Kuna watu wana visababu vingi haijawahi tokea, hawezi kukosa sababu kwanini amekwama eneo hilo alipo sasa. Kuna sababu zingine zinaonekana ni za kuendelea kujitia moyo, ila ukweli ilikuwa haina sababu ya kujisingizia kwa hilo alilopaswa kuchukua hatua.

Upo umri ambao huwa wengi tunajidanganya Sana, na sijui watu walipata wapi andiko hilo, la kusema kula ujana sasa hivi ili uzeeni usije ukaanza kufanya vitu ambavyo ulipaswa kufanya ujanani.

Ikiwa na maana kwamba, tembea kwa uasherati na wadada/wakaka uwezavyo ili ukifika umri fulani usije ukafanya hilo kosa. Ajabu yake ni kwamba mtu mpaka amezeeka ila bado ana vitabia vya kigono kigono.

Hili jambo linatutafuna tulio wengi sana, na wengi wameharibika hapa kwenye umri mdogo wakifanya yaliyo machukizo mbele za Mungu. Kwa kigezo cha wanakula ujana, wakisahau hakuna umri fulan wa kutenda dhambi na upo umri fulani wa kumtumikia Mungu.

Laiti tungeyajua haya mapema tungekuwa na mabikira wengi sana wa kike na wa kiume, wakiwa watumishi wa Mungu wazuri kabisa. Wasio na utani mbele za Mungu, wakisimama madhabahuni wanafanya kweli, wakisimama kutoa huduma yeyote lazima nguvu za MUNGU zishuke.

Umri umekuwa kitanzi kibaya sana kwa vijana wengi, tunachezea muda mwingi sana kwa mambo yasiyo na msingi wowote. Huku tukijiona sisi ndio wajanja wa mjini au kijijini, wote tunajua wapo wale wadada/ wakaka wanaojulikana mtaani wao ndio wajanja sana. Kila kitu wao wanajua, hawapitwi na umbea wa aina yeyote wao wanakuwa nao.

Tunakuja kushtuka tayari tunaitwa baba/mama, hapo unakuwa huna tena kujivunia ujana wako ulifanya nini wakati bado upo peke yako. Ndipo unakuta baba/mama alipoteza muda wake mwingi kwa vitu ambavyo havikumzalia Mungu matunda.

Wengine tumekaa tunasubiri tukifika umri fulani ndio tutaanza kuishi maisha matakatifu, maisha yenye barua njema kwa watu wengine wasiomjua Kristo na wanaomjua Kristo. Tayari unakuwa umekosa nafasi yako ya mhimu kufanya vitu vya kiMungu ukiwa na umri mdogo.

Najua ulipokuwa shule ya msingi/sekondari umeshuhudia vijana wadogo wakiwa na nguvu ya Mungu, wakihudumia jamii kwa kumhubiri Yesu Kristo. Chuoni wengi wanakuwa watu wazima, tunaangalia umri ule wa shule ya msingi na sekondari, unakuwa ni umri wenye shida sana kwa vijana wengi wanaoanza kupevuka.

Lakini tunamwona kijana mmoja ndani ya biblia, ambaye ni mdogo sana mwenye umri wa miaka nane, ambapo tunaweza kusema bado ananukia maziwa ya mama. Akishika nafasi ya kifalme kumtumikia Mungu katika nafasi ile, biblia inatuweka bayana kabisa kuwa kijana yule alifanya vizuri sana katika uongozi wake.

Tunaweza kujiaminisha zaidi kwa kusoma maandiko haya;
Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja huko Yerusalemu. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, akaziendea njia za Daudi babaye, asigeuke kwa kuume wala kwa kushoto. 2 NYA. 34:1‭-‬2 SUV.

Unasubiri nini mpaka sasa hujaanza kumtumikia Mungu kwa kile amekupa ndani yako umtukuze, anza sasa achana na dunia hutoiweza.

Ikiwa upo shule mwonyeshe Yesu wako waziwazi bila kificho, usijizuia kile Mungu amekipanda ndani yako umtumikie. Umri wako sio shida, watu wataona Roho wa Mungu akiwa ndani yako kwa matendo yako.

Kuanzia sasa ondoa mawazo potofu ya kucheza na umri ukisubiri uoe/uolewe ndio uanze kumhubiri Yesu Kristo kwa bidii. Huko ni kujidanganya ndugu yangu, kuanza ni hapo ulipo, ndio unapaswa kuanzia.

Mungu akubariki sana kwa muda wako,
Usiache kujifunza NENO siku zako zote.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com