Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake”, Mt 14:23 SUV.

Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake”, Mt 14:23 SUV.

Moja ya kipengele ambacho wengi hatukitilii maanani sana ni hichi cha kuwa na faragha na Mungu kwa kuomba, wengi husubiri hadi tuwe na shida au kusanyiko fulani la kanisa, na wengine hadi tusikie maombi yakitangazwa.

Sio vibaya kutii na kufuata vile kanisa linakutaka ufanye, ila ukiwa kama mwana wa Mungu unapaswa kuwa na ratiba yako binafsi ya maombi, unapaswa kuwa na utulivu wa peke yako.

Tunajifunza hili kwa Yesu alipokuwa duniani, mara nyingi Yesu alitafuta muda wa faragha na Mungu, jambo ambalo alilifanya mara kwa mara katika maisha yake.

Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko”, Mk 1:35 SUV.

Tukitaka kustawi vizuri katika maisha yetu ya kiroho, tunapaswa kuwa na muda wa faragha na Mungu wetu aliye hai, hili linapaswa kuwa kwa kila mwamini, sio kwa watu au kundi fulani maalumu.

Tunapaswa kuelewa kwamba kukosekana kwa shauku ya maombi ya faragha na mawasiliano na Baba yetu wa mbinguni ni ishara ya uhakika kwamba maisha ya kiroho ndani yetu yako katika mchakato wa kushuka chini.

Ukiona hali ya kukosa shauku ya kumwomba Mungu, huna budi kuyaacha yote yanayomuudhi Bwana na kujitoa upya kwa bidii ya kumtafuta Mungu na neema yake iokoayo.

Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa”,

Lk 18:1 SUV.

Usikubali kukaukiwa na kiu ya maombi ndani yako, ukiona hali ya kukosa kiu, kaa chini ujitafakari, utagundua jambo lililosababisha hiyo hali ikutokee.

Yamkini ni mwenendo wako usio sawa mbele za Mungu, ama inawezekana vipaumbele vyako kwa mambo ya Mungu havipo tena katika maisha yako. Ama umekata tamaa kabisa na huna imani na Mungu tena.

Ukipoteza kiu ya maombi na ukaacha kuwa na faragha na Mungu wako, utaona kiwango chako cha kiroho kikishuka kwa kasi kubwa, hata huduma aliyoweka Mungu ndani yako utakuwa unaifanya pasipo matokeo makubwa.

Kataa kuchoka, kataa hali ya kukosa faragha ya maombi na Mungu wako, jenga utaratibu mzuri wa kujificha mahali kuongea na Mungu wako, hajalishi mazingira yako, ukiwa na nia hutokosa mahali pa utulivu kuongea na Baba yako wa mbinguni.

Tunaposema maombi sio lazima upaze sauti kubwa, inawezekana mazingira yako hayakuruhusu kufanya hivyo au una mahitaji ya siri hutaki mwingine asikie unachoomba, unaweza kuomba kwa sauti ya chini sana na ukaona matokeo makubwa katika maombi yako.

Ukiwa unasoma ujumbe huu na uliacha maombi ya faragha, anza sasa, omba toba mbele za Mungu na ujenge utaratibu wa kuomba Mungu, yapo mengi sana ya kuombea kadri Roho Mtakatifu atakavyokuwa anakupa msukumo.

Maombi ni afya kwenye huduma yako, kazi yako, biashara yako, ndoa yako, watoto wako, na mengine mengi. Ukiwa na muda wa kuzungumza na Baba yako, yapo mengi sana magumu utavuka, yapo majaribu mengi utaepukana nayo.

Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu”, Mk 14:38 SUV.

Unapata changamoto ya kushindwa kusoma biblia kila siku na umekosa njia nzuri ya kukusaidia kusoma? Tumekuandalia kundi la wasap la watu wenye kiu ya kusoma biblia kila siku na kutafakari, wasiliana nasi kwa wasap +255759808081 utaunganishwa uwe miongoni mwao.

Soma neno ukue kiroho

Mungu akubariki sana

Samson Ernest