Unyenyekevu ni kitu cha muhimu sana kuwa nacho ndani yako, ukiwa na unyenyekevu ndani yako huwezi kuabika mahali popote pale. Maana unyenyekevu unakulinda na aibu nyingi ambazo ungekutana nazo kwenye matukio mbalimbali ya kijamii.

Kuna mahali utafika ambapo watu hawakufahamu kabisa wewe ni nani mpaka pale utakapojitambulisha, sasa unapofika kwenye kusanyiko fulani kubwa. Badala kutulia viti vya nyuma mpaka pale utapotambuliwa cheo chako au nafasi yako ni ipi, ili watu waweze kukuelekeza mahali pa kukaa, wengi hujitanguliza kukaa viti vya mbele.

Badala ya kupata heshima yao inavyostahili, wengi wameondoka na aibu, baada ya kuja mtu mwenye cheo zaidi yake na kuambiwa pisha kiti mkuu akae. Lakini hii fedheha kubwa aliyoipata huyu ndugu alikuwa na uwezo wa kuikwepa mapema kabla haijampata.

Wengi tunaingia kwenye fedheha za namna hii kwa sababu hatuna unyenyekevu ndani yetu, wengine ni kwa sababu ya kukosa maarifa ndani yetu. Kukosa maarifa ndani yetu imetuingiza kwenye mambo ambayo yametufanya tudharauliwa na watu.

Neno la Mungu limebeba kila kitu, linatufundisha mambo kama haya na linatuelekeza namna ya kukaa tunapofika ugenini, kwenye sherehe mbalimbali, kwenye mikutano, kwenye ibada za kanisani.

Jambo lingine unalopaswa kulifahamu pia, unapofika ofisini kwa mtu, usikae kwenye kiti kabla hujakaribishwa na mwenyeji wako, subiri akuambie kaa kwenye kiti hicho hapo.

Haijalishi utafika kwenye ofisi ambayo huyo mwenye ofisi umemzidi umri, haijalishi utafika kwenye ofisi ambayo huyo mkuu wake umemzidi cheo. Tulia ukaribishwe na kuoyeshwa mahali pa kukaa, kwanza itakuepusha na aibu nyingi.

Ndio itakuepusha na mengi, unaweza kukaa kwenye kiti bila kukaribishwa, ukakaa kwenye kiti ambacho ni kibovu, utasema kwanini mtu aweke kiti kibovu kwenye ofisi? Hilo ni jambo lingine ila utakuwa umeshaanguka chini na aibu itakuwa imeshakupata.

Usipende ukubwa wa kujiinua sana, kama wewe ni mtu ambaye una nafasi fulani katika jamii, watu watakufahamu, na watatambua uwepo wako mahali pale. Ukipenda sana ukubwa wa kujiinua, utajiinua hata mahali ambapo hustahili kujiinua.

Hii ninayokueleza ni hekima ya Neno la Mungu, sikuelezi hekima za kibinadamu, nakueleza mambo ambayo yapo kibiblia kabisa. Mambo ambayo ukiyazingatia utakuwa salama katika uongozi wako, utumishi wako, kwenye nafasi yeyote ile utakayowekwa.

Hebu turejee maandiko matakatifu tuone yanasemaje kuhusu haya ninayokueleza hapa, hebu soma kwa makini na uifanyie kazi hii hekima kubwa iwe na kwako.

Rejea: Ukialikwa na mtu arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe, akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma. Bali ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote walioketi pamoja nawe. LK. 14:8‭-‬10 SUV.

Haleluya, unaona vile unyenyekevu unavyoweza kukuletea heshima mbele za watu, na vile unavyoweza kumfanya mwenyeji wako aweze kukukarimu vizuri. Maana unaweza kugeuka mzigo ghafla pale wakati ulipaswa kuwa baraka kwa watu.

Bila shaka umejifunza kitu kikubwa na cha msingi, usiishie hapa, yaweke kwenye matendo yale umejifunza kupitia somo hili. Utaona yakikusaidia kwenye maeneo mengi katika maisha yako.

Mungu akubariki sana.
Rafiki yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com
+255759808081