“Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi”, Lk 19:17 SUV.

Mtu yeyote ambaye amekuwa mwaminifu katika kumtumikia Mungu na kulitumikia lile kusudi lake kwa uaminifu, mtu huyo atapata thawabu kubwa katika dunia ya sasa na ufalme ujao.

Watu hawa waaminifu na wenye bidii watapewa majukumu makubwa zaidi katika mbingu mpya na nchi mpya.

“Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena”, Ufu 21:1 SUV.

Wale ambao uaminifu wao ulikuwa mdogo mbele za Mungu watapokea nafasi ndogo na wajibu mdogo kutokana na uwajibikaji wao mdogo.

Tusijidanganye kuwa tutakuwa sawa na wale watu waaminifu mbele za Mungu, watu wanaotoa muda wao mwingi mbele za Bwana, watu linapofika suala la kujituma wanajituma haswa, tukaona tutakuwa sawa! Tusahau hilo.

Hakuna usawa hata kama wote tutaingia peponi au maisha ya umilele, kila mmoja atapewa taji yake sawasawa na utendaji wake akiwa duniani.

Tunaona hata katika maisha yetu ya kila siku, wale walio waaminifu katika kazi zao, huvuna matunda ya uaminifu wao na bidii yao.

Kanuni ya Kimungu ndivyo ilivyo, kila mmoja atalipwa sawasawa na matendo yake, ukiwa unafanya kazi kwa bidii kubwa utavuna matunda ya bidii yako, na ukiwa unafanya kazi kwa uvivu utavuna matunda ya uvivu wako.

Tuweke bidii kwa yale Mungu ametupa wito ndani yetu tuyafanye, kila mmoja anao wito maalumu amepewa na Mungu, wito huo unaweza usilingane na wa mtu mwingine kabisa.

Ukifanya kwa uaminifu na kwa bidii kubwa utalipwa na Bwana, ukiwa duniani na utapofika mbinguni, utapongezwa kwa kazi yako njema.

Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081