Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Mungu ametupa kibali cha kuiona.

Zipo sababu nyingi tunaweza kuzitengeneza ili kujitetea, kujitetea kule kunaweza kulenga kutukinga ili tuendelee kuwa mbali na Mungu.

Sawa na mtu anasema hana muda na familia yake ndio maana mambo mengine yameharibika, elewa Mungu hajui hilo, ndio maana ni Mungu wa utaratibu. Tunamwona mtumishi Eli alikuwa mtu mwema wa Mungu ila hakuwa karibu na watoto wake, wala hakuwapa maonyo. Mungu hakuwatazama tu watoto wale kwa hukumu bali alimtazama na baba yao.

Kweli tunafika wakati hatuna namna ya kuweza kupaza sauti zetu kwa ajili ya kuzungumza na Mungu, ila bado tuna uwezo wa kupiga magoti tukaomba kwa sauti ya chini. Tukazama zaidi katika sauti ile ya ukimya na Mungu akatusikia, kuliko kujipa sababu ya kuacha kabisa kwenda mbele za Mungu.

Yapo maeneo mengine ambayo yanaweza pia kutufanya tukashindwa kumwabudu MUNGU wetu kwa uhuru, pamoja na hayo bado hatuwezi kuacha kutafuta mahusiano yetu na Mungu.

Unaweza kusema vyovyote vile kujifariji ila nakwambia kuna watu wamejikuta wapo maeneo ambayo hawezi kutamka NENO YESU. Ila hawakukubali mazingira yale yawe kizuizi kwao kuliita jina la Yesu.

Kukusanyika kwetu pamoja kwa ajili ya kumwabudu Mungu ni ishara njema kwetu sisi kuwa na ushirika wa pamoja.

Mtu anayelijua hili NENO la MUNGU linalosema hivi;

Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Yak 4 : 8.

Mtu huyu hawezi kukaa mbali na Mungu wake, maana anajua kukaribia kwake mbele za MUNGU kuna faida nyingi zaidi ya miujiza mbalimbali inayokimbiliwa na wengi.

Kadri unavyozidi kujenga uhusiano wako na Mungu; ndivyo unavyozidi kuwa na moyo wa unyenyekevu mbele za Mungu, ndivyo unavyozidi kuwa na moyo wa toba, ndivyo unavyozidi kujua njia uliopo sasa ni sawa au umekuwa na njia mbili tofauti.

Ukiona mtu anakwambia hawezi kuomba Mungu kwa sababu yupo na watu wasiomjua Mungu, jua mtu yule hana mahusiano mazuri na Mungu.

Ukiona mtu anakwambia hawezi kusoma biblia kwa sababu yupo bize sana, elewa mtu yule ametawaliwa sana na mambo ya mwili. Ila kiroho chake kina utapiamlo kwa ukosefu wa lishe bora ya NENO la Mungu.

Uhusiano wetu mzuri na Mungu wa kupenda kujifunza, na kuketi hemani mwake kwa ajili ya mafundisho yake unatukumbushe wajibu wetu.

Rejea; Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane. Isaya 1 :16_17.

Nyakati nyingine tunaenenda tukijua tupo sawa kumbe tumepotea na tumekuwa kikwazo kwa wengine. Lakini tunapokuwa karibu na Mungu, ni rahisi kusema nasi tukasikia na kuziacha njia zetu mbaya.

Tuneweza kujaa kiburi cha uzima, tuneweza kujaa kiburi cha sifa, tunaweza kujaa kiburi cha wingi wa mali na fedha tulizonazo. Lakini tukiwa karibu na Mungu, kupitia NENO lake hutuonya na kutuelekeza yatupasayo kutenda kupitia mali zetu.

Ikiwa unazo mali, anakuambia uwe baraka kwa wajane na yatima, ukiwa una nafasi serikalini na wapo wanyonge wasio na kitu wanahitaji msaada wako, wapaswa kuwasaidia.

Bado tunaona mazingira yetu ya kazi hayawezi kutuzuia uhusiano wetu na Mungu, bado kila mmoja wetu anaweza kuhubiri habari za MUNGU aliye hai akiwa kwenye shughuli zake.

Watu wamwone Mungu wako aliye hai, hata kama uwe mazingira magumu, ukishindwa kuzungumza kwa mdomo wako, basi matendo yako yazungumze.

Kazi na mazingira uliopo yasikutenganishe na Mungu, haijalishi maovu yamezidi sana, endelea kujitakasa na kuwaombea Rehema wale wote unaoona wanatenda yasiyo mema.

Mazingira yasikuondoe kwenye kusoma NENO la Mungu, uwe mtu wa kujifunza kila wakati neno. Pasipo neno kumtenda MUNGU dhambi ni rahisi sana.

Rejea; Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. Yoh 5 : 24.

Mungu akubariki sana, endelea kutafakari maneno haya.

Samson Ernest.

+255759808081.