Kama hujawahi kujiuliza hili swali, anza kujiuliza leo, je! Ukiondoka hapa Duniani utaandikwa kwa mema yapi? Je! Kipi chema kitakufanya uishi ndani ya mioyo ya watu? Je! Kipi kitakufanya ukumbukwe kizazi hadi kizazi?

Kama unaishi ilimradi siku ziende, utakuwa unakosea sana, leo tunasoma habari za akina Esther kwa sababu walifanya jambo. Leo tunasoma habari za kina Ibrahim kwa sababu kuna jambo walifanya mbele za Mungu, wapo watumishi wengi sana kuanzia agano la kale hadi agano jipya tunasoma habari zao.

Lazima ufike mahali ujihoji mwenyewe, una faida gani kwa uwepo wako hapa duniani? Lipi haswa unalolifanya na Mungu wako akatukuzwa kupitia hilo unalolifanya?

Mfano rahisi, unaweza kujitathimini kupitia mahali unapofanyia kazi. Manufaa gani watu wanayapata kupitia wewe, siku haupo kazini watu wanaona pengo lako au hawaoni chochote na hawajui kama umechukua likizo.

Nyumbani kwenu wanajivunia nini kutoka kwako, kipi haswa wanaweza kufika mahali wakasema tuna mtu muhimu sana Mungu ametupa katika familia yetu. Au upo nyumbani kama mzigo fulani hivi, yaani hakuna kitu cha thamani wanachokipata kutoka kwako.

Kwa kile unamtumikia Mungu, unatumika vile ipasavyo na watu wanamtukuza Mungu kupitia wewe au unafanya huduma kimazoea au unafanya huduma kwa kulazimishwa/kusukumwa.

Leo tunajifunza kupitia mti huu wa mzabibu, ambapo sisi leo tunaweza kuutumia kujitathimini maisha yetu kwa ujumla. Hebu soma hapa kwa umakini.

Rejea: Mwanadamu, mzabibu una sifa gani kuliko mti mwingine, au tawi la mzabibu lililokuwa kati ya miti ya msituni? Je! Mti wake waweza kutwaliwa, ili kufanya kazi yo yote? Watu waweza kufanya chango kwa huo, ili kutundika chombo cho chote? Tazama, watupwa motoni kwa kuni moto umeziteketeza ncha zake zote mbili, nao umeteketea katikati, je! Wafaa kwa kazi yo yote? Tazama, ulipokuwa mzima, haukufaa kwa kazi yo yote; sembuse ukiisha kuliwa na moto, na kuteketea; je! Waweza kufaa kwa kazi yo yote? EZE. 15:2‭-‬5 SUV.

Ndugu yangu, wewe una sifa gani ambayo itakufanya watu wajutie kukupoteza, kulia watalia sawa kwa sababu umeondoka. Kipi haswa cha ziada ambacho kitawafanya watu waone Mungu amekuchukua mapema, nasema hivi; kipi kitakufanya ukumbukwe kama Doricas?

Kipi kitakutetea usiangamizwe? Kile kitashawishi watu waseme hapana huyu hastahili hii adhabu, waseme hapana huyu mtu amekuwa baraka sana kwetu. Mungu alipo mbinguni ajivunie wewe, ni kipi hicho kitamfanya Mungu ajivunie wewe.

Mungu alijivunia mtumishi wake Ayubu, alijua ana mtumishi wake imara, ndio maana shetani alienda kumshataki na Mungu akampa kibali cha kumpitisha Ayubu kwenye majaribu mazito. Na Mwisho wa Ayubu ulikuwa ni ushindi mkubwa.

Usije ukaonekana huna faida kama huu mti wa mzabibu ulivyoonekana hufai kwa chochote. Hata kama ukichomwa moto hakuna kitakachoharibika/kupungua. Inaonyesha ni kiasi gani huu mti hukuwa na umhimu/thamani sana kwa watu wake.

Nimalize kwa kusema, hakikisha unakuwa mtu wa faida kwa wengine, unapokuwa faida kwa wengine kwa utukufu wa Mungu. Hata Mungu mwenyewe anakuona wa maana sana kwake, acha kuishi maisha ya jumuiya, jitofautishe na wengine kwa kitu alichokupa Mungu wako.

Mungu akubariki sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081