“Lakini yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba”, Lk 5:16 SUV.

Hapa tunamwona Luka anasisitiza zaidi ya waandishi wengine wa vitabu vya injili(Marko, Yohana, Mathayo) kuhusu nafasi ya maombi katika maisha na kazi ya Yesu.

Roho Mtakatifu alipomshukia Yesu katika mto Yordani alikuwa anaomba Mungu.

“Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe”, Lk 3:21‭-‬22 SUV.

Wakati mwingine Yesu alijitenga na makundi ya watu akaenda akaomba na alikuwa anakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu.

Tunaona pia kabla ya kuchagua wale wanafunzi kumi na wawili alimwomba Mungu kwanza kwa masaa ya kutosha.

“Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu”, Lk 6:12 SUV.

Tunaona pia wakati wa kubadilika sura yake alikuwa mlimani kuomba, na kubadilika kwake kulitokea akiwa katika kusali/kuomba.

“Baada ya maneno hayo yapata siku nane, aliwatwaa Petro na Yohana na Yakobo, akapanda mlimani ili kuomba. Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta”, Lk 9:28‭-‬29 SUV.

Tunamwona Yesu pia kabla ya kuwafundisha wanafunzi wake sala ya Bwana alikuwa anaomba Mungu.

“Ikawa alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake”, Lk 11:1 SUV.

Tunaona pia pale Gethsemane aliomba sana (Lk 22:44), pia akiwa juu ya msalaba aliwaombea wengine (Lk 23:34).

Tunaona pia katika maneno yake ya mwisho kabla ya kifo chake yalikuwa ni maombi (Lk 23:46), hayakuwa tu maneno ya kawaida.

Luka anaeleza kuwa Yesu aliomba baada ya kufufuka kwake (Lk 24:30)

Tunapojifunza kupitia maisha ya Yesu tunaona katika injili nyingine aliomba kabla ya kutoa mwaliko, “njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo” (Mt 11:25-28).

Hatuishi hapo, tunamwona Yesu aliomba katika kaburi la Lazaro (Yn 11:41-42), na wakati wa kushiriki chakula cha Bwana (Yn 17).

Kwanini nimekupitisha kwa Yesu sana, nataka uone umhimu wa maombi katika maisha yako ukiwa kama mwamini au mtumishi wa Mungu.

Ukiwa utayachukulia maombi kawaida na kuona sio jambo la muhimu katika maisha yako, utakuwa umejitangazia kujikwamisha kwa mambo mengi sana.

Weka ratiba ya maombi katika maisha yako, mwombe Mungu kwa kila jambo la maisha yako, usichukulie urahisi kwa kila jambo ukaacha kuomba.

Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081