“Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu”, Yn 14:16‭-‬17 SUV.

Yesu anamwita Roho Mtakatifu msaidizi wetu, ukiliangalia neno hili “Msaidizi” katika tafsiri ya lugha ya Kiyuyani ni “Parakletos”, likimaanisha kuwa “aliyeitwa kusaidia”.

Neno hili lina maana kubwa sana, ukilichukulia haraka haraka unaweza kuona ni la kawaida, ila unapaswa kuelewa huyu “aliyeitwa kusaidia” alikuwa na jukumu kubwa sana kwetu.

Jukumu hili alilopewa Roho Mtakatifu tunaliona katika vipengele hivi; Ni Msahauri wetu, Mtia nguvu wetu, Mfariji wetu, Wakili wetu, Mwombezi wetu, Mshirika na Rafiki yetu.

Huyu ndiye Msaidizi ninayemzungumzia hapa, anazo sifa zote, kupita sifa za wasaidizi wengine wote, unaweza kupewa walinzi wa kukulinda ila hawawezi kufikia viwango vikubwa kama hivi, yapo maeneo mengi watapelea.

Maajabu yanayoshangaza kwa msaidizi huyu na anachotufundisha sisi ni kwamba amekuja kuendeleza zile zile kazi za Yesu alizokuwa anazifanya akiwa duniani, tofauti kabisa na wasaidizi wengine wanaweza kwenda kinyume na wale waliowateua wawasaidie.

Roho Mtakatifu moja ya kazi yake kubwa anakuwa upande wa wale watu wanaompokea Kristo na kufanyika watoto wake, yeye anakuwa mwalimu wao akiwasaidia na kuwatia nguvu, na wao wakiwa wanafunzi wa Yesu.

“Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma”, Mt 14:31‭-‬32 SUV.

Anawafundisha njia ya kweli ya kufuata katika maisha yao ya wokovu, njia ambayo itawasaidia kuwafikisha mbinguni kwa Bwana wao, njia ambayo inahitaji mwalimu sahihi wa kuwaelekeza wasije wakapotea (Yn 14:26).

Jukumu kubwa lingine ambalo analifanya kwetu ni kutuombea ipasavyo kwa Mungu wetu, hili unaweza kujiuliza anatuombeaje, sisi tunaweza tusifikie viwango vinavyotakiwa au tunaweza tusijue kuomba yapasayo, yeye hutusaidia katika udhaifu wetu huo.

“Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu”, Rum 8:26‭-‬27 SUV.

Kuwa rafiki, moja ya changamoto mtu anayoweza kukutana nayo kwenye maisha yake ni kutengwa na marafiki au watu wake wa karibu, wengine inaweza kusababishwa na kumwamini Yesu. Inapotokea hali kama ile yupo Rafiki wa kweli anayeambatana na huyo mtu, huyu hawezi kumwacha labda mtu mwenye amwache.

Kutusaidia malengo yetu, tunaweza kufikiri nguvu ya kufanikisha malengo yetu huwa ni ya kwetu wenyewe, ukiona mtu amefikia hatima njema ya malengo yake usifikiri yeye ni mujuzi sana wa mambo. Elewa yupo Roho Mtakatifu anayemsaidia kufikia malengo yake aliyojiweka katika maisha yake.

Roho Mtakatifu kuja kwetu haimaniishi Yesu ametuacha, Yesu bado ni msaidizi na mwombezi wetu kule mbinguni, bado anatenda kazi yake.

“Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee”, Ebr 7:25 SUV.

Hapa duniani Roho Mtakatifu ndiye msaidizi wetu aliye ndani yetu waamini, na mwombezi wetu hapa duniani.

“Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe”, 1 Kor 6:19 SUV.

Mkaribishe Roho Mtakatifu ndani yako kwa kumwamini Bwana Yesu, utakuwa umejiongezea thamani kubwa sana mbele za Mungu, duniani na mbinguni.

Vipo vitu unapambana navyo kuvifikia lakini unashindwa kwa akili zako, kwa sababu umemwacha au umemkataa Roho Mtakatifu, umebaki unatumia nguvu na akili zako ukifikiri unaweza kufanya yote bila Roho Mungu.

Badilisha mtazamo wako namna unavyomchukulia Roho Mtakatifu, tumeona vile yeye alivyo karibia maeneo yote ya maisha yetu, anatenda kazi kwa namna tofauti tofauti kwa kila eneo.

Nimalize kwa kusema, ninaweza kusema sana ila siwezi kumaliza kuusema uzuri wa Roho Mtakatifu, huyu ndiye msaidizi anaweza kukurejesha haraka kwenye njia sahihi kuliko mtu yeyote labda mwenyewe uamue kutomsikiliza.

Karibu kwenye kundi la kusoma neno la Mungu na kushirikishana tafakari zetu kila siku kwa njia ya wasap group, ukiwa na kiu ya kujenga nidhamu hii wasiliana nasi kwa wasap +255759808081. Usihangaike kupiga simu wewe tuma ujumbe wa maandishi kupitia hii namba utaunganishwa.

Soma neno ukue kiroho
Kwetu kusoma biblia ni maisha
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081