Mungu amenifundisha jambo hili kwa namna ya pekee sana, na nimeguswa sana na ushuhuda huu nikaona nikushirikishe na wewe rafiki yangu.

Mzee mmoja akasimama mbele yetu na kuanza kushuhudia mapito ya utumishi wake, akaanza kwa kusema sikupenda kuanza kumtumikia Mungu katika umri huu mkubwa namna hii wa miaka 60. Bali nilitaka kuanza kutumika nikiwa kijana mdogo.

Nilibatizwa mwaka 1980, baada ya kubatizwa nilisikia wito ndani yangu na kuanza kuhubiri habari za Yesu nyumba kwa nyumba(mtaa kwa mtaa)

Watu wengi waliokoka katika huduma ya uinjilisti niliokuwa nafanya katika kipindi hicho chote. Hadi ikafikia kiongozi wangu akabarikiwa na huduma niliyokuwa naifanya na kuniahidi kunifungulia kanisa maeneo niliyokuwa naishi.

Kweli baada ya muda fulani kupita kanisa lilikuja kujengwa maeneo yale ambayo mchungaji aliniambia, lakini haikuwa kama vile niliambiwa. Aliletwa mtumishi mwingine wa kulisimamia hilo kanisa, hii ilichangiwa na mimi kutokuoa kipindi hicho, nikawa mwimbaji wa kwaya huku nikiendelea na huduma yangu ya kuhubiri injili mtaa kwa mtaa.

Katika safari yangu hiyo nilipatwa na shida ya kuugua kichaa, baada ya hapo sikujua kilichokuwa kinaendelea tena katika maisha yangu.

Shida hiyo niliyoipata ilinifanya kumnyang’anya mtu baiskeli yake kwa kumtishia panga(kwa mjibu wa maelezo ya watu) na kuanza kukimbia nayo, hilo kosa lilisababisha nikafungwa jela miaka 30. Maana kipindi hicho makosa kama hayo watu walikuwa wanafungwa hiyo miaka.

Nilikaa jela miaka mitatu nikiwa naugua kichaa, mwaka wa tatu nilizinduka na kujikuta nikiwa nimefungwa pingu miguuni. Mwenzagu aliyekuwa karibu alishtuka na kuniita wewe mwehu unataka kunipiga baada ya kuanza kumsogelea?

Nilimuuliza mwehu ni nani hapa? Naye aliponiona naongea vizuri alishtuka na kuniuliza “umepona?” Nikamuuliza na yeye kwanini nimefungwa hivi?

Askari magereza alifika, nikamuuliza huyo Askari nataka kujua kwanini nipo hapa? Nataka kujua kosa la mimi kuwepo hapa ni lipi?

Askari yule alimpeleka sehemu ambapo kulikuwa na faili lake, hilo faili baada ya kutafutwa na kupatikana alisomewa kosa lililomfanya afungwe jela.

Huo ndio ulikuwa mwisho wake wa kuugua kichaa, baadaye sasa serikali ilitangaza msamaha wa wafungwa. Yeye hakuachiwa huru ila akawa amepunguziwa miaka, badala ya miaka 30 ikawa miaka 10.

Baada ya kumaliza hiyo miaka 10 alirudi nyumbani na kuendelea na huduma yake, na hadi sasa ni mzima kabisa na huwezi kujua kama amewahi kupata hiyo shida. Jambo la kumshukuru Mungu zaidi ni kuwa ameendelea na utumishi wake, huu ni mwaka wa sita sasa tangu arudi tena kwenye huduma yake na ana kanisa.

Mzee huyu amenifikirisha sana, amenifanya nianze kukumbuka baadhi ya kauli za watu wanazozitoa, moja ya kauli hizo ni “ulikuwa wapi wakati wa ujana wako hadi unakuja kupata wito wakati wa uzee?”

Kupitia ushuhuda huu niliosikia kwa masikio yangu kutoka kwa mhusika mwenyewe, umenifanya ninyenyekee sana mbele za Mungu na kuchunga sana ulimi wangu. Kwanini, kwa sababu huwa tunajipa kazi ya kuwaambia maneno mabaya ya kuwaumiza wazee wetu.

Tunapaswa kufahamu Mungu mwenyewe ndiye aliyewaita, tuwaache watumike hadi aliyewaita awaambie imetosha na wao wenyewe wataona imetosha. Maana aliyewaita anajua ni wakati gani wao kupumzika, na uzuri hawatuzuii sisi kutumika.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
+255759808081