Kuhubiri injili.

Elimu ni nzuri sana, wala sio ya kupuuza hata kidogo, elimu ya darasani ndio imetufanya tunaweza kusoma na kuandika, pasipo elimu ya darasani tusiwengeweza kusoma Neno la Mungu.

Leo mimi na tunaweza kuwasiliana kwa maandishi, kwa sababu tulifundishwa darasani tukajua kusoma na kuandika. Wengine hawajaishia kusoma tu na kuandika, wameenda mbali zaidi kwa kusoma kozi mbalimbali za kuwaongezea ujuzi wa kutengeneza vitu.

Leo tunaweza kuwasiliana kwa simu, kwa sababu ya mtu mmoja mwenye elimu/ujuzi alikaa chini akaunda kifaa cha simu na leo tunaweza kuwasiliana ndugu na jamaa.

Unaweza kuona jinsi gani elimu ilivyo na umhimu mkubwa, na hatupaswi kuipuuza hata kidogo, tunapaswa kuona ni jambo la msingi sana kwa kila mmoja kuwa nacho.

Japo kusoma sio kuelimika, ila kutokuelimika kwa mtu hakuwezi kuondoa umaana wa elimu. Elimu itabaki kuwa ya muhimu kwa maisha yetu hapa Duniani.

Tumeona umhimu wa elimu, zipo faida nyingi sana ila nimekupitisha chache uweze kuona ni jinsi gani elimu ni muhimu sana. Hili halina ubishi hata kidogo, hata kama unamjua mtu fulani amesoma sana ila mambo anayoyafanya hayaendani kabisa na elimu yake, hilo lisikufanye ukadharau elimu.

Ipo elimu ya darasani, na ipo elimu ya kujifunza mwenyewe kwenye vitabu mbalimbali, zote zina umhimu kutegemeana na uhitaji wako, na unataka nini kwa wakati huo.

Pamoja na kuona umhimu wa elimu, elimu hii ya darasani haiwezi kutupa ujasiri wa kiMungu, utajiamini kama msomi mwenye elimu kubwa ila unapofika eneo la kiroho huwezi kuwa na ujasiri kwa kuangalia kiwango chako cha elimu.

Unaweza ukawa msomi mwenye elimu kubwa, lakini ukanyimwa usingizi na mchawi, au ukatishiwa kupotezwa uhai wako na wachawi, ukaogopa kweli na kuwa mdogo kama mtu asiye na digrii za kutosha kichwani.

Asikudanganye mtu, ujasiri wa watumishi wa Mungu, hautokani na elimu kubwa ya theologia, wala hautokani na kiwango chao cha mali. Ujasiri wa mtumishi wa Mungu au kwa mtu yeyote yule aliyeokoka, unatokana na ujazo wa Roho Mtakatifu ndani yao.

Vile vile ukimwona mtu ana ujasiri mkubwa, alafu mtu yule hajaokoka ujue ipo nguvu nyingine ambayo inamfanya awe na ujasiri huo mkubwa. Usifikiri ujasiri alionao umetokana na kiwango chake cha elimu alichonacho, hapana, zipo nguvu za giza zinampa ujasiri huo.

Hili tunajifunza kwa watumishi wa Mungu, Petro na Yohana, hawa watu wawili hawakuwa na elimu ile kubwa waliyokuwa nayo watu wengine. Elimu yao ilikuwa imetokana na shule ya Roho Mtakatifu, hicho ndicho kiliwafanya wasimwogope mtu yeyote.

Rejea: Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu. MDO 4:13 SUV.

Ukimwamini Yesu Kristo na kumpokea Roho Mtakatifu, wewe sio mtu wa kawaida, nikiwa na maana kiwango chako hakilingani na asiye mwamini Yesu Kristo. Hakuna mtu atakuja kukutisha kwa namna yeyote ile akakufanya ukaacha kufanya huduma, wala hakuna mchawi yeyote anaweza kukutisha ukashindwa kulala.

Kama nilivyoanza kukuambia, ujasiri wetu hautokani na elimu kubwa tuliyonayo, wala elimu kubwa haileti ujasiri kwenye maisha ya wokovu/kiroho. Unaweza ukawa na elimu kubwa, lakini usiwe na ujasiri wowote ndani yako, unaweza kutishwa na paka tu ukaanza kuhangaika.

Ujasiri wa Petro na Yohana hukutokana na elimu au maarifa yeyote ya Dunia hii, ujasiri wao ulitokana na aliyewaita, na kuwachagua wamtumikie. Hata wewe uliyempokea Yesu Kristo, umeitwa na Yesu, maana wakati ukiwa ni mtu wa Dunia, ulivyosikia habari za Yesu Kristo ulichukua hatua ya kuokoka.

Ukiwa kama mkristo ambaye una safari ya kwenda mbinguni, na ukiwa hapa Duniani, hakikisha unajazwa nguvu za Roho Mtakatifu. Ukishajazwa utaweza kumhubiri Yesu Kristo kwa ujasiri mkubwa, hata kama kuna mahali utafika ukazuiwa kuhubiri/kufundisha habari za Yesu hutaweza kujizuia, wala hutaweza kunyamaza.

Rejea: Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. MDO 4:31 SUV.

Ujasiri wetu unatokana na ujazo wa Roho Mtakatifu, bila Roho Mtakatifu, hatuwezi kujawa na ujasiri ndani yetu, tutakutana na changamoto ngumu kwenye maisha yetu ya wokovu. Alafu tutajawa na hofu, na tunaweza kufikia hatua tukachukia na wokovu.

Kufahamu haya unapaswa kuwa msomaji wa Neno la Mungu, hakikisha unasoma Neno kila siku. Kama hili ni changamoto kwako, karibu sana kwenye kundi letu la kusoma Neno kila siku, tutafute wasap kwa namba hii +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com