Haleluya,

Mungu wetu ni mwema kwetu, anaendelea kutupa kibali cha kuendelea kuishi, haijalishi tunapita katika changamoto mbalimbali ila bado anatupa nguvu na kibali cha kusonga mbele.

Kumtambua mtu mwenye tabia chafu wala haichukui muda mrefu sana, utajua kile kilichoujaza moyo wake pale anapozungumza.

Keti na kijana au mzee mwenye tabia chafu, haitachukua muda mrefu utamwona yakimtoka ya moyoni. Anaweza kuongea alafu baadaye akajishtukia kwa kile amekizungumza, lakini tayari alishazungumza.

Jinsi anavyoanza kuongea uchafu wake muda mwingine anaweza msiongee naye, ila jinsi akavyotamka na mtu mwingine pembeni ndio utajua umeambatana na mtu wa namna gani.

Mfano mwanaume asiyejiheshimu katika ndoa yake, akikutana na mwanamke mbele yake utamwona anaanza kuweweseka na kuongea ujinga ujinga.

Mwingine anaweza kujikausha asiongee lolote kutokana na labda hamjazoeana au mazingira alipo ni mageni anachofanya ni kujitahidi kujizuia kusema. Ila haichukui mzunguko mrefu sana utamjua tu ni mtu wa namna gani.

Hili nimeona kwa wanaume wengi wasiojiheshimu katika ndoa zao na wale wasiojiheshimu katika ujana wao. Mara nyingi sana wakifika miji/mikoa ya watu, cha kwanza utamsikia nitafutie mwanamke/mdada wa kulala naye.

Kile kimeujaza moyo wa mtu ndicho anaweza kukizungumza mara nyingi zaidi…mfano mtu aliyezoea kutanguliza matusi kwanza ndipo aongee alichotaka kuongea. Atajihidi kujikaza na kujaribu kujibana ili asionekane tabia yake, ila akiendelea kuongea utajua kabisa huyo ni mtu wa namna gani.

Mtu mwovu, yeye huwaza mabaya masaa mengi sana, awe kitandani atawaza ujinga, awe kwenye shughuli zake atawaza ujinga, awe sehemu yeyote ile atawaza tu uovu. Maana ufahamu wake umetawaliwa na uovu.

Rejea: Maneno ya kinywa chake ni uovu na hila, Ameacha kuwa na akili na kutenda mema. Huwaza maovu kitandani pake, Hujiweka katika njia mbaya; ubaya hauchukii. ZABURI 36:3‭-‬4 SUV.

Tofauti ya mtu mwovu na mtu mwema ni kwamba, mtu mwema yeye huwaza muda mwingi mambo mazuri. Hata kusema kwake utamwelewa kabisa huyu mtu utamkuta ana hofu ya Mungu ndani yake.

Uzuri wa hili eneo huwezi kuvaa sura ya wema kwa muda mrefu utaumbuka tu. Maana utajikuta yanakutoka yale yameujaza moyo wako.

Tuache kona kona, kama tumeamua kuokoka kweli mioyo yetu inapaswa kujaa Neno la Mungu ili tuweze kunena maneno ya hekima vinywani mwetu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.