“Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu”, Mk 1:8 SUV.

Yohana Mbatizaji alikuwa mtu wa kwanza kuhubiri habari njema kumhusu Yesu Kristo. Marko ambaye ni mwandishi wa kitabu cha Marko, anafanya ufupisho au muhutasari wa mahubiri yake na kuyaweka katika wazo moja.

Kutangazwa sana kwa Yesu Kristo na Yohana Mbatizaji, ambaye angekuja na kuwabatiza watu wake kwa Roho Mtakatifu, kulitimia siku moja.

Hii inatufunza kuwa wote wanaompekea Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yao, wanapaswa kutonyamaza bali wamtangaze Yesu kwamba ndiye anayewabatiza watu kwa Roho Mtakatifu.

“Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi”, Mdo 1:8 SUV.

Ubatizo wa Roho Mtakatifu kwa mwamini au kwa mfuasi wa Kristo ni muhimu sana, mtu anapojazwa na Roho wa Mungu anajawa na ujasiri usio wa kawaida.

Ujasiri huu utamsaidia mambo mengi, mojawapo ni kuweza kushinda dhambi, na lingine ni kuweza kuhubiri injili ya kweli kwa ujasiri mkubwa.

“Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri”, Mdo 4:31 SUV.

Unaweza kuona ni jinsi gani Roho Mtakatifu alivyo wa muhimu katika maisha yetu ya kila siku, tunapookoka tu tunamkaribisha Roho Mtakatifu ndani yetu.

Hatua inayofuata tunapaswa kujazwa, na ishara mojawapo ya kuonyesha kuwa umejazwa na nguvu za Roho Mtakatifu ni kunena kwa lugha mpya.

“Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka”, Mdo 2:3‭-‬4 SUV.

Ukiwa mfuasi wa Yesu unapaswa kufurika nguvu za Roho Mtakatifu kama glasi iliyojaa maji hadi yakamwagika chini, hii itakusaidia sana katika maisha yako ya wokovu.

Tamani kujazwa na nguvu za Roho Mtakatifu, kuna mahali utakuwa unapita kwa wepesi sana, hasa nyakati za changamoto ngumu katika maisha yako.

Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081