Mara nyingi nimekuwa nikishuhudia watu wengi wakisongwa na changamoto za maisha kiasi kwamba wamefika mahali wamevunjika moyo. Wameona wao ni wa kufa tu, hakuna jambo lingine la kufanya hapa duniani zaidi ya kusubiri kufa tu.
Sio kuona watu wengine tu, nakumbuka miaka ya nyuma kidogo, nimewahi kukumbwa na hali kama hii, mbaya zaidi sikuwa na mtu wa karibu kunitia moyo zaidi ya kusikiliza nyimbo, sikuwa na Neno la Mungu la kusema linivushe sehemu fulani. Nilikuwa mtupu ndani yangu, tena nilikuwa mtoto kiroho kweli kweli.
Nilikuwa nimejaa hofu nyingi sana, kujiamini kwangu ilikuwa hakupo ndani yangu, nilishajidharau mimi mwenyewe na kuona sina kitu cha kusema mtu akanielewa. Changamoto za maisha zilinifanya nijione hivyo, hali duni ya maisha ilifanya niwe hivyo.
Pamoja na magumu hayo yote ilikuwa ni shule kwangu, shule ambayo naona imekuwa na msaada mkubwa sana kwenye maeneo mengi katika maisha yangu ya sasa. Shule hiyo ilikuwa na mambo yasiyotamanika kuendelea kujifunza ila nilitoka nikiwa imara sana. Baada ya hofu kuniachia nilijiona nikiwa huru na imara sana katika maisha yangu.
Ushuhuda huu mfupi niliokushirikisha hapa nilitaka uone kwamba kuna maeneo watu tunapitia, yapo maeneo magumu sana watu wanapitia na hawajui wafanye nini ili waweze kutoka humo. Yupo mtu anaenda kanisani kila jumapili ila hana habari kama anaye Mungu ambaye anaweza kumtwisha mizigo yake.
Wapo watu wamelemewa na mizigo mizito, mizigo ambayo imekuwa tishio la uhai wao, hawajui pa kuitua ni wapi. Na kama wanajua ni wapi pa kuitua, wanakuwa hawana uhakika sawasawa kama kweli Mungu anaweza kuwasaidia shida walizonazo.
Kutoamini kwao inaweza kuchangiwa kiasi kikubwa sana kwa kukosa Neno la Mungu mioyoni mwao, hili ndilo tatizo kubwa la wakristo walio wengi. Wengi Neno la Mungu halimo mioyoni mwao, zaidi sana kuna mistari michache ya kukariri, ambayo haiwezi kuleta badiliko katika maisha yao.
Mzigo unaozungumziwa hapa, haimanishi gunia la mkaa, haimanishi gunia la mahindi, haimanishi gunia la mchele, wala haimanishi gunia la viazi. Mzigo wako unaweza ukawa familia yako, unaweza ukawa masomo yako, unaweza ukawa ndoa yako, unaweza ukawa mahusiano yako ya uchumba yanakutesa.
Hayo yote ni mzigo wako, mzigo ambao unaweza kumtwisha Mungu pekee, yeye ndiye atakusaidia kuondokana na shida yako. Yeye ndiye ataweza kukupumzisha na mzigo ulionao katika maisha yako, anakusubiri utambue na uchukue hatua ya kumwendea yeye.
Mungu ndiye anayetuagiza tuende kwake, haijalishi madaktari wamekuambia na vipimo vimeonyesha hutozaa mtoto maisha yako yote, kutokana na shida uliyonayo kwenye kizazi au tumbo la uzazi. Hilo peleka kwa Yesu Kristo, atakusaidia, na utapata mtoto.
Sio mimi nasema ni Yesu mwenyewe anasema twende kwake wenye kulemewa na mizigo, naye atatupumzisha. Haleluya, kama pumziko la kutua mizigo yetu lipo, kwanini uendelee kusumbuka na mizigo yako?
Rejea: Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. MT. 11:28 SUV.
Neno la Mungu ni hakika na Amina, huna haja kujiuliza itakuwaje hii shida yangu kuisha, wewe amini, wewe uliumbwa kwa mfano wa Mungu. Hakuna mnyama wala ndege aliumbwa kwa mfano wa Mungu, ni mwanadamu pekee ndiye aliumbwa kwa mfano wa Mungu.
Sijui nini inakukabili katika maisha yako, kiri ushindi, hata kama kuna ugonjwa unakusumbua sana, madaktari wameushindwa, yupo daktari mkuu asiyeshindwa jambo lolote. Amini hivyo ndugu yangu, amini Neno la Mungu.
Rejea: Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. ISA. 53:4-5 SUV.
Kwa kupigwa kwake sisi tumepona, ndio kwa kupigwa kwake wewe umepona, ugonjwa unaokusumbua usikutishe. Imani yako ipeleke kwa Bwana Yesu, utaona mabadiliko yakianza kutokea kwako, utaanza kuona kustawi tena kwa upya kabisa kukija kwako.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.