“Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende”, Mdo 3:6 SUV.

Kama kuna jambo la kujivuna nalo waamini ni hili jina la Yesu, moja ya silaha kubwa tuliyonayo waamini ni hili jina la Yesu, hili linatosha kabisa kuondosha shida zote zinazotusumbua katika miili yetu.

Moja ya muujiza mkubwa uliofanyika kwa kutumia jina la Yesu ulikuwa ni kuponywa kwa kiweke aliyekuwa ombaomba, akaombewa na kupokea uponyaji wake.

Yesu aliwaeleza wazi wale wafuasi wake kuhusiana na wale watakaomwamini yeye, watu hao wataweza kuweka mikono yao juu ya wagonjwa nao watapokea uponyaji kupitia jina la Yesu.

“Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya”, Mk 16:17‭-‬18 SUV.

Tunaona hili katika kanisa la kwanza liliendeleza huduma ya Yesu ya uponyaji katika kuyatii mapenzi yake. Miujiza mingi ilitendeka kwa imani kupitia jina la Yesu Kristo, na karama za uponyaji zilitenda kazi kupitia kwa Petro ambapo tunaona mfano mmoja wapo wa kuponywa kwa kiwete.

Petro alimuweka wazi yule kiwete ombaomba kuwa yeye hana kitu cha kumpa kama alivyokuwa anataka ila alikuwa anacho kitu kikubwa na cha thamani zaidi kuliko fedha alizokuwa anazihitaji.

Mfano huu hai unatufundisha mengi sana kama kanisa la Kristo, tunaweza tusiwe na fedha za kuwapa wahitaji mbalimbali ila tunaweza kuwaombea na Yesu akawaponya na shida zao.

Tunahitaji kuwa na uhusiano mzuri na Yesu Kristo, maisha yetu yanapaswa kuwa na ushuhuda mwema kwake, uhusiano wetu na Mungu unapaswa kuwa wa karibu mno.

Tunapaswa kufanya nini ili kurudisha ile nguvu ya kuweza kutenda kazi? Tunapaswa kuwa na muda na Mungu wetu, tuwe watu wa maombi, tusome neno, tuwe na utulivu mzuri na Mungu, na tuache maisha ya dhambi.

Tukifanya hivyo tutaona jina la Yesu likifanya kazi kubwa katika maisha yetu kupita vile tuwazavyo kwa akili zetu za kibinadamu.

Liwe jua iwe mvua soma biblia
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081