“Akatoka Yesu na wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya Kaisaria-Filipi; na njiani akawauliza wanafunzi wake, akasema, Watu huninena mimi kuwa ni nani? Wakamjibu, Yohana Mbatizaji; wengine, Eliya; wengine, Mmojawapo wa manabii. Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo”, Mk 8:27‭-‬29 SUV.

Tunapokuwa katika nafasi Fulani, tunahitaji watu ambao wataweza kutueleza ukweli, watu ambao hawana hila na wivu ndani yao, watu wanaotueleza ukweli kwa upendo kabisa, wakituambia vile tunatenda au kufanya.

Kwa kawaida wengi hupenda kusikia mazuri tu, lakini kuna wakati tunahitaji kuambiwa hata yale tusiyoyapenda ilimradi yawe ni kweli, na inakusaidia kuchukua hatua za kukufanya uondokane na maisha hayo.

Tunapoacha kusikia wengine wanatuonaje, tunaweza kujiona ni bora Zaidi ila inaweza kutuingiza kwenye hatari ambayo tungeacha mlango wazi wa kusikiliza wengine wanayotuambia kutuhusu, tungeepuka kuingia kwenye anguko.

Yesu alitamani kufahamu wanafunzi wake wanasikia nini kule nje kuhusu yeye, wanafunzi wake walikuwa wazi na huru kumweleza kile wanachosikia huko nje watu wanasema, maana yake wanafunzi wa Yesu walikuwa wanakutana na maneno mengi juu ya mwalimu wao.

Huenda hawa wanafunzi walifika wakati wakapata wasiwasi juu ya yale wanayosikia kuhusu Yesu, nasema hivyo kutokana na ubinadamu wetu, unapokuwa humfahamu vizuri mtu alafu ukawa naye karibu katika ofisi moja. Unaweza kujikuta wasiwasi unakupata kutokana na maneno ya watu.

Wakati mwingine usipokuwa makini unaweza kumchukia mwalimu wako, mchungaji wako, au bosi wako, au mfanyakazi mwenzako, au jirani yako, kutokana na taarifa unazozipata kuhusu yeye na unaweza kumweka kwenye kundi tofauti na alivyo.

Ikiwa huna uhuru au unaogopa kumweleza kile unasikia kwa watu wengine, unaweza kufika wakati ukaona unayosikia ni ya kweli, kumbe ni maneno ya watu na mitazamo yao hasi juu yake. Lakini anavyosemwa na alivyo sivyo hivyo.

Tukiwa kama wazazi tunahitaji kufahamu watoto wetu wanatusemaje au wanatuonaje! ndio ni muhimu sana, unaweza kuona haina haja kufahamu hilo ila ni muhimu sana kama mzazi mzuri kwa watoto wake. Wakati mwingine watoto wako wanaweza ukawa wanakuona kama adui yao mkubwa, vyema kufahamu sababu ni nini ya kukuona hivyo.

Ukiwa mwalimu wa shule, kiongozi wa serikali kwa ngazi yeyote ile, na ukiwa kiongozi wa kanisa, unahitaji kufahamu unaowaongoza wanakuonaje na kukusamaje, utasema ni ngumu kufahamu, sio ngumu maana wale wanaokusaidia kazi au wanaokuzunguka au wa chini yako wana mambo mengi kukuhusu wewe.

Yesu alivyoelezwa na wanafunzi wake vile watu wanamsema yeye ni nani, alirudi kwao na kuwauliza swali hilo hilo kuwa wao kama wao wanamsema au wanamwona ni nani?

“Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo”, Mk 8:29 SUV.

Ndio tunapaswa kujua wale tunaowauliza kuhusu watu wengine wanasemaje kuhusu sisi, na wao wanatuonaje sisi, tuko vipi, wasije na wao wakawa wanatuona tofauti na tulivyo, yaani vile watu wanatuchukulia kwa ubaya na wao wakawa wanatuona hivyo.

Tunamwona Petro peke yake alimjibu Yesu swali lake kuwa “wewe ndiwe Kristo”, hatujui hawa wanafunzi wengine walikuwa wanamwonaje Yesu, hii inatuonyesha wazi kuwa watu wetu wa karibu wanaotusaidia kazi au tunaofanya nao kazi hawana uhakika na sisi, au wanatuona tofauti na tulivyo.

Kujifanyia tathamini kupitia watu wengine ni jambo la muhimu sana na tunapaswa kulifanya mara kwa mara katika maisha yetu, hasa tunaoongoza au kuwatangulia watu, na kuishi na watu, tusishikilie sana misimamo yetu na kujiona tupo sahihi kwa kila jambo au eneo.

Mwisho, ninakualika kujiunga na mpango huu mzuri wa kusoma biblia kila siku na kupata muda wa kushirikishana tafakari na wandugu wengine, na wewe kupata nafasi ya kusoma tafakari za wengine. Kama unahitaji kujiunga na mpango huu, wasiliana nasi kwa wasap +255759808081 ili uweze kuunganishwa kwenye group.

Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest