Kuna watu huwa hawaaminiki kabisa, wakikabidhiwa vitu au wakiachiwa vitu lazima wafuatiliwe kwa ukaribu sana.
Wanafuatiliwa kwa sababu wanajulikana kwa kudokoa/kuiba. Ukimpa kitu kinaweza kisirudi, na kikirudi kinarudi kikiwa pungufu.
Watu kama hawa huwa wanajiharibia sifa zao, wanawafanya watu wengine wasiwe na imani nao kabisa.
Ndio maana mtu anaweza akawa anafuatiliwa sana, wakati mwingine mpaka yeye anaanza kulaumu na kusema “mbona hamna imani na mimi?”
Bila kujua aliyesababisha watu wasiwe na imani naye ni yeye mwenyewe.
Wapo watu pia wanajulikana kwa sifa ya uaminifu, hata wakipezwa mzigo kupeleka mahali wataufikisha kama walivyoupewa.
Watu hawa wana utofauti mkubwa sana na wale wasioaminika, wanaoaminika huwa hawafuatiliwi sana.
Tena mtu anayeaminika huwa akimpa mtu kitu, wale wanaopewa huwa hawahangaiki sana kukihakiki hicho kitu.
Wanajua moja kwa moja kipo sawa, na kweli wakiangalia utakuta kipo sawa. Labda itokee alikosea kidogo, na akiambiwa anakuwa na uelewa.
Changamoto iliopo hapa kwenye kuaminiwa na watu, huwa haitokei siku moja ukaaminiwa na Watu. Huwa kuna mchakato mrefu sana hadi mtu kufikia kiwango cha kuaminiwa na ndugu, jamaa, na marafiki.
Tunalithibitisha hili kupitia maandiko matakatifu, tunaona wale watu waaminifu hapakuwa na haja ya kutakiwa kutoa hesabu yao ya matumizi.
Rejea: Wafanyakazi waliosimamia kazi hii walikuwa waaminifu kabisa, kwa hiyo hapakuwa na haja ya kuwataka watoe hesabu ya matumizi ya fedha hizo. 2 Wafalme 12:15 BHN.
Unapaswa kujipima kupitia hili somo, ukiona watu wanakutaka sana utoe mchanganuo wa matumizi kwa pesa waliyokupa.
Ukiwapa mchanganuo wako wa matumizi bado hawaonyeshi kuamini kile umewapa maelezo, ujue huaminiki.
Kama huaminiki ujue kuna mahali haupo vizuri, hapa nazungumzia kwa mtu ambaye anakufahamu alafu anakuwa haonyeshi kukuamini.
Sisi kama wakristo tunapaswa kuaminiwa na watu, hawatatuamini tu kwa sababu tunasema tumeokoka. Watatuamini kwa kuonyesha uaminifu wetu kwa mambo mbalimbali.
Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
+255759808081