
Uongozi wa mtu huanzia nyumbani kwake, taratibu unaanza kutoka nje ya familia yake na kuwa kiongozi wa watu wengi.
Kiongozi mzuri ni yule anayeweza kujiongoza yeye mwenyewe, anayeweza kujisimamia yeye mwenyewe, na anayemsikiliza sana Mungu katika uongozi wake.
Tunapokuwa viongozi tunapaswa kuwa na moyo wa uvumilivu, yapo mambo utalaumiwa sana na kuonekana hujafanya vizuri.
Wapo watu watakuona umewapoteza kwa maamzi yako ya hovyo, kumbe wewe unachokiona kama kiongozi ni tofauti na wao.
Kulaumiwa na unaowaongoza ni jambo ambalo haliepukiki kamwe katika uongozi wako, au katika utumishi wako.
Hili tunajifunza kwa Musa, wana wa Israel walifika mahali wakaanza kumlaumu Musa kwanini aliwatoa nchi ya Misri.
Rejea: Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri? KUT. 14:11 SUV.
Kikwazo cha kuona bahari mbele yao, huku nyuma yao wanaona wanafuatiliwa na jeshi la Misri. Wakasahau shida walizokuwa wanakutana nazo, wakaanza kumlaumu Musa.
Nimefurahia sana majibu ya Musa aliyowajibu wana wa Israel, inaonyesha wazi kabisa Musa alikuwa anaelewa anachofanya.
Rejea: Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. KUT. 14:13 SUV.
Mtumishi huyu wa Mungu aliyepewa jukumu la kuchunga na kuongoza, Mungu alimpa namna ya kusema nao.
Alikuwa na ujasiri wa kusema kile anaona Mungu atakifanya kwao, hakuwa na wasiwasi kutokana na majibu yake.
Rejea: BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya. KUT. 14:14 SUV.
Huyu ni kiongozi ambaye uhusiano wake na Mungu upo vizuri, anajua kabisa lipo jambo Mungu atalitenda kwao. Hata kama wanaona kuangamizwa, yeye anaona kwa sura nyingine nzuri.
Tukubali kutupiwa lawama ila tusikubali kurudishwa nyuma na maneno makali ya wale tunaowaongoza au tunaowalea kiroho.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com