Tukiachana na changamoto zingine za maisha zinazowakabili wanawake, moja ya changamoto kubwa inayowasumbua wadada/wanawake wengi ni kuwa na hamu ya kuolewa na mwanaume sahihi kwao. Ila pamoja na kuwa na hamu hiyo, hao wanaume wanakuwa hawaonekani, wengi wanaokuja kwao ni wale wanaotaka kufanya nao uasherati kwanza.

Hakuna kitu kibaya kinachokujia katika maisha yako bila kuwa na sababu, kuchelewa kuolewa kwa mwanamke, ipo sababu ambayo imepelekea huyu dada kuchelewa kuolewa. Ndio lazima pawepo na sababu ya kumfanya huyu mwanamke achelewe kuolewa hadi kufikia umri mkubwa, wa kutoka kwenye usichana hadi kuwa mtu mzima.

Yupo mwanamke wakati wa usichana wake alikuwa anachagua sana wanaume kwa kuzitegemea akili zake mwenyewe, badala ya kumwomba Mungu ampe mume sahihi. Yeye alikuwa hana huo muda, na kama alikuwa nao, alikuwa anaangalia zaidi uwezo wake kiuchumi, alikuwa anangalia sura, alikuwa anaangalia uvaaji wa mwanaume.

Kuangalia vitu kama hivyo sio vibaya, isipokuwa anapozitegemea akili zake katika hivi vitu, bila kuruhusu Mungu ahusike katika uchaguzi wake. Wengi wameishia kuchagua hadi ikafika mahali wanaume hawaji tena kwake kama zamani, na huenda wanaokuja kwa wakati huo sio wale walio siriazi.

Yupo mwanamke mwingine wakati wa ujana wake, alikuwa bado hajamjua Yesu Kristo, hata kama alionekana ameokoka, nyuma yake maisha yake ya wokovu hayakuwa vizuri. Walikuja wanaume mbalimbali wakacheza naye kwa ngono, hadi wengine wakazaa naye mtoto/watoto wakamwachia hapo awalee.

Sasa walipofika wakati wakaona wampe Yesu Kristo maisha yao kwa upya, wakaachana kabisa na tabia chafu, wakawa siriazi na mambo ya Mungu, yaani wakaanza kumaanisha katika maisha yao ya wokovu. Siku za mwanzo walikuwa wanaona matumaini makubwa sana ya kupata wanaume wazuri wanaomcha Mungu.

Lakini cha kusikitisha kwao, kadri siku zilivyozidi kwenda mbele yale matumaini makubwa waliyokuwa nayo, yale matumaini makubwa waliyokuwa wanapewa na watu mbalimbali waliokoka siku nyingi. Matumaini yao yalifika wakati yakaanza kufifia/kupungua siku hadi siku.

Ulikuwa unamwona dada huyu au mwanamke huyu alikuwa na bidii sana kwa mambo ya Mungu, lakini kadri anavyoona wadogo zake wanaolewa na wanaume wazuri, tena kwa ndoa nzuri. Dada/mwanamke huyu moyo wake unaanza kusinyaa na kujiona yeye hawezi tena kuolewa na mwanaume sahihi wa kufunga naye ndoa ya kikristo.

Wengi wanapofika hatua hiyo ya kukata tamaa, huwa wanaona waache na wokovu, wengine huwa wanaona waache kujibidiisha na mambo ya Mungu. Yupo alikuwa na bidii sana katika ibada, ghafla anaacha kuwa mtu wa ibada, yupo alikuwa mwombaji mzuri sana, ghafla anaacha maombi, yupo alikuwa msomaji mzuri sana wa Neno la Mungu, ghafla anaacha kabisa kusoma Neno la Mungu.

Anapoacha hayo yote, asipopata mtu wa kumsaidia haraka, na huyo atakayemsaidia ushauri, akawa hataki au akawa hayupo tayari kuchukua ushauri atakaopewa, mwanamke huyu anaenda kurudi kwenye maisha yake ya kale. Asiporudi, basi atakuwa wa mkristo wa kawaida tu, yaani ile bidii yake kwa mambo ya Mungu haitakuwepo tena.

Baada ya kujua hayo yote, unawezaje sasa kuvuka kipindi hichi kigumu kwako wewe kama wewe, ili uweze kupata hitaji la moyo wako. Na ili uweze kupokea majibu ya maombi yako uliyoomba sana kipindi cha nyuma, na ukafika mahali ambapo upo sasa, ukawa umevunjika moyo wako, ukawa huna matumaini tena ya kupokea majibu yako.

Hebu tuone Neno la Mungu linasemaje, unaweza kuona umesubiri sana, unaweza kuona labda Mungu hawezi kukujibu tena, au umeona Mungu bado anakumbuka dhambi zako za zamani. Unapaswa kujua Mungu sio mwanadamu hata aseme uongo, maana amesema akishakusamehe dhambi zako hawezi kuzikumbuka tena.

Rejea: Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba. 2 Petro 3:9.

Haleluya, huenda hapo ulipo umeona Mungu amekawia sana kukujibu hitaji lako, la mume, fahamu kwamba, Mungu hatakawia kutimiza ahadi yake kwako. Kama kiu yako ni kuolewa, huna kosa katika hilo, cha msingi ni kuwa na uvumilivu, haijalishi unaona umri umeenda sana.

Mungu huwa hatazami kama mwanadamu anavyotazama, utakosea pale utapovunjika moyo wako, na kupunguza ile bidii ya kulitumikia kusudi la Mungu. Unachotakiwa kufanya ni kuendelea kujibidiisha na mambo ya Mungu, yeye ana wanaume wa kutosha, ana stoo ya kutosha ya wanaume, ukiwa mwaminifu kwake atakutolea mwanaume mmoja kwenye stoo yake.

Huna haja ya kuwa na mashaka, kikubwa ni kuwa na subira, unayemtumikia ndiye anaweza kukupa mume wa kwako. Na ukimpata utabaki kumshukuru Mungu maisha yako yote hapa Duniani.

Rejea: Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma. Yakobo 5:11.

Bila shaka unafahamu habari za Ayubu, hata kama hujasoma kitabu cha Ayubu, utakuwa umesikia watumishi wa Mungu wakihubiri/wakifundisha habari zake. Ayubu alipita katika kipindi kigumu sana, lakini kilichomsaidia ni subira yake, na mwisho wa Ayubu ulikuwa mzuri sana.

Heri usubiri dada yangu, maana Mungu anajua hitaji lako, kama anajua hitaji lako na wewe ni mwaminifu kwake, lazima akupe haja ya moyo wako. Hakikisha huondoki kwake, imani yako kwa Mungu inapaswa kubaki pale pale, mwamini Mungu siku zote.

Na haijalishi umefiwa na mume wako siku nyingi, kama hitaji lako ni kuolewa tena, endelea kumwamini Mungu, atamleta mume wako atakayeweza kuendana na wewe mjane. Na utamfurahia na huyo mwanaume atakayemleta kwako.

Kama ulikuwa umevunjika moyo wako, Yesu Kristo akurejeshe tena kwa upya, uwe na tumaini jipya ndani yako, ukiwa unajua ipo siku yaja Mungu atakukutanisha na mume wako. Atakapokuja mume wako, hutokuwa na mashaka naye, amani ya Kristo ndani ya moyo wako itakuambia. Tena huyo mwanaume atakapokuja kwako hatakuwa na konakona zozote, atakuwa amenyooka kwenye lengo, maana ameletwa na Yesu mwenyewe.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
+255759808081
www.chapeotz.com