana kuhusu uhuru walioupata kwa kumwamini Yesu Kristo.

Uhuru huu haukuwa wa kufanya kila kitu, uhuru uliozungumzwa hapa ulikuwa wa kutoka katika utumwa wa dhambi na wa sheria.

Uhuru huu ulikuwa haumpi mtu ruhusa ya kufanya kila baya ambalo lingejitokeza mbele yake, ulikuwa ni uhuru usiopelekea kumkosea Kristo.

Tunaweza kufikiri kwa kuwa tumewekwa huru tunaweza kufanya kila kitu bila kuzuiliwa na mtu yeyote, huo sio uhuru uliozungumzwa hapa.

Nchi yetu kuwa huru sio tiketi ya watu kufanya kila kitu wanachojisikia kufanya, kuna mipaka ya kufanya vitu ndio maana kuna Polisi na mahakama.

Tunapaswa kuheshimiana, mkubwa anapaswa kuheshimu mdogo na mdogo anapaswa kuheshimu mkubwa.

Viongozi wa ngazi zote wanapaswa kuheshimiwa kwa nafasi zao, hatupaswi kufanya chochote kibaya juu yao kwa sababu tupo huru, huo sio uhuru mzuri.

Tutumie uhuru wetu vizuri, hatupo huru kufanya dhambi na kuishi tunavyopenda sisi, na kuona watu wengine hawapaswi kuingilia maisha yetu.

Tukiishi kwa namna hiyo au tukawa na uhuru wa namna hiyo hatutaweza kumpendeza Mungu wetu, utakuwa ni uhuru unaotufakaranisha na Mungu wetu.

Tunapaswa kumsikiliza Roho Mtakatifu vile anatuongoza katika uhuru mzuri, ili tusiwe na uhuru ambao unamkosea Mungu wetu.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081