Haleluya,
Leo uzinzi na uasherati ni jambo la kawaida kwa waumini wengi makanisani, sio jambo la kuogopeka kama ilivyokuwa zamani ukisikia mkristo ana fanya uzinzi/uasherati. Lazima kila mtu apate mshangao mkubwa.
Leo uasherati na uzinzi ni sehemu ya ibada za watu, kijana wa kiume anatembea na wadada bila wasiwasi wowote. Dada naye hana aibu kabisa anatembea na wakaka kanisani, na akiona kanisani atajulikana haraka, anakuwa na mkaka wa kanisa lingine nje na kanisa lake.
Wengine wanaona wadada/wakaka wa kanisani watawasumbua, wanaamua kuwa na wakaka/wadada wa kiislamu. Wanatembea nao weee mwisho wa siku ni kupeana mimba, na wengine wanapeana magonjwa, na wengine mwisho wake unashangaa mdada/mkaka anabadili na dini, Yesu Kristo kwake anakuwa sumu.
Baba zetu na mama zetu nao hawaishiwi mikasa, unakuta mama mtu mzima hatulii kwenye ndoa yake. Anahaingaika na vijana wadogo huko nje, mwingine anahangaika na wake za watu, na mwingine anahangaika na waume za watu.
Mwisho wa machafu hayo yote ni aibu kwa mhusika, tena aibu kubwa mno. Tumeshindwa kusimama vizuri na kumhubiri Kristo kwa sababu ya uzinzi na uasherati.
Tunapoonywa hatusikii kabisa, tunasubiri mambo yameharibika ndio tunaanza kukumbuka maneno ya walimu mbalimbali waliyotuasa tuache uzinzi na uasherati.
Najua yupo miongoni mwetu humu mtu mwenye tabia hii ya uzinzi/ uasherati, moyo wake ni shahidi wa tabia yake. Anajua uchafu anaoufanya, kabla aibu na fedheha havijamkuta, nakusihi uache mara moja na utubu kama unasoma ujumbe huu.
Narudia tena, najua yupo humu mwenye tabia hii, huenda wewe ni miongoni mwao. Nakusisitiza tena na tena, achana na wake za watu, achana na waume za watu, achana na tabia ya kulala ovyo na wakaka/wadada. Subiri wakati wako uoelewe/uoe, utafanya hayo yote mpaka tani yako.
Turudi kwenye maandiko matakatifu yanasemaje kwa hili, usije ukasema naongea tu hakuna maandiko ya hivyo. Naomba usome Neno hili, nimeona nitumie biblia ya habari njema ina kiswahili kirahisi sana.
Rejea: Mwishoni mwa maisha yako utaomboleza wakati mwili wako utakapoangamizwa. Hapo utasema, Jinsi gani nilivyochukia nidhamu, na kudharau maonyo moyoni mwangu! Sikuisikiliza sauti ya waalimu wangu, wala kuwategea sikio wakufunzi wangu. Methali 5:11-13 BHND.
Nakusihi tena, usisubiri ufumaniwe uanze kukatwakatwa mapanga ndio ukumbuke haya, usisubiri uzalishwe na mume wa mtu alafu akikukimbia ndio uanze kukumbuka maonyo haya. Usisubiri uambukizwe magonjwa yasiyo na tiba, ndio uanze kukumbuka maneno haya.
Wakati ni sasa, amua leo kuagana na uzinzi/uasherati, wenzako tuliona hapafai huko tukaona heri kuingia mzima mzima kwa YESU. Kuliko kuwa nusu nusu, ingekuwa ni dili kuwa mzinzi tungeendelea kuwa huko, lakini nakwambia hakufai ndio maana tumekimbilia kwa YESU.
Usipoelewa hayo maandiko matakatifu, nielewe hata mimi, acha kabisa biashara ya uzinzi na uasherati. Huhitaji kwenda kuomba ruhusa mahali popote pale, unahitaji kuchukua maamzi yako binafsi tena ya kumaanisha kutoka moyoni.
Usifike mahali ukaanza kusema hivi; Hapo utasema, Jinsi gani nilivyochukia nidhamu, na kudharau maonyo moyoni mwangu! Sikuisikiliza sauti ya waalimu wangu, wala kuwategea sikio wakufunzi wangu. Methali 5:12-13 BHND
Namaliza kwa kusema, mwenye sikio na asikie maneno haya, imekupendeza fanyia kazi. Maana wahenga walisema “sikio la kufa halisikii dawa”
Chapeo Ya Wokovu
www.chapeotz.com
chapeo@chapeotz.com
+255759808081